RIWAYA YA TAHARUKI (mwanzo mpaka mwisho)



RIWAYA – TAHARUKI
MTUNZI – DAUD MAKOBA
0754 89 53 21

SURA YA KWANZA

Mako, mwosha magari maarufu mtaani Sakubimbi, alishughulika kama kawaida yake. Leo alionekana kuchoka zaidi, pengine tenda ya kuosha Fuso, ilimnyong’onyeza vilivyo. Mwanaume huyu alikuwa na mwili wa wastani tu, kakamavu aliyezifikia kilo 61 kwenye uzani.

Wakati akiendelea kuosha Fuso ile, jua liliendelea kuipiga ngozi yake, naye hakuisha kushika nywele, kipilipili kilichokoza, ngumu zimerundikana na kutengeneza kitu kama mkutano wa nzi, labda hazikuliona chanuo kwa muda!

Fuso sasa ilitakata haswaa, Mako akatembea mpaka alipo mwajiri wake, akachukua fedha na kuzielekeza kibindoni, kabla hazijafika akastushwa na sauti yenye kitetemeshi cha kuigiza,
“Uko chini ya ulinzi, toa fedha uishi…”

Mako akabinua bichwa ili apate kumtazama aliyetema maneno hayo,macho yake yakagongana na sura ya mtoto mdogo, umri miaka saba, kavaa sare za shule na begi dogo kalipachika mgongoni, kisha akambeba kindakindaki. Kwa ambae angewaona hata kama angekuwa mgeni eneo hilo ni lazima angegundua kuwa viumbe wale walikuwa ni mtu na mwanae. Nkenye alifanana mno na baba yake, hasa zile nywele, kipilipili kilichokoza. Majirani walisema Nkenye alijaa urumbi wa maneno kama babaye.

Baba akamrusha mwana juu, kisha akamshusha chini. Hakutaka kumuuliza habari za shule, akaagana na wafanyakazi wenzake, kwa vile magharibi ilikwisha anza kuingia, akaikamata njia ya kuelekea nyumbani., Nkenye akifuata nyuma kama mkia.

Mako alipanga chumba kimoja na sebule katika mtaa wa Sakubimbi, mahali walipoishi makabwela. Nyumba yenyewe ilikuwa chakavu mithili ya tambala la deki, kwanza iliezekwa mabati chakavu, bila shaka kila mvua iliponyesha wakazi hawa walilowa vilivyo. Mwisho nyumba hii ilizungukwa na jalala kubwa la taka upande wa mashariki na kila upepo ulipovuma, pua zao zilijuta kunusa. Baba na mwana walifika nyumbani, sebuleni walimkuta mama Nkenye kashughulika kwelikweli, yuko kimya anampara samaki mkubwa.

“Leo samaki?” aliuliza Mako kisha akavuta kiti cha plastiki akakaa kivivu.

“Unauliza jibu!” alijibu mama Nkenye, mdomo kaubetua kama anayetaka kupiga chafya.
“Mpige atakuzoea!” alishauri Nkenye, baba yake akamshika mkono kwa nguvu kisha akaamuru,
“Haya kimbia chumbani, kabadili nguo za shule… panya weeeh!”

Nkenye alitii amri, haikupita sekunde, alitoweka sebuleni na kuzama chumbani.

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya utani tu ya wanandoa hawa, katika uhalisia walipendana sana, maisha yao ya chini hayakushusha morari wa mapenzi. Nafsi zao zilizungumza lugha moja. Majirani walipogombana, kwao mambo yalikuwa tofauti, ndo kwanza walikula wakanywa, wakashiba.

SURA YA PILI

Kama ilivyo kawaida yake, jioni ya siku ile Mako alikwishamaliza kazi zake za kuosha magari. Alionekana akitabasamu muda wote kwani siku hii alipata kuosha magari mengi zaidi kibindo chake kikatuna.

Lakini ghafla tabasamu lake lilikatika, wasiwasi ukamjaa, kwa sababu ilikuwa ni kawaida kwa mwanaye Nkenye kupita pale kila siku atokapo shule. Sasa ilikuwa saa kumi na moja jioni, mtoto hakuonekana!

Wazo kubwa lililomjia kichwani, ni kwamba, pengine Nkenye alipitiliza moja kwa moja nyumbani hasa ukizingatia usiku wa jana palipikwa wali na samaki aliyenona, hivyo pengine mtoto huyo alikwenda kumalizia kiporo. Mako akili ikachemka, akachukua simu yake ya kupapasa haraka sana akampigia mkewe.

