Jinsi ya kujibu maswali ya fasihi - riwaya, tamthiliya na ushairi


Jinsi ya kujibu maswali ya fasihi - riwaya, tamthiliya na ushairi

Utangulizi

Kijitabu hiki ni mwongozo wa namna ya kujibu maswali ya tamthiliya, riwaya na ushairi. Mada hii imekuwa ngumu na yenye changamoto kubwa, hapana shaka kuwa kijitabu hiki kitarahisisha ugumu huo.

Katika mtihani wa mwisho wa kidato cha nne, maswali yahusuyo tamthiliya, riwaya na ushairi yanapatikana mwishoni mwa mtihani.

Swali la kitabu linaweza kuwa la kueleza kwa isha fupi au kueleza kwa insha ndefu. Swali la kueleza kwa insha fupi linaweza kusema, "Fananisha kwa kutumia hoja nne wasifu wa ndani wa wahusika Mamantilie na Sekai." Katika makala hii, tunaangazia insha ndefu zenye alama 15 kwa swali moja.

Mwanafunzi atakaye kisoma kijitabu hiki ataweza kujibu maswali ya tamthiliya, ushairi na riwaya.

Kukisoma kitabu hiki ni kumiliki alama 45% za mtihani wa mwisho wa kidato cha nne hata kabla ya kuufanya mtihani wenyewe!

Mwalimu Makoba.

SEHEMU YA KWANZA; USHAIRI

Kama wasemavyo Mlokozi na Kahigi (1982;25), ‘ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.’

Hivyo basi tunaweza kusema kuwa, ushairi ni mpangilio maalumu wa maneno yenye lugha ya picha na ya mkato wenye lengo la kufunza jambo fulani.

SEHEMU KUU KATIKA INSHA YA USHAIRI

i.              Utangulizi
ii.            Kiini
iii.           Hitimisho

UTANGULIZI

Katika utangulizi ni vyema kuzingatia mambo manne muhimu;

i.              Toa maana ya neno uliloulizwa
ii.            Kubali au kataa kauli iliyopo katika swali
iii.           Taja majina ya vitabu utakavyovitumia katika kujibu swali lako. (vitabu viwe viwili na majina yaandikwe kwa herufi kubwa)
iv.           Tambulisha kitabu unachoanza kujibu swali

KIINI

Kiini hupaswa kuwa na hoja tatu, ama kwa wale wenye utajiri wa hoja na kasi ya kuandika basi ukingo wao uwe hoja nne kwa kila kitabu.

Kila hoja inatakiwa iwe na mambo matano muhimu;

i.              Hoja yenyewe
ii.            Jina la shairi linalothibitisha hoja hiyo
iii.           Maelezo ya hoja hiyo
iv.           Nukuu ya shairi. (nukuu itolewe na yule aliyekariri mistari au beti za shairi husika, la, hujakariri basi usidanganye ukapoteza alama hata za ule ukweli ulioueleza)
v.            Onesha uhusiano wa kile ulichokisema na jamii yako. Kwa maana fasihi ni zao la jamii na kujaribu kuitenga na jamii ni kukaanga mawe kwa matarajio ya kula maini!!

HOJA YA KUKARIBISHA KITABU CHA PILI

Hii ndio hutoa taarifa kuwa umehama kitabu cha kwanza na sasa unaingia kitabu kingine, mara nyingi hujengwa kwa maneno kama, sambamba na hayo, fanaka na hayo, kwa kuachana na hayo, n.k nilipokuwa mwanafunzi kwa ngazi uliyopo nilipenda kutumia, sambamba na hayo… sina sababu ya uchaguzi huo ila waweza tumia neno lolote kati ya hayo yaliyoorodheshwa.

HITIMISHO

Huu nu muhtasari wa kile ulichokieleza. Andika hitimisho lako kwa ufupi tu, lugha fasaha yenye kueleweka na epuka porojo na mizunguko isiyokuwa na maana.

Sio vigumu… ni rahisi sana, mfano ufuatao unaelezea zaidi.

Swali la necta mwaka 2013

“Mshairi siku zote hukemea uonevu katika jamii.” Thibitisha kauli hii kwa kutoa hoja tatu kutoka

katika kila diwani kati ya diwani mbili ulizosoma.

