Uhakiki wa Diwani ya Fungate ya Uhuru
JINA LA KITABU; FUNGATE YA UHURU
MWANDISHI; MOHAMED SEIF KHATIBU
MCHAPISHAJI; DUP
MWAKA; 1988
MHAKIKI; Daud Makoba
UTANGULIZI
Fungate ya uhuru ni diwani inayozungumza bila kificho
matatizo yote yanayozipata nchi zinazoendelea. Mwandishi kwa namna fulani
anaona kuwa uongozi ndio tatizo la kwanza linalosababisha maafa haya. Mwandishi
anawachora viongozi wa Afrika wakiwa katika ‘fungate’ wakisherekea matunda ya
uhuru bila kukumbuka sasa ni wakati wa kuachana na sherehe hizo na
kuwaunganisha watu kuijenga nchi yao.
Maudhui
Dhamira
1. Ukombozi wa kisiasa
Tatizo kubwa linalojadiliwa na mshairi ni anasa
zinazoendekezwa na watawala. Watawala hawawajibiki badala yake wanaponda
starehe na kusababisha uchumi uzorote. Katika shairi la ‘Fungate ya uhuru’ mshairi anasema,
"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Namajumba mazuri, wamekwishajijengea.Watembea kawa magari, hivi zimewazowea." Uk.1
Paa, ni mnyama porini,ni mwenye nyingi papara.
Paa,ni kuteka mekoni, moto uwake imara.
Paa, ni toa magambani, samaki atiye sura.
Paa, pia la nyumba, kmakuti au karara.”
Na kazi ikatayarishwa,
Ili uchafu kuondoshwa.”
2. Kuuheshimu na kuutunza utamaduni wa kiafrika
Katika utamaduni mshairi analizungumzia suala la lugha ya
Kiswahili, anawaasa wanajamii waiheshimu na kuitunza ligha hii kwani ni
kitambulisho cha utamaduni wetu. Katika shairi la Dafina mshairi anaonesha jinsi ambavyo lugha ya Kiswahili
inajitosheleza na utamu ilionao hasa katika mchezo wa maneno,
“Paa,
ni kuruka angani, kama ndege na tiara.
3. Usaliti
Mshairi amefanikiwa kujadili kwa kina usaliti unaofanywa na
viongozi, anatoa ahadi ya kuwahukumu viongozi wasaliti, pia anauasa umma
usicheke na viongozi hawa kwani ndio chanzo cha umasikini na matatizo yote
katika jamii. Katika shairi la Nikizipata
bunduki, mshairi anasema,
"Nikizipata shembea,
Takamata
viongozi, wasaliti wa nchini,
Niwachinje
kama mbuzi miiko wasoamini…"
4. Wizi
Mshairi anatoa kauli kali kuwa wizi upo kila sehemu, hata katika
nyumba za ibada! Anaionesha jamii ikiwa imeoza, isiyo na uaminifu hata kidogo,
katika jamii hii kila mtu anaiba! Ajabu ni kwamba hata vyombo vya usalama
vilivyoaminiwa kukabiliana na wezi navyo vinakengeuka na kupita katika mkondo
huu. Katika shairi la Wizi mshairi
anasema,
“Walinzi hawapo? La hasha!
polisi hulinda
wezi,
majeshi
huhalalisha wezi,
na dini zawabariki
wezi”
5. Unyonyaji
Mshairi anadadavua bila kuogopa namna ambavyo mataifa
yaliyoendelea yanavyolinyonya bara la
Afrika. Rasilimali zote huibiwa na mataifa haya na kuyafanya yatajirike huku
nchi za kiafrika zikididi kudidimia katika lindi la ufukara. Mshairi katika
shairi la Afrika anasema
Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika,
Ni kwa mingi miaka,
Nasi
tukafukarika.
6. Mapenzi
Mshairi anamsimanga mwanamke ambaye alimpenda hapo awali
kabla hajabadilika na kuamua kumwacha. Mshairi anaonesha jinsi ambavyo
mahusiano ya wawili hubadilika pale ambapo mmoja huamua kuvunja kiapo. Katika
shairi la U wapi uzuri wako? Mshairi anatoa yote ya moyoni mwake jinsi ambavyo
aliachwa na mwanamke aliyempenda. Hata hivyo mwanamke huyo alikokwenda hakukuwa
mahala sahihi kwani alipoteza sifa zake zote za mwanzo.