“Hallo!” Upande wa pili uliitika.

“Vipi? Nkenye kafika huko?”

“Bado sijamuona, wewe si…” Hakumaliza kuongea, Mako alikata simu.

Masaa yalizidi kukatika, Nkenye hakuonekana nyumbani, wazazi wawili wakajawa na wasiwasi usiokuwa na kipimo. Mako alikunja uso wake, ukatengeneza vitu kama matuta, akatafakari kwa kina, kisha akamtazama mkewe, mrembo haswaa, rangi yake maji ya kunde, shavu dodo, kapewa nyama kiasi hata alipokaa hakukalia mifupa. Mwanamama huyu naye kanyamaza kimya mawazo yamemjaa.
“Mi naona tutoke nje tukamtafute huyu mtoto.” Mako alivunja ukimya, kabla mkewe hajajibu, akaingia msichana mnene kama kiboko, yuko mbiombio,
majasho yanamtoka kalowa utadhani kanyeshewa mvua, lakini kwa bahati mbaya msichana huyu kabla hajasimama kusema chochote, akateleza, kikasikika kishindo kikubwa, pembeni ya miguu ya Mako. Mako akamnyanyua haraka kisha akamketisha katika kiti kikubwa kilichokuwa pembeni na kusema kwa sauti,

“Vipi Pamela, mbona mbiombio?”

“Nkenye kagongwa gari… yuko hospitali ya Mando!”

Habari ile iliiripua mioyo ya wanandoa wale, haraka wakajiandaa, maandalizi yalipokamilika, watu hawa watatu walitoka, Zena binti wa miaka 20 akashika njia ya kuelekea nyumbani kwao. Mako na mkewe wakashika njia ya kuelekea hospitali ya Mando alikolazwa Nkenye, mtoto pekee waliyejaaliwa kumpata katika miaka tisa waliyodumu katika ndoa yao!

xx xx xx
Mako na mkewe walikuwa ndani ya ofisi ya daktari bingwa. Daktari kama kawaida yake alivaa koti kubwa jeupe, shingoni kapachika kifaa cha kupimia mapigo ya moyo. Wote watatu katika ofisi hii walikaa katika viti vilivyopendezeshwa kwa rangi ya hudhurungi, daktari yuko mbele, Mako na mkewe wamekaa mkao wa kutazamana lakini hawakutazamana, walimtazama daktari.
“Wewe ndiye baba wa huyu mtoto?” Daktari alivunja ukimya.
“Ndiyo!” Alijibu Mako, wasiwasi umemjaa.
“Na wewe ndiye mama bila shaka?” Daktari aliuliza akimtazama mama Nkenye.
“Ndiyo!”
“Aaah… hali ya mgonjwa wenu, ni mbaya sana hii imesababisha hata tusiwaruhusu kumuona, lakini bado tunajaribu kuokoa maisha yake… kapata ajali mbaya sana na ameumia mno kichwani, mpaka sasa tumeshindwa kurejesha fahamu zake… hivyo mtoto wenu anahitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa… milioni 15 zinahitajika mtoto akatibiwe India!”
“milioni 15?... Za kitanzania?” Mako aliuliza macho kayatoa pima.
“Ndiyo za kitanzania!” alijibu daktari kisha akaendelea, “Tena ni vyema fedha hizo zipatikane ndani ya siku tatu, vinginevyo tunaweza kumpoteza mtoto huyu.

Mako akaishiwa nguvu, akamtazama mkewe, mashavu ya mama Nkenye yaliyojaa kama embe dodo bivu, yalilowa kwa machozi, michirizi ikachoreka mpaka kidevuni. Mako kwa ujasiri mkubwa, akamshika mkono mkewe kisha akamnyanyua na kumueleza,

“Nitapata fedha hizo, usilie, nyanyuka twende nyumbani!” kisha akamgeukia daktari, akaendelea kusema,

“Asante sana dokta, nitakuja na hizo milioni 15 kabla ya siku tatu.” Kisha haraka akamvuta mkewe, akafungua mlango na kwenda naye nje.

Zilikuwa ndoto za asubuhi kwa mwosha magari Mako kuzipata milioni 15, kijana mdogo tu mwenye miaka 23, lakini aliyejipachika jukumu kubwa la kuwa na familia aliahidi haswaa pasipokujua angetumia njia ipi. Machozi na huzuni ya mkewe ndivyo vilimfanya atoe jibu hilo la faraja! Lakini jambo kubwa, Mako hakuwahi kuruhusu kushindwa katika maisha yake, mwanae kufa kwa sababu ya ukosefu wa fedha kulikuwa ni kushindwa. Mako asingekubali!