JIBU

       Uonevu ni kumfanyia mtu jambo la dhuluma au mateso. Ni kweli kabisa kuwa mshairi siku zote hukemea uonevu katika jamii. Kauli hiyo yaweza kuthibitishwa kwa kutumia diwani mbili, MASHAIRI YA CHEKECHEKA  kilichotungwa na Theobard Mvungi na WASAKATONGE chake Mohammed Seif Khatib.

       Kwa kuanza na MASHAIRI YA CHEKACHEKA tunaona kuwa,

       Mshairi anakemea usaliti. Suala hili linaonekana katika shairi la MASHAIRI YA NGULU. Mshairi anaikemea serikali kwa kushindwa kupeleka huduma za kijamii vijijini na hivyo kufanya maisha ya huko yawe ya tabu. Mshairi anasema,

                                    ‘Ngulu kule kijijini, chanzo cha huyu malenga,
                                     Ngulu katika diwani, kijiji kisichoringa,
                                     Ngulu taringia nini, ni mengi yamenizinga.’

Ni kweli kuwa wanachi hao wamesalitiwa hata hawawezi kuringa. Hata katika jamii yetu vipo vijiji mfano wa Ngulu, vijiji ambavyo vimenyimwa huduma muhimu kama umeme na maji ni vyema visaidiwe.

       Mshairi anakemea matabaka. Suala hili linaonekana katika shairi la UTU UMEKUWA KIMA. Mshairi amejadili kwa kina na kuonesha jinsi ambavyo tabaka tawala linavyowanyanyasa wasionacho. Mshairi anasema,

                                    ‘Yenye miiba ya mkonge,
                                     Kunyang’anyana matonge,
                                     Mwenye nguvu ndiye mtu.’

Mshairi anatamani kuiona jamii ambayo haina matabaka. Hata katika jamii yetu, tabaka la chini linanyanyaswa na tabaka tawala, ni vyema matabaka yakaondolewa.

       Mshairi anakemea uongozi mbaya. Suala hili linaonekana katika shairi la TUAMBAE UKASUKU. Mshairi anawashauri wasanii wote waungane ili wakemee uongozi mbaya. Mshairi anasema,

                                   ‘Beti kali tuzitunge, ziwakate wahujumu,
                                    Zikemee hata wabunge, wazembe tuwahukumu,
                                    Wabunge waote meno, wasivirambe viatu.’

uongozi mbaya ni chanzo cha maovu yote. Hata katika jamii yetu uongozi mbaya upo, athari zake ni kuongezeka kwa umasikini, ni vyema uongozi mbaya uondolewe.

       Sambamba na hayo, kwa kutumia diwani ya WASAKATONGE, tunaona kuwa,

       Mshairi anakemea rushwa. Suala hili linaonekana katika shairi la MVUJA JASHO. Mtu wa chini ananyanyaswa kwa kuombwa rushwa katika kila jambo na kumcheleweshea maendeleo. Mshairi anasema,

                                 ‘Rushwa imezagaa,
                                  Uozo ulojaa,
                                  Hakuna manufaa.’

wananchi hawapati manufaa ya jasho lao kwa sababu ya rushwa. Katika jamii yetu rushwa ipo na imeendelea kuwa adui wa haki, ni wakati sasa wa kuungana pamoja na kuipinga rushwa.

       Mshairi anakemea ukeketaji wa mwanamke. Suala hili linaonekana katika shairi la TOHARA. Mshairi anashauri kuepukana na ngariba kwani wao ndio vinara wa ukeketaji wanawake. Mshairi anasema,

                                   ‘Epuka hao ngariba, wajuaji,
                                    Hufika navyo viroba, wachinjaji,
                                    kumbuka hawana tiba, wauaji…’

Mshairi hakubaliani kabisa na suala la ukeketaji wa mwanamke. Katika jamii yetu ukeketaji wa mwanamke bado unaendelea, suala hili limesababisha vifo vya wanawake wengi. Ni wakati sasa jamii inatakiwa kuachana na mila hii mbaya.

      Mshairi anakemea manyanyaso wanayofanyiwa wanachi wa kawaida. Suala hili linaonekana katika shairi la KOSA? Wananchi wananyanyaswa bila kosa lolote la msingi, mshairi anasema,

                                    ‘msitunyanyase,
                                     sio watwana,
                                     watu wa mana,
                                      tuloungana…’

       wananchi wananyanyaswa kwa sababu ya kudai haki zao. Jambo hili halikubaliki. Hata katika jamii yetu manyanyaso yapo ya kila aina, ni vyema wananchi wakaheshimiwa na kuacha kunyanyaswa hasa pale wanapojitokeza kudai haki zao.

