Uhakiki wa Diwani ya Chungu Tamu
MWANDISHI; THEOBALD MVUNGI
MCHAPISHAJI; TPH
MHAKIKI; DAUD MAKOBA
Chungu tamu ni diwani ambayo inajaribu kupinga dhuluma
kwa nguvu zote na kutetea haki za wanyonge. Maudhui yanayoibuliwa yana uhalisia
wa moja kwa moja na nchi za kiafrika hususani Tanzania.
Maudhui
Dhamira
1. Ulanguzi na biashara za magendo
Mwandishi anajadili jinsi ambavyo ulanguzi unachochea
dhiki katika jamii. Ulanguzi husababisha bidhaa zikapanda bei na maisha kuwa
magumu. Katika shairi la Chanzo ni wenye
kauli mshairi anasema,
“mianzo tukiijua, mipango tajipangia,
Kamwe pasiwe na njia, ulanguzi kujirudia,
Iwe tu twahadithia, mithili historia.”
2. Viongozi wazembe
Hawa ni viongozi ambao husimama katika mikutano na
kuwahimiza watu wafanye kazi huku wao wakiendekeza uzembe kwa kulala ofisini na
kukesha katika majumba ya starehe. Mshairi anawataka viongozi hawa waongoze kwa
mfano. Katika shairi la Wimbo wake
hotubani, mshairi anasema,
“cheo kiko mkononi, agizo li mdomoni,
Kila siku yu pombeni, mchana kutwa ndotoni
Wimbo wake hotubani, raia kazi fanyeni.”
3. Suala la demokrasia
Mshairi anajadili demokrasia ya nchi za kiafrika,
anaonesha jinsi ambavyo viongozi wa nchi hizi hawako tayari kuachia madaraka. Watawala
hawa wanataka kutawala milele. Migogoro hii ya kukosekana kwa demokrasia ndio
inasababisha kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukosekana kwa amani.
Katika shairi la Kademokrasi katoweka
mshairi anasema,
“Barani mabavu yatumika,
Dikteta asijeanguka,
Na majungu pia ayapika,
Udikteta pasi shufaka,
Nasimulia ya Afrika.”
4. Matabaka
Katika shairi la kitaswira la Chatu na kuku, mwandishi anaonesha matabaka mawili, tabaka la
wanaonyonywa (kuku) na tabaka la wanyonyaji (chatu). Shairi hili linalenga
kuamsha hisia za wanyonyaji ili kujikwamua toka mikono ya mnyonyaji.
mwandishi amewatumia chatu na kuku kwamba awali
wamekuwa wakiishi pamoja lakini mwishowe chatu akaishia kuwala vifaranga wa
kuku. Hivyo katika hali ya kawaida chatu na kuku hawawezi kuishi pamoja tangu
mwanzo wa dunia, hivyo mwandishi ametumia hivyo lengo kufikisha ujumbe kwa
jamii husika kwani ndiyo inayoteseka pale matabaka yanavyozidi kuibuka siku
hadi siku.
“Babu hakujali swali langu,
Akaendelea kunipasha habari,
Piku alimezwa huku analia,
Dua akawaombea chatu wote,
Mabaya yawafike,
Wapi kuku akamezeka,
Paku akafungwa,
Pangoni akafikishwa.”
5. Uzalendo
Shairi
la Daktari askari linaonesha jinsi
ambavyo Adam alivyomzalendo kwa kuamua kuipigania nchi yake ya Tanzania katika
vita vya Kagera. Shairi hili ni chachu kwa vijana wote kuamsha morari wa
uzalendo na kuipenda nchi yao, kwani kwa kiasi fulani uzalendo umepungua sana
katika jamii.
“Basi sikiliza ..... Paukwa . . !,
Vita vikaja,
Damu zikavuja,
Watu wakatoweka,
Maiti zikanuka,
Mali zikatimka,
Raha ikaaga,
Vijiji vikawa mbuga,
Pema pakawa alama ya uovu,
Mabomu
yaliacha makovu”
6. Mmomonyoko wa maadili
Shairi
la Fikra za waungwana linamjadili mwanamke aliyepoteza maadili yake ya asili
hata akathubutu kuomba aolewe na wanaume wawili! Suala la mwanamke kuolewa na
wanaume wawili ni kinyume na maadili ya Mtanzania. Mshairi anasema,
“Mume wangu nakupenda, Joseph amenikuna,
Nimekula naye tunda, ninampenda sana,
Na usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Joseph.
7. Mapenzi
Mwandishi
anajadili dhana ya mapenzi katika shairi la Manzese
mpaka Ostabei. Mashaka anampenda msichana wa Ostabei Dora, lakini wazazi
wake Dora, wanakataa binti yao kuolewa na kijana masikini wa Manzese. Mvutano
mkubwa unatokea lakini Dola analazimisha kwa hali na mali lazima awe na
Mashaka. Hatimaye wazazi wanakubali na ndoa inafungwa.