SURA YA TATU

Mako aliamka asubuhi sana, akamtazama mkewe , jicho la mama Nkenye lilikuwa kavu, pia liliashiria kutokulala kwa masaa kadhaa.

“Lala sasa!” Alishauri Mako.
“Hakuna usingizi… mwanangu anakufa!” Alilalama mama Nkenye.

“Laiti kama ningemkamata aliyemgonga mwanangu, ningemchoma yeye na gari lake… ana bahati alikimbia kabla sijafika!”

“Mungu atamlipa… malipo yote ni hapahapa duniani.”
“Usijali mke wangu, leo ng’ombe wa masikini atazaa. Nakwenda kutafuta fedha.”
Mama Nkenye alisikia maneno hayo, akatoa tabasamu la huzuni, alijua wazi kuwa mumewe asingeweza kupata kiasi hicho cha fedha, lakini hakutaka kumkatisha tama, akamweleza kwa upole,
“Katafute mume wangu, nami ifikapo saa nne asubuhi, nitakwenda hospitali nikaone kinachoendelea.”

Mako hakujibu, alikwisha vaa viatu vyake, shati kubwa na suruali chupa, hakukumbuka kuchana nywele – kipilipili kilichokolea! Kisha huyoo akaelekea nje, kutafuta milioni kumi na tano za kitanzania. (KICHEKO)!

XX XX XX

Mako alizunguka mjini Takayungu, alikwishautoka mtaa wa Sakubimbi, mbele kidogo ya kijia kidogo akaona nguzo ya umeme ambayo iligongelewa bango lililoyavutia macho yake, hakusita akalisoma taratibu,

“MGANGA TOKA SHINYANGA, TUNAONGEZA AKILI ZA DARASANI, TUNATOA PETE YA BAHATI, TUNATOA FEDHA ZA MAJINI NA TUNAUNGANISHA WATU FR…” Mako hakuendelea kusoma, alisonya msonyo mrefu kisha akamlaani aliyeandika bango hilo la kitapeli.haraka akakaza nyonga, mbele akasonga!.

Saa nane kamili mchana ilifika, jua liliwaka vilivyo, Mako aliyetembea mwendo mrefu usio na mafanikio, aliloa majasho mwili mzima. Asingeweza tena kutembea, akajisogeza karibu na kibanda cha mpemba mmoja, akatoa fedha aliyoisindikiza kwa maelekezo. Haukupita muda, mpemba alimpatia mteja wake andazi moja kubwa na maji mengi yaliyofungwa kwenye kifuko cheupe, naye Mako akiisha kuvipokea, akaketi katika ‘benchi’ lililokuwa pembeni mwa mlango wa duka la mpemba. Hapo akatafuna haraka andazi lake kisha akalisindikiza kwa maji baridi. Roho yake ikaburudika kiasi.

“Nipatie vocha!” Aliagiza tena Mako. Mpemba akatii.
“Wacha nitalii kidogo katika mitandao ya kijamii, siku haiendi, mafanikio hakuna!” Alijisemea, shingo kaipinda, anakwangua vocha.
Saa moja na dakika hamsini usiku, mama Nkenye alikaa juu ya mlango wa nyumba aliyoishi, kwa mbali akamuona mumewe akirudi. Anatembea kivivu, mikono kaipachika kichwani, kachoka kama punda!

“Za hapa!” Aliuliza Mako baada ya kufika alipokaa mkewe.
“Mbaya sana… vipi fedha imepatikana?”
“Hapana lakini haina maana kuwa haitapatikana.”
“Mmmh… Haya lakini siku ya kwanza ndo hii imeisha!”

Mako akastushwa kidogo na jibu hilo, akamkamata mkono mkewe wakaingia ndani.
Siku ya pili Mako aliamka asubuhi zaidi, hakuaga, aliondoka kimyakimya, mavazi yake yaleyale, shati kubwa, suruali chupa na kiatu kirefu. Alikwenda moja kwa moja mpaka kwa rafiki yake Blonko, hapo akaazima pikipiki aina ya ‘Boxer’ na kutokomea nayo mtaani.

