SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya pili)


Hatutaki uhasama wala vita tena katika nchi hii… hivyo atakayekwenda huko aende kutatua matatizo kwa njia ya Amani.” Mfalme alikohoa kidogo kisha akaendele kuzungumza kwa sauti kubwa zaidi,
            “Kama mjuavyo chombo chetu cha masafa ya mbali huwa hakiwezi kupandwa na mtu mzima ila mtoto mdogo tu kwa sababu ya nguvu ya mvutano ya Dunia, hivyo anatakiwa apatikane mtoto mdogo asiyezidi miaka 15 na asiyepungua miaka minane…”
Kabla mfalme hajaendelea kuzungumza, nilipaaza sauti huku nikisogea mahala aliposimama,
            “Mimi Nkenye, nitakwenda Vumu kuusaka mwezi, nina umri wa miaka tisa, nimekuwa nikifanya kazi ya kuusafisha mwezi pale unapochafuka na kutoa mwanga hafifu, pia mimi ni mtoto wa shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya anga kwa kipande cha sindano butu!”
Umati mzima ulinishangilia, mfalme akanikumbatia, bila shaka ni kwa sababu ya ujasiri mkubwa niliouonesha. Watu wote waliamuliwa kuondoka, baba, mama na kaka yangu Mowasha walibaki kunitakia kwa heri ya kuonana! Baba alinisogelea na kuninong’oneza maneno haya,
            “Wewe ni mtoto wa shujaa nenda kaipiganie nchi yako… usitetereke!” nilitikisa kichwa kuashiria kwamba nilikubaliana na maneno yake, kisha aliniachia, mama alinifuata akanikumbatia, hakusema neno, Mowasha alinishika mkono huku akisema,
            “Ukifika huko, nichukulie zeze… nasikia vijitu ni vitaalamu vya kutengeneza vyombo vya muziki!”
            “Ha! Ha! Ha! Nitakuletea…” nilijibu, baada ya hapo mkuu wa usalama akanichukua, ndugu zangu wakaelekea nyumbani.
Mkuu wa usalama alinipeleka mpaka katika chumba maalumu ambacho kiliandaliwa kwa ajili ya kuniaga, humo ndani alikuwamo mfalme na mawaziri wake wote, nilipofika  niliwasalimu kwa heshima kisha nikakaa katika kiti kimojawapo. Mfalme alisimama akaanza kuzungumza.
            “Nkenye, jambo hili ni la haraka sana hivyo hatuna muda wa kupoteza, tumekuita humu kukuaga na kukutakia kila lenye heri katika safari yako, utaondoka sasa hivi kwenda kuusaka mwezi, utapaa na chombo cha Mapandagila214… wewe si mgeni katika kutumia chombo cha masafa ya mbali hivyo tunategemea mafanikio makubwa kutoka kwako.” Mfalme alimaliza, wote wakanipigia makofi kama ishara ya kunitia moyo.
Mfalme na watu wengine wote waliokuwamo waliinuka, wakanipeleka katika uwanja mpana uliokuwa katikati ya jengo la mfalme ambapo hapo ndipo Mapandagila 214 ilihifadhiwa. Mapandagila 214, ilifanana na jabali gumu, ilikuwa kubwa kutosha kukaa mtoto mmoja tu. Kilikuwako chombo kingine cha masafa ya mbali kiliitwa Mapandagila 107. Hiki kiliacha kutumika baada ya kuvumbuliwa Mapandagila 214 ambacho kilikuwa cha kisasa zaidi.

Tulifika na kumkuta binti mfalme aliyeitwa Minza akimalizia kuifuta Vumbi Mapandagila 214. Minza alikuwa na umri sawa na wangu, binti huyu alipenda sana kufanya kazi hata ungemwona usingedhani kwamba alikuwa binti mfalme!

Itaendelea Jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024