Mwandishi
anajaribu kuonesha kuwa suala la mapenzi halina ubaguzi bali ni watu kuridhiana
na kupendana wa dhati peke.
“Hadithi
njoo, uende Manzese,
Upite Kariakoo,
Mwisho wako Ostabei,
Mjini Bandarisalama,
Wengine wameliita Jiji…”
Ujumbe
1. Mapenzi hayachagui chochote ilimradi watu wapendane na kuridhiana.
Ujumbe
huu unapatikana katika shairi la Manzese
mpaka Ostabei.
2. Taifa lipige vita na kuwakomesha mara moja viongozi wazembe.Ujumbe huu umejadiliwa katika shairi la Wimbo wake hotubani.
3. Demokrasia ni suala lisilokwepeka kwa maendeleo ya jamii yoyote ileKama ilivyojadiliwa katika shairi la Kademokrasi katoweka.
4. Nchi itajengwa na wananchi wenyewe hivyo ni vyema kutengeneza mazingira ya kupata vijana wazalendo walio tayari kulipigania taifa lao.
Kama ilivyojadiliwa katika shairi la Daktari askari.
Migogoro
-
Migogoro ya kisiasa
Viongozi
wanang’ang’ania madaraka, wanadhulumu mali ya umma na kunyanyasa watu
wanaojaribu kuwapinga. Mgogoro huu unadhihirishwa katika shairi la Kademokrasi katoweka.
-
Migogoro ya kiuchumi
Katika
jamii yanaonekana matabaka mawili kinzani, tabaka la wenye nacho na wasionacho.
Wenye nacho wanawanyonya na kuwanyanyasa wasionacho na kusababisha mgogoro
ambao suluhisho lake si rahisi kupatikana, kama inavyooneshwa katika shairi la Chatu na kuku.
-
Migogoro ya kiutamaduni
Mwanamke
anaonekana akipingana na utamaduni wake kwa kudai naye aolewe na wanaume wawili
kama jinsi ambavyo mwanaume ana uhuru wa kuwa na wanawake wawili na kuendelea.
Mgogoro huu umejitokeza katika shairi la Fikra
za waungwana.
Msimamo
Mwandishi
anamsimamo wa kimapinduzi kwani ametoa suluhisho la kupambana pamoja ili
kuyaondoa matatizo mbalimbali yanayozikumba nchi za kiafrika. Mwandishi
anashauri kurejeshwa kwa demokrasia ili serikali ziwe mali ya ‘umma’ na si mali
ya wachache wenye tamaa.
Falsafa
Mwandishi
anaamini katika usawa kwa watu wote ili kuleta maendeleo. Mwandishi
hafurahishwi hata kidogo na kustawi kwa matabaka ambayo yamepelekea kuwagawa
maskini na matajiri.
Fani
Muundo
Msanii ametumia
muundo changamano. Hata hivyo mashairi mengi yametumia muundo wa tarbia, mfano katika shairi la Fikra za waungwana pamoja na
sabilia, mfano katika shairi la Daktari
askari.
Mtindo
Mshairi ametumia
mitindo yote miwili, yaani wa kimapokeo na wa kisasa.
Matumizi ya lugha
TAMATHALI ZA
SEMI
-
Tashibiha
Mweusi
kama kiatu cha jeshi (Manzese mpaka
ostabei)
-
Tashihisi
Katika
ile baridi kali, mabomu ya mikono yakatubusu miguuni (Daktari askari)
-
Sitiari
Ushairi
ni sukari tamu (Chungu tamu)
-
Tafsida
Nimekula
naye tunda (Fikra za waungwana)
PICHA NA TASWIRA
Chatu –
inawakilisha wanyonyaji
Kuku –
wanyonywaji
Ngulu –
vijiji/jamii iliyosahaulika katika kupatiwa maendeleo
MISEMO NAHAU NA
METHALI
-
Lakini haikutiwa chumvi mitaani
-
Kuvaa masulupwete
-
Umoja ni nguvu
-
Sasa mwaleta shari
Kufaulu kwa mwandishi
Amejadili kwa
kina matatizo mengi yanayozipata jamii za kiafrika, pia amejaribu kutoa
masuluhisho ya matatizo hayo.
Vilevile amefaulu
kutumia mitindo yote miwili, kimapokeo na kisasa.
Kutofaulu kwa mwandishi
Baadhi ya
mashairi yametumia lugha ngumu ambayo inamfanya kila mhakiki alifasiri shairi
kwa mtazamo wake.
TAMATI