Mako alikimbiza pikipiki kwa mwendo wa wastani, akaiingia barabara kubwa ya Sarawi, baada ya muda mfupi, akakunja kushoto, akavuta mafuta, akaongeza gia mpaka alipofika karibu na geti kubwa lililoandikwa ‘RADIO HURUMA’ akasimama na kusababisha vumbi jingi litimke.

Aliegesha pikipiki kisha akatembea mpaka kwenye geti na kuanza kugonga, haukupita muda, mlinzi alifungua geti.

“Karibu una shida gani?” Alihoji mlinzi, macho kayakaza.

“Samahani naomba kuonana na mtangazaji wa kipindi cha ‘Msaada wako’… mwanangu mgonjwa, nahitaji kuchangiwa na wananchi.”

“oooh… pole sana!” Alijibu mlinzi kwa sauti ya chini, kisha akaendelea, “Watu wengi wana matatizo, kuna zaidi ya watu 50 wanasubiri kueleza matatizo yao na kama unavyojua kipindi hiki kinaruka mara moja tu kwa wiki…” Kabla mlinzi hajamaliza kuzungumza, Mako aliondoka kinyonge, kichwa chini, kakata tama, polepole akawasha pikipiki na kuendesha kwa mwendo wa taratibu.

Aliendesha pikpiki kwa mwendo kasi wa kilomita ishirini kwa saa, alikuwa mnyonge mwenye mawazo mengi, kubwa zaidi alikata tama, hakuwa na tumaini jingine, alikwishajisalimisha na aliukubali ukweli kuwa asingeweza kupata milioni 15 kwa matibabu ya mwanaye pekee aliyempenda.

Lakini ghafla alistuka baada ya kuona gari dogo jeupe likija kwa kasi, haraka akakwepa na kudondoka kwenye mtaro, kabla hajanyanyuka, gari aina ya ‘Defender’ ilipita kwa kasi pia, ikiifukuzia ile gari ndogo nyeupe. Defender imejaa askari imara waliobeba bunduki aina ya ‘SMG’ fupi za kichina. Bila shaka askari hawa watiifu, walifukuza majambazi.

Haraka Mako akainyanyua pikipiki yake, akapiga ‘kiki’ moja, ikaunguruma kama chui, akatia gia, akavuta mafuta, akatia gia tena na tena, akavuta mafuta, pikipiki ikatembea kwa mwendo kasi wa kilometa115 kwa saa!

Barabara ikapendeza kwelikweli, mbele gari dogo jeupe lililobeba majambazi, katikati gari la polisi, nyuma yupo Mako ambaye hata hivyo haikujulikana alimfukuza nani na kwa nini alivamia ugomvi ule usiomhusu!

Katika mfukuzano ule, hali ilibadilika, askari wakaanza kupiga risasi gari la majambazi, majambazi yakajibu, risasi zikarushwa mfululizo, wema na ubaya ukapambana!

Mako alilikaribia kabisa gari la askari, askari wakashangazwa na mtu huyo, Mako hakujali, akatoa ishara ya kuwaomba wampishe ili aifukuze gari ya majambazi! Askari mmoja akamfokea.
“Acha ujinga dereva bodaboda, hatuchezi tunafukuza majambazi toka utakufa!”

“Majambazi yanaelekea kuwaacha, nipisheni nikawakamate, nipeni njia!” Alilalama Mako, sura kaikunja kwa hasira, lakini kabla hajajipenyeza kunako njia, askari mmoja akamfyatulia risasi, ikavunja ‘side mirror’ pikipiki ikayumba lakini haikudondoka! Sasa Mako akaanza kulifuata gari la askari kwa tahadhali kubwa.

Katika kitu ambacho hakikutarajiwa na askari ni risasi ambayo ilipigwa katika gurudumu la mbele, gari ikayumba kisha ikaacha njia na kupinduka vibaya. Roho tatu za askari zikatoka palepale! Waliopona mifupa yao ikabaki nyang’anyang’a, majambazi yakafurahia ushindi, yakarukaruka ndani ya gari kama makinda ya ndege na kumpongeza mdunguaji aliyewaondoa askari katika njia.
Lakini majambazi wakiendelea na furaha ya ushindi, wakastushwa na mlio wa pikipiki iliyokuwa inakuja kwa kasi.

“Nani tena huyo?”

“Huyo nadhani yuko pamoja na wale askari, nilimuona akiwa ametutega njiani, nikataka kumgonga, akakwepa na kutumbukia kwenye mtaro, sasa kakifuata kifo… shambuliaa!” Dereva alitoa amri, risasi zikamiminwa uelekeo wa Mako.

