SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya nne)
Tukiwa njiani kuelekea
katika mji wa jitu hili, nilijitahidi kuuliza maswali.
“unaonekana
u mtu mwema kwangu lakini watu wa jamii yako hawatanidhuru?”
“hakuna
awezaye kukugusa!”
“kwa
nini?”
“mimi
ni mwana wa mfalme.”
Nilifurahishwa na jibu hili na lilinipatia furaha, wakati
tunaendelea kutembea tuliufikia mji na niliona nyumba zilizojengwa na watu hawa
wa chuma. Nyumba zao zilijengwa kwa vioo vigumu na zilifanana sana hata haikuwa
rahisi kubaini wapi aliishi tajiri na wapi aliishi maskini.
Wakati tukiendelea kutembea majitu mengi yaliendelea
kunikodolea macho na kunishangaa sana, lakini hawakuthubutu kunigusa nilikuwa
na mwana mfalme.
Punde tulifika katika jumba kubwa, jumba lilikuwa
tofauti na nyumba nyingine, jumba hili lilijengwa kwa dhahabu pekee. Hapo hapo
nikagundua nilikuwa ndani ya nyumba ya kifalme. Mwenyeji wangu aliiweka
Mapandagila 214 katika uwanja wa jumba lile.
Tuliingia ndani, mbele kidogo nikamuona mfalme, mfalme
akacheka kisha akasema,
“Chokusi,
leo umeleta kiumbe dhaifu kutoka sayari ya Dunia!!”
Hapo nikagundua kuwa mwana mfalme aliitwa Chokusi,
nilipomtazama usoni alicheka, kisha akanambia nisiogope hakuna baya
litakalonipata.
“Kiumbe
toka Duniani jitambulishe.” Mfalme alitamka.
“Naitwa
Nkenye, nipo katika safari ya kuusaka mwezi ulioibwa na kijitu toka Vumu.”
Nilijibu.
Mfalme alicheka kisha akaniambia,
“Wanadamu
ni viumbe wa ajabu sana, mtoto mdogo kama wewe kupewa kazi ya kuutafuta mwezi
ni unyanyasaji.”
Sikutaka kumjibu mfalme, kuna mambo ambayo
hakuyafahamu, nilikaa kimya.
Tulizungumza mengi na mfalme na alidai ya kuwa wao
wanajua uwepo wa wanadamu waliotengenezwa kwa nyama lakini sisi hatujui uwepo
wao watu wa chuma. Kikubwa zaidi mfalme aliahidi kunisaidia kufika katika
sayari ya Vumu.
Mwana mfalme alinichukua na kunipeleka uwanjani,
wakati tunaelekea huko niligundua kuwa viumbe hai vyote katika sayari hii
viliumbwa kwa chuma. Nilistaajabu nilipokutana na mbwa wa chuma, akataka
kunirukia, rafiki yangu Chokusi akamkata kofi zito, mbwa akafyata mkia na
kukimbia.
Niligundua kuwa kumbe mwanamfalme pamoja na urefu wake
wa futi sita na nguvu alizokuwa nazo, alikuwa
na umri sawa na wangu, yaani miaka tisa!
Itaendelea jumapili.