SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya sita)



Looh kabla hata sijamaliza kusema, wali na nyama ya kuku ulikuwa mezani. Nilikula haraka haraka huku watu wote wakinishangaa, sikuwajali, kwa njaa niliyokuwa nayo, nilistahili kula hivyo.

Wakati nikiendelea kula, kuna jambo lilinishangaza, binti waziri alikuwa akiteta jambo na mfalme, huku wakinitazama sana. Nilipotazama pembeni sikumuona rafiki yangu Chokusi. Nikahisi hatari kubwa ilikuwa ikininyemelea.

Niliendelea kula nikiwa na mashaka, mpaka chakula chote nikakimaliza. Mfalme akanitaka nikalale, pia akanieleza ya kwamba kesho alikuwa na mazungumzo muhimu sana na mimi. Nilikubali kisha nikajikokota katika chumba kilichokuwa jirani, humo nilimkuta mwana mfalme Chokusi amekwisha lala. Nikaungana naye.

Asubuhi niliamshwa na Chokusi, akaniomba tukacheze mpira wakati tukisubiri chai. Hapo nikagundua ya kwamba nchi hii watu wake hawapigi mswaki.

“Aaah, mfalme alisema anataka kuzungumza nami, hivyo nisindikize kwanza nikamuone.” Nilimjibu Chokusi, haraka akanisindikiza mpaka alipokaa mfalme.

Tulifika na kumkuta mfalme akiwa amevalia mavazi meupe, pembeni yake alikaa binti waziri, shingoni akiwa kauning’iniza upembe wa shaba! Mtu wa tatu alikuwa yule mzee wa jana aliyetoa habari za binti waziri.

Niliruhusiwa kukaa katika kiti kimojawapo, Chokusi akaambiwa apishe, naye akatii kwa adabu. Nikiwa nimekaa mfalme akaanza kuzungumza nami.

“Mwanadamu sisi ni viumbe wema kwako, tumekusaidia nawe sasa ni zamu yako kutusaidia. Kuna hazina ya vitabu muhimu sana vya mafanikio vilifichwa nchi ya mbali, sehemu palipo vitabu hivi kuna sumaku kali ambayo ndiyo sumu kwetu, viumbe wa chuma hunaswa na sumaku na huo huwa mwisho wetu. Lakini wewe mwanadamu wa nyama, sumaku haina madhara kwako… tafadhali tunaomba utusaidie kuvipata vitabu hivyo!”
Nilijua ni kazi rahisi tu, nikamjibu mfalme kuwa nilikuwa tayari kwenda hata asubuhi ile. Mfalme akanijibu,

“Asante sana… lakini nilisema vitabu hivi vilifichwa mbali sana, kufika huko sio safari ya siku moja, ni safari ya miaka tisa kwenda, kwa hivyo itakuchukua miaka kumi na nane kwenda na kurudi!”

Taarifa hiyo ilinishtua sana, nikajikaza na kumweleza mfalme,

“Haiwezekani… ndugu zangu hawawezi kuishi miaka kumi na nane bila mwezi… ni lazima nikautafute mwezi wetu na kuurejesha nyumbani mapema iwezekanavyo.”
Mzee aliyekuwa pembeni akafoka,

            “Akisemacho mfalme ni amri, huna haki ya kupinga… utake utakwenda usitake utakwenda.”


Baada ya mzee kutoa maneno makali, mfalme alinyanyuka kisha bila kutegemea nilikamatwa na askari sita, wakanipeleka mpaka katika chumba kimoja kidogo kilichokuwa na giza kali wakaniacha humo, nikiwa sina lolote la kufanya.

itaendelea jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1