Mako alipata wakati mgumu, risasi zilikuja mfululizo, akalala kifudifudi juu ya pikipiki, mikono imeshika usukani, kichwa mbele! Hakukata tamaa, japo alijawa hofu kiasi!

Mfukuzano uliendelea, majambazi yanafyatua risasi kama mvua, Mako hashambulii anakwepa na kuwafukuza. Dereva wa majambazi akazidi kuongeza mwendo, akakimbia kilomita 127 kwa saa. Barabara ikaanza kupata kona, kona ya
kwanza akapita, kona ya pili akapita ila gari likalala kidogo, kona ya tatu gari likayumba, kona ya nne gari likaacha njia kisha likagonga mti mkubwa wa mbuyu. Ni ajabu kama majambazi haya yangepona!

Haraka Mako akakanyaga breki baada ya kupangua gia, akaacha njia na kulifuata gari la majambazi ambalo halikutamanika! Alipofika akachungulia ndani, jambazi moja lilikuwa likipumua, akalipiga konde zito ikawa tiketi murua ya kwenda kuzimu. Baada ya hesabu ya muda, akagundua walikuwa majambazi wanne, wote walitulia kimya, damu ikiwavuja sababu ya ile ajali mbaya.

Kitu kimoja kikamvutia Mako, ulikuwa mfuko mkubwa mweusi, akauchukua haraka kisha akaufungua, hakuamini alichokiona, noti nyekundu zilijazana katika fuko hilo, hapo akagundua kwa vyovyote wale walikuwa ni majambazi waliotoka kuiba popote pale huenda ikawa benki!

Ilikuwa yapata saa kumi na nusu jioni saa za Afrika ya mashariki! Mako akalichukua lile fuko la fedha, akapanda pikipiki yake na kutokomea barabarani.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Mako alitulia tuli katika chumba kidogo kilichokuwa na mwanga hafifu, alikwisha hesabu fedha yote aliyochukua toka kwa majambazi wale asiowafahamu! Alizipanga vyema katika sanduku kubwa la mbao, shilingi milioni mia moja kamili za kitanzania. Kabla hajafanya lolote, akachukua simu yake ya kupapasa, akaiwasha, akatazama muda, ilikuwa saa tisa usiku. Akaamua kupitia katika ‘blogi’ mbalimbali ili aone taarifa zinasemaje kuhusu tukio lililotokea, akashangazwa na kichwa cha habari kilichosomeka,

“MAJAMBAZI YAIBA MILIONI 220, BENKI YA MABEPARI.” Mako akasonya kisha akasema kwa sauti ya chini,

“Nchi hii kila mtu anaiba, mabepari wanaiba jasho letu, majambazi wameiba milioni 100 za mabepari, meneja wa benki kaiba milioni 120… muungwana ni mimi tu, nimeokota milioni 100!”
Mako hakuendelea tena kuperuzi katika mitandao, akaamua kumpigia simu mkewe ili kumuondoa hofu.

“Hallo!”

“Hallo mume wangu… muda wote simu yako haipatikani, uko wapi?”
“Hupaswi kujua kwa sasa… kesho nenda kwa Blonko, chukua milioni 30, peleka mtoto India akatibiwe, natumaini hatujachelewa.” Akakata simu bila kusubiri majibu, kisha haraka akaizima. Baada ya muda mfupi, akapitiwa na usingizi, akalala kishujaa!

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Pablo Max Chata, mwanaume mweusi kama kipande cha giza, mrefu azipataye futi sita kamili, mwili imara umejaa misuli, ndevu zake kanyoa kabakisha sharubu za paka, jamaa huyu alikuwa kiongozi mkuu wa kikosi cha majambazi na wahalifu. Tena yasemekana, mshipa wa huruma hakuzaliwa nao kwa jinsi alivyokuwa katili!

Mwanaume huyu alipanda katika ‘lift’ ya hospitali waliyotibiwa watu wazito, pembeni alizungukwa na walinzi wanne, wameshiba misuli, tena wamevaa suti nyeusi naye Chata alivaa suti nyeupe pengine ni kujaribu kujitofautisha na watwana wale.

‘Lift’ ilisimama, Chata na walinzi wake wakatembea kwa mwendo wa haraka, hawakuchelewa, walikwishaingia chumba namba 80 alimolazwa askari Kabengo.

“Karibu Boss.” Alikaribisha Kabengo, mguuni kafungwa plasta ngumu nyeupe, vivyo hivyo kichwani kafungwa plasta na juu zaidi alitundikiwa drip ya maji!