Bao la mkahawani , kila mtu akalia…
Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokea…
Pia mashairi mengine yanayozungumzia mapenzi ni kama, Nchi yangu, Wewe peke yako, Nia yangu
sigeuzi, na Kuntu sauti ya kiza.
Ujumbe
1. Ili nchi ipate maendeleo lazima iwe na viongozi
wachapakazi na waaminifu.
Kama inavyothibitishwa katika shairi la ‘Fungate ya uhuru’. Mwandishi anaonesha
jinsi ambavyo viongozi wazembe na wavivu wanavyolikosesha maendeleo taifa.
2. Lugha ya kiswahili ni kitambulisho cha taifa letu hivyo
ni lazima tuitunze na kuithamini wakati wote.
Ujumbe huu unapatikana katika shairi la Dafina.
3.
Wizi ni chanzo cha umasikini na matatizo
yasiyokwisha
Mshairi
anaonesha jinsi ambavyo jamii inakaliwa na watu wanaoendekeza vitendo vya wizi
bila kufanya kazi. Katika jamii hii, mshairi anasema kila mtu anaiba hata
askari wenye jukumu la kulinda watu na mali zao nao wanajihusisha na vitendo
vya wizi! Ujumbe huu unapatikana katika shairi la Wizi.
4.
Mataifa yaliyoendelea yanazinyonya nchi
za kiafrika na kuzifanya ziwe na uchumi duni.
Ujumbe
huu unajitokeza katika shairi la Afrika.
Migogoro
1. Migogoro
ya kisiasa
Kuna
uhusiano mbaya baina ya serikali na watu wake. Raia wanaonekana kuchoka hata
wanahidi kuwaangamiza viongozi wao kama ilivyojadiliwa katika shairi la Nikizipata bunduki.
2. Migogoro
ya kiuchumi
Shairi
la Fungate ya uhuru, linaonesha kwa
kina mgogoro huu. Hii inathibitishwa kwa uwepo wa matabaka kati ya wenye nacho
na wasio nacho. Wasionacho wanaishi maisha duni na manung’uniko makuu, huku
wenye nacho wakiendelea kula fungate. Katika shairi la Nikizipata bunduki masikini wanaahidi kupambana na matajiri ili nao
waipate keki ya taifa.
Msimamo
Mshairi
anamsimamo wa kimapinduzi kwani anashauri kuwa matatizo yote yaliyopo katika
jamii kama rushwa, wizi, umasikini na mengine mengi suluhisho lake ni wananchi
kuwaondoa viongozi wazembe na wala rushwa na kuweka viongozi imara ambao
wataisimamia serikali katika kujiletea
maendeleo.
Falsafa
Mwandishi
Mohamed Seif Khatibu, falsafa yake anaamini katika ujamaa, anaona kuwa itikadi
ya ujamaa ndiyo inayofaa kufuatwa na nchi za kiafrika ili kuleta usawa, haki na
maendeleo ya watu wake, anaamini kuwa ujamaa unaweza kuondoa unyonyaji,
matabaka na mambo yanayofanana na hayo katika jamii.
Fani
Muundo
Katika
utanzu wa ushairi, muundo tunaangalia idadi ya mistari katika beti, kama
mwandishi katika diwani yake atatumia mistari miwili katika kila ubeti, basi
tutasema kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathnia, na kama atatumia mistari
mitatu kwa kila ubeti, tutaseama kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathilitha,
na mistari mine ni muundo wa tarbia na mistari mitano na kuendelea utakuwa
muundo wa takhmisa.
Kwa
upande wake, mshairi Mohamed Seif Khatibu katika diwani hii, ametumia muundo
changamano kwani mashairi tunayoyaona katika diwani hii ametumia miundo zaidi
ya mmoja.
-
Muundo wa Tathnia umeonekana katika
shairi la Mjamzito.
“Mjamzito, Amelazwa
"thieta"
Lazima kupasuliwa.”
-
Muundo wa Tathlitha umeonekana katika