Hivyo ndivyo mshairi alivyokemea uonevu katika jamii. Mambo yanayokemewa na mshairi yakifanyiwa kazi kwa kuyaondoa yale yasiyofaa, jamii mpya yenye misingi ya ubinadamu itapatikana na kuifanya Dunia iwe mahali salama.

SEHEMU YA PILI; RIWAYA NA TAMTHILIYA

Maswali ya riwaya na tamthiliya hujibiwa kwa muundo wa aina moja. Hakikisha kwamba kabla hujajibu swali la riwaya au tamthiliya uwe umelielewa, lazima uelewe swali linataka nini, baadaye uwe na uelewa wa jinsi ya kulijibu swali hilo.

Insha yako ya riwaya au tamthiliya inatakiwa iwe na sehemu sita muhimu kama zifuatazo;
1.    Utangulizi

Mambo muhimu ya kuzingatia katika kipengele hiki ni;

-          Toa maana ya kitu unachotakiwa kujibu

-          Kubali au kataa ukweli wa kauli iliyotolewa

-          Toa ushahidi wa kukubali au kukataa kwa kutumia vitabu viwili

-          Majina ya vitabu yaandikwe kwa herufi kubwa na yaandikwapo kwa herufi ndogo basi yapigiwe msitari.

2.    Aya ya kutambulisha kitabu cha kwanza

3.    Toa hoja za kitabu cha kwanza

-          Zingatia kuwa kila aya angalau iwe na mistari mitano tu. Ikizidi basi iwe saba au nane.
-          Waweza tumia aya tatu au nne kwa kitabu kimoja

-          Epuka kutoa maelezo mengi kupita kiasi na lugha za mizunguko

4.    Aya ya kukaribisha kitabu cha pili. Maneno yatumiwayo ni, pamoja na hayo, sambamba na hayo, vilevile n.k

5.    Hoja za kitabu cha pili

6.    Hitimisho

Kwa vile fasihi ni zao la jamii basi haina budi majibu yako ukayahusisha na jamii.

Mfano wa kwanza; swali la riwaya

Swali la necta mwaka 2013


“Fasihi ni chuo cha kufundisha maisha kwa jamii husika. “Jadili ukweli wa kauli hii kwa kutoa hoja tatu kwa kila riwaya kati ya riwaya mbili ulizosoma.

JIBU

       Fasihi ni sanaa ambayo hutumia lugha kufikisha ujumbe wake. Ni kweli kabisa kuwa, fasihi ni chuo cha kufundisha maisha kwa jamii husika. Kauli hii yaweza kuthibitishwa kwa kutumia riwaya mbili, WATOTO WA MAMAN’TILIE yake Emmanuel Mbogo na TAKADINI iliyotungwa na Ben J Hanson.

      Kwa kuanza na riwaya ya WATOTO WA MAMAN’TILIE, kauli hii inathibitishwa,

      Fasihi inatufundisha kuwa ulevi si jambo jema. Mzee Lomolomo ni mlevi mtiifu, pesa yake yote iliishia kwenye pombe. Ulevi ndio unamfanya mzee huyu ashindwe kusomesha watoto wake na kujikuta wakifukuzwa shule. Madhara ya ulevi yanaonekana zaidi pale anapokunywa pombe zilizokwesha muda wake na kumsababishia kifo. Katika jamii yetu ulevi umekithiri, watu wanaokunywa pombe muda wa kazi ni mfano tosha, ulevi utokomezwe kwani ni chanzo cha umasikini.

       Fasihi inatufundisha kuwa watoto wasifukuzwe shule kwa kukosa ada. Watoto Zita, Pita na Musa wanafukuzwa shule kwa kukosa ada, kufukuzwa kwao kunawafanya wakose mwelekeo, Musa na Pita wanajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya na kuwafanya wakamatwe na polisi. Katika jamii yetu mambo yamerekebishwa kiasi kuwafanya watu wote wapate elimu bora bila kulipia kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Ni vyema pia huduma mbalimbali zikiboreshwa zaidi ili kutoa elimu bora.