“Nipe habari ninazozitaka haraka… inakuwaje vijana wangu wanapata ajali na fedha yote inaibiwa?” Alifoka Chata.

“Sisi tulipata ajali…” Alizungumza kwa shida Kabengo, akakohoa kisha akaendelea, “Nyuma yetu kuna dereva bodaboda alitufuatilia… baada ya gari letu kuanguka, jamaa aliendelea kuwafukuza vijana wako, kwa bahati mbaya gari ikaacha njia na kugonga mbuyu, nadhani jamaa alitumia nafasi hiyo kupora fedha iliyoporwa na vijana wako.”

“Unamfahamu huyo jamaa?”

“Namfahamu, jamaa ni mwosha magari, lakini sifahamu kazi ya udereva bodaboda kaanza lini… mmh… usijali… nitakutumia ramani nzima na jinsi ya kumpata.”

“Safi!” Alipongeza Chata, kisha bila kuaga akatoka na walinzi wake!

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Ilikuwa asubuhi tulivu siku ya ijumaa, jua lilikuwa bado kuchomoza, mawingu yalirandaranda na kuchezacheza kwa furaha. Ilikuwa asubuhi tulivu sana, vyura hawakupiga kelele, waliufaidi usingizi wa asubuhi!

Asubuhi hiyo , Mako alijibanza pembeni ya mti mkubwa, macho yake kayaelekeza katika barabara ya kuingia uwanja wa ndege - kuna mtu alitamani amuone akipita katika barabara hiyo, ndiyo maana hakupepesa jicho lake.

Baada ya muda mfupi, lilipita gari la wagonjwa likielekea uwanja wa ndege, Mako akachungulia kwa makini, akamuona mkewe kaka kwa matumaini, Mako akafurahi, akalitazama gari lile lililosonga taratibu mpaka lilipopotea machoni kwake.

Masaa mawili yalipita, Mako akiwa mahala palepale alipojificha, mara akaliona dege kubwa likipaa, likapaaa usawa wa juu kiasi kisha likageuka kwa mbwembwe na kuikamata njia ya kuelekea India. Tabasamu pana la Mako likaonekana, matumaini yakarudi, akafurahi, kisha akasimama na kuruka juu kwa madaha, kabla hajatua, akapigwa na kitu kizito kichwani. Akadondoka na kupoteza fahamu.

SURA YA NNE

Fahamu zilimrudia Mako, akajikuta akiwa ndani ya chumba chenye giza, chumba chenyewe kidogo kiasi hakikupitisha hewa sawasawa. Akaanza kukumbuka matukio yaliyopita… kichwani akaliona dege, akajiona akiruka kwa furaha, kisha hakukumbuka kilichofuata.

Aliyahisi maumivu ya kichwa, akatafakari kidogo, kisha akawa na mashaka juu ya Yule aliyemteka alitaka nini? Moja kwa moja aligundua sababu ya yeye kuwa pale ni zile shilingi milioni 100 alizopora kwa majambazi yaliyopora benki iliyopora jasho la wananchi! Hapo akashtuka na kuvuta umakini kwani kitendo cha kuzubaa kingesababisha kifo chake.

Jambo kuu lililomchanganya sasa, ilikuwa ni sehemu ile alimofungiwa. Alitafakari kama mahali pale ni polisi ama ni ngome ya majambazi wenyewe. Taratibu akakitalii chumba kwa jicho lake la kushoto, akagundua uwepo wa tundu dogo ambalo lingemwezesha kuchungulia nje, kabla hajasimama, mlango ulifunguliwa, jamaa mmoja aliyeikamata vyema ‘SMG ‘ akaingia na kumpeleka nje.

Alipelekwa mpaka chumba kingine kilichokuwa na mwanga wa kutosha, akaamuliwa kukaa katika kiti kimojawapo, akaketi taratibu akiwa amejawa hofu kiasi, kisha akatazama mbele ambako walisimama wanaume kadhaa waliojaa misuli. Mwanaume mmoja mwenye umri wa makamo akamsogelea Mako kisha akamnasa kofi moja kali ambalo lilimfanya agugumie kwa maumivu.

“Kijana…” Aliita jamaa Yule, kisha akaendelea, “Naitwa Pablo Max Chata, mtu hatari sana, eleza ulikoficha fedha zangu kabla sijakumaliza.”
“Mzee mbona sikuelewi!?” Alijibu Mako.
“Chinda, njoo umueleweshe.” Aliamuru Chata.
Chinda akasogea, akatoa kisu kikali na kukielekeza zilipo ‘nyeti’ za Mako kisha akafoka,
“Eleza, la sivyo nakugeuza ‘bwabwa’.”
Pengine hakuna kitu alichokithamini Mako katika mwili wake kama sehemu hizo zilizotishiwa kuondolewa. Akajitetea haraka,
“Tafadhali… fedha zenu sikuiba lakini najua zilipo.”
“Vizuri!” Alipongeza Chata ambaye tayari alikwisha msogelea Mako, Chindo akarudi nyuma.
“Sasa waweza nieleza ni wapi zilipo fedha zangu?”
“Lakini mzee, fedha zile vijana waliiba benki, utaziitaje zako?” Aliuliza Mako, Chata akamnasa kofi zito kisha akafoka,
“Unacheza na mimi kijana, eleza wapi ulikoficha fedha!”
“Sawa mzee nasema.” Mako akakohoa, kisha akameza mafunda kadhaa ya mate makavu, akaendelea kuzungumza,
“Wajua gari la vijana wako liligonga mbuyu,… wakafa wote, si mimi niliyewaua, ni ajali na malipo ya ujambazi wao! Nilisogea eneo lile nikagundua uwepo wa mfuko mkubwa wa fedha. Ni nani aisemaye vibaya fedha? Hata wewe Chata unanona kwa sababu ya fedha ya unyang’anyi. Hivyo mimi niling’amua ya kwamba fedha ile nisiiache kwani hata kama ningeiacha angeokota mwingine. Hivyo mimi sikuiba fedha yenu – niliokota.” Mako akanyamza, Chata akafoka,
“We mpumbavu, endeleaaaah…”
“Nilichukua fuko lile la fedha, nikakimbia nalo mkukumkuku mpaka pori la Sushi. Kukiwa hakuna mtu aliyeniona, nilichimba na kuzifukia fedha zile mahali salama ila naomba usiniulize jembe nilitoa wapi.” Mako alimaliza kisha akatega sikio kusikia wanasemaje.
“Vijana.” Aliita Chata, walipoitika akaendelea, “Andaeni gari zuri, twende tukachukue fedha pori la Sushi harakaaah.

SURA YA TANO

Basi dogo jeusi lilikimbia kwa mwendo wa wastani, ndani ya basi hilo kulikuwa na wanaume kumi, wawili kati yao, walikuwa Mako na Chata. Mako pekee ndiye hakuwa na silaha yoyote, waliosalia walibeba mseto wa silaha, Chata alikamata bastola kubwa, wengine walibeba SMG na AK47!

Dereva alikunja kona kadhaa, kisha akaikamata njia ya vumbi ambayo moja kwa moja ilielekea pori la Sushi. Ukimya ulitawala Mako akaamua kuuvunja.

“Chata… umekuwa jambazi kwa muda mrefu sasa na unayo mali nyingi, kwa nini usiniachie hii milioni mia moja ili nikukumbuke.”

Chata hakujibu, Chinda akainyanyua SMG na kumpiga kwa kitako katikati ya kichwa, Mako akainama, akayasikiliza maumivu kwa majonzi.

Gari sasa lilifika pori la Sushi, Mako aliyejua wapi alipoficha fedha, akawaomba washuke ili wapate kutembea kwa mguu katika njia ambayo gari lisingeweza kupita. Wote wakashuka, Mako akatangulizwa mbele, nyuma akamulikwa kwa mitutu ya bunduki.

Mako akaongoza njia akitembea mwendo wa taratibu, nyuma akifuatiwa na Chinda, Chinda akifuatiwa na Chata, Chata akifuatiwa na wahuni wengine.

Wakati wakiendelea kutembea, mara ghafla akatokea sungura mmoja ambaye alifukuzwa na fisi, macho yote yakageukia lilipo tukio hilo, Mako akatumia nafasi, haraka akakimbia kwa mwendo wa kupindapinda.

Majambazi walipogeuza macho yao, wakamuona Mako akiwakimbia, wote kwa pamoja wakafungua usalama wa bunduki zao, kisha wakakoki kuweka risasi kwenye chemba, haraka vitako vya silaha vikagusa mabega huku wakianza kumkimbiza kijana aliyeanza kuwapotea.

Risasi zilifyatuliwa kwa fujo, lakini zote hazikumpata Mako. Majambazi yakahamaki, mtuhumiwa akapotea katika nyasi za pori lile, wakaamua wasimame wasiojua wampate wapi.
“Kila mtu atembee peke yake kumtafuta huyu panya… tusirundikane sehemu moja, haya sambaa.” Aliamrisha Chata, kisha kila mtu akashika njia yake.

Chinda alielekea kulia akiwa ameikamata vyema bunduki aina ya SMG ambayo tumbo lake lilishiba risasi 30. Akatembea taratibu akimtafuta adui, sasa alipita pembeni ya nyasi ndefu kiasi, kabla hajaendelea na safari yake, akapigwa ngumi nzito ya shingo. Mawasiliano baina ya kichwa na kiwiliwili yakakatika palepale, ikawa tiketi muhimu sana iliyompeleka kuzimu maramoja!
Mako aliyekwisha badilika akiwa hana masihara hata punje, akaikamata ile bunduki kisha akapanda nayo juu ya mti mrefu. Akiwa juu ya mti ule, aliweza kuwaona wabaya wake nane wakiwa wamesambaa, kila mmoja yuko peke yake akizungukazunguka.

Mako hakuchelewa, akalifumba jicho lake moja, akaweka shabaha kisha akaminya ‘triger’ risasi ikatoka na kuua jambazi mmoja kisha akasema kwa sauti “Wamebaki saba.” Akaendelea kuwatungua wahalifu wale mpaka aliposikika akisema,
“Kabaki mmoja!”

Kwa uwezo wa shabaha mithili ya mdunguaji aliokuwa nao Mako, aliweza kuwadondosha maadui wote isipokuwa mtu mmoja tu – Chata. Hakutaka kumwangamiza akiwa juu ya mti, akaamua kushuka.

Mako alitambaa kama nyoka kuelekea alipokuwa Chata. Chata alikwishaanza kuhisi hatari mara baada ya kusikia milio kadhaa ya risasi.

“Weka bastola yako chini, umezidiwa ujanja!” Sauti kali iliamuru.

“Nani kanizidi ujanja?” Chata aliuliza kwa sauti kali, lakini ya kuigiza.

“Mako kakuzidi ujanja, kwanza kaokota milioni mia moja unazodai zako na sasa anataka kukushikisha adabu… weka silaha chini, shwaini.”

Chata akaitupa chini bastola kisha akageuka na kutazamana uso kwa uso na Mako, ambaye ameikamata vyema SMG, akamsogelea Chata kwa kasi ya ajabu, Chata akarusha teke kali ambalo lilifanya bunduki ya Mako idondoke mbali. Sasa wote wakabaki hawana silaha.

Chata akaamsha teke jingine likazipiga mbavu za Mako, akaongeza jingine, Mako akaliona akakwepa. Chata hakuchoka, akarusha ngumi, ikakipiga kichwa cha Mako, akarusha nyingine, Mako akakwepa.

Hapo sasa Mako akauona ugumu uliokuwa mbele yake, kupambana na Chata ilihitaji ujuzi. Mako akaanza mbwembwe na visa, kwanza akakichezesha kichwa chake ili kisipigwe tena, akamtisha Chata, Chata akashtuka, Mako
akarusha teke zito, likampata Chata katikati ya tumbo na kifua. Hakutulia akarusha tikitaka, ikakifunua kichwa cha Chata, Chata akadondoka chini kishaMakoakapaa juu akiwa amelikunja goti lake, alipotua, akatua katikati ya shingo ya Chata. Chata, jambazi lililokubuhu akalala ‘unono’ milele.
Mako kwa ukakamavu akainuka na kuupekua mwili wa Chata, akatoa simu ya jamaa huyu kisha akaingiza namba +91… akapiga, haukupita muda, simu ikapokelewa.
“Nani?... Hallo!” Sauti ya kike iliuliza
“Mako hapa naongea…”
“Oooh! Nambie mume wangu, uko salama?”
“Niko salama, vipi hali ya mwanangu, anaendeleaje?”
“Aaah! Matibabu yameshafanyika na anaendelea vizuri, siku yoyote tunaweza kuruhusiwa kurudi… mmh! … huyu hapa ongea naye.”

“Shikamo baba.” Alisalimia Nkenye.

“Marahabaah!” Alijibu Mako kisha akakata simu, hakutaka kuongea mambo mengi kwa wakati ule. Akaitupa chini simu ya Chata huku akitembea mbele kwa furaha.

TAHARUKI imemwisha!

TAMATI

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024