       Fasihi inatufundisha kuwa rushwa ni adui wa haki. Mamant’ilie anashindwa kupiga hatua katika biashara yake ya kuuza chakula kwa sababu mgambo wa jiji walichukua rushwa kwake kila siku. Faida yote ya Mamant’ilie inaishia mikononi mwa mgambo na kumfanya ashindwe hata kusomesha watoto wake. Katika jamii yetu rushwa ipo, bila kutoa rushwa huwezi kuhudumiwa, ni vyema vyombo vilivyopewa dhamana ya kupambana na rushwa vikaongeza bidii ili kutokomeza uovu huu.

       Sambamba na hayo kwa kutumia riwaya ya TAKADINI, kauli hii inathibitishwa kama ifuatavyo,

       Fasihi inatufundisha kuwa walemavu wanaweza kufanya mambo makubwa na muhimu katika jamii kama walivyo watu wengine. Takadini pamoja na ulemavu wake aliweza kufanya mambo mengi kama kuimba, kupiga mbira, kutibu watu na mambo mengine mengi yaliyowashangaza watu waliowanyanyasa walemavu. Katika jamii yetu walemavu wakipewa nafasi wanaweza kufanya mambo makubwa ya kuisaidia jamii. Pia wapo walemavu wa ngozi ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali kwa mafanikio makubwa.

       Fasihi inatufundisha kuwa baadhi ya mila zimepitwa na wakati na hazifai kuendelea kutumiwa. Miongoni mwa mila hizo ni zile zinazowataka walemavu wauawe. Takadini ananusurika kuuawa lakini ujasiri wa mama yake unamsaidia. Jamii yetu imekuwa na Tamaduni ya kuwaficha na kuwatenga watu wenye ulemavu, pia watu wenye ulemavu wa ngozi wanakabiliwa na wimbi kubwa la mauji ambapo wauaji wanaamini kuwa viungo vyao vinaweza kutumika kuwapatia utajiri. Hii ni imani potofu na inabidi kutokomezwa kwa nguvu zote.

       Fasihi inatufundisha kuwa ndoa ni makubaliano ya watu wawili na haipaswi kuingiliwa na mtu yeyote. Takadini anapendana na Shingai lakini wazazi wake Shingai hawakubaliani na jambo hilo kwa sababu tu Takadini ni mlemavu wa ngozi. Pamoja na pingamizi la wazazi Shingai anashikilia msimamo wake na wanapata mtoto asiyekuwa na ulemavu wa aina yoyote. Wapo wazazi katika jamii yetu ambao wamejaribu kuingilia mahusiano ya watoto wao na kuwaharibia maisha. Jambo hili halikubaliki na ni kinyume na haki za binadamu.

      Hivyo ndivyo fasihi ilivyotumika kufundisha maisha kwa jamii. Mafundisho yaliyopo katika fasihi yana umuhimu mkubwa katika ujenzi wa jamii mpya hivyo ni vyema kwa wanajamii kuyafuata mafunzo hayo yenye mchango chanya.

Mfano wa mwanafunzi aliyejibu swali la riwaya NECTA



Mfano wa pili; swali la tamthiliya

Swali la necta mwaka 2008


 “Waandishi wengi huandika kazi zao kwa lengo la kutoa ujumbe katika jamii”. Kwa kutumia tamthiliya mbili (2) zilizoorodheshwa, thibitisha ukweli wa kauli hii.

JIBU

       Ujumbe ni funzo linalopatikana katika kazi ya fasihi. Ni kweli kabisa kuwa waandishi wengi huandika kazi zao kwa lengo la kutoa ujumbe katika jamii. Kauli hii inaweza kuthibitishwa kwa kutumia tamthiliya mbili, KILIO CHETU chao Medical Aid Foundation na NGOSWE – PENZI KITOVU CHA UZEMBE kilichoandikwa na Edwin Semzaba.

       Kwa kuanza na tamthiliya ya KILIO CHETU inathibitishwa kuwa,

       Mwandishi anatoa ujumbe kuwa elimu ya ujinsia na mahusiano itolewe kwa watoto. Elimu hii ni muhimu na inahitajika sana kuwakomboa watoto dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Tunamuona Suzi na Joti wakiwa hawana elimu ya jinsia na mahusino, madhara yake ni kwamba, Joti anamwambukiza Suzi virusi vya UKIMWI pia anamsababishia mimba. Pengine wangepewa elimu wasingepatwa na matatizo. Hata katika jamii yetu elimu ya jinsia na mahusiano inahitajika ili iweze kuwaokoa watoto dhidi ya maradhi. Ni vyema kuachana na ukale unaopiga vita elimu hii.

       Mwandishi anatoa ujumbe kuwa sayansi na teknolojia itumiwe kwa uangalifu kwani inaweza kuwaathiri watoto. Joti, Chogo, Jumbe na Mwarami wanaangalia mikanda ya ngono bila kuwa na hofu yoyote. Uangaliaji wa picha hizi unawafanya watamani kuyafanya yale wayaonayo. Suala hili linahatarisha elimu na maisha yao. Hata katika jamii yetu ni vyema watoto wakasimamiwa na wazazi wao katika vipindi waangaliavyo katika televisheni. Watoto waangalie vipindi ambavyo vitawasaidia kukua katika maadili mema.

      Mwandishi anatoa ujumbe kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Joti ni mhusika ambaye hakufunzwa vyema na wazazi wake badala yake anaadabishwa na dunia. Kulingana na mienendo mibaya ya kijana huyu kama vile kutembea na wanawake waliomzidi umri, anaambukizwa virusi vya UKIMWI na kupelekea kifo chake. Katika jamii yetu watoto aina ya Joti wapo, hivyo wazazi wanatakiwa wawafunze vyema watoto wao, elimu pekee wanayotakiwa kuwapa ni elimu ya jinsia na mahusiano.

       Sambamba na hayo, kwa kutumia tamthiliya ya NGOSWE – PENZI KITOVU CHA UZEMBE, kauli hii inathibitishwa,

       Mwandishi anatoa ujumbe kuwa tusichanganye mapenzi na kazi. Ngoswe anamtamani mtoto wa Mzee Mitomingi na kusahau kazi ya kuhesabu watu iliyompeleka, anajaribu kutoroka na Mazoea lakini anasahau makaratasi ya sensa ambayo yanachomwa na Mzee Mitomingi na kuifanya hesabu iharibike. Katika jamii yetu watu wanaoendekeza mapenzi badala ya kazi wapo, suala hili linarudisha nyuma maendeleo kwani kazi hazifanyiki kwa ufanisi. Ni vyema kutofautisha kati ya muda wa kazi na muda wa mapenzi.

       Mwandishi anatoa ujumbe kuwa hasira ni hasara. Mzee Mitomingi anafanya maamuzi akiwa na hasira. Maamuzi ya kuyachoma moto makaratasi ya sensa yanasababisha hasara kubwa kwa serikali na wananchi, kwani lengo la watu kuhesabiwa ni kuirahisishia serikali upangaji wa maendeleo katika nchi yake. Katika jamii yetu hasara kubwa zimetokea kwa sababu ya watu waliojaribu kufanya maamuzi wakiwa na hasira, watu wengi wamejikuta wakiua kwa sababu ya hasira na hasira zilipokwisha wakaanza kujuta. Kama mtu anahasira, basi asifanye maamuzi yoyote.

       Mwandishi anatoa ujumbe kuwa suala la malezi lihusishe wazazi wote wawili. Katika jamii ya Mitomingi, wanawake ndio wanapewa jukumu la malezi ya watoto wao. Mazoea anapotoroshwa na Ngoswe Mzee Mitomingi anawalaumu wake zake kwa kushindwa kuchukua hatua. Katika jamii yetu suala hili lipo kwa kiasi kikubwa. Mama peke yake kuachiwa mzigo wa malezi kumesababisha jamii yetu iwe na watoto ambao hawana maadili sawasawa. Ni vyema suala la malezi likahusisha wazazi wote wawili kama wapo.

       Waandishi huandika kazi zao kwa lengo la kuifundisha jamii. Ni jukumu la wanajamii kuyafuata mafunzo hayo ili kusaidia katika ukombozi wa jamii. Ni dhahiri kuwa mengi yasemwayo na waandishi huwa na malengo ya kuikomboa jamii.

Mfano wa mwanafunzi aliyejibu swali la Tamthiliya NECTA




MAREJEO
E. Mbogo.(2002). Watoto Wa Maman’tilie. Heko publishers: Dar es salaam
B. Hanson. (2004). Takadini. Methew book store: Harare, Zimbabwe
Medical Aid Foundation. (1995). Kilio Chetu. Tanzania publishing house: Dar es salaam
Marejeo mengine ni
Kitabu cha Ngoswe - penzi kitovu cha uzembe
Mashairi ya chekacheka
Wasakatonge

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Notes za Kiswahili Kidato cha Pili | Form Two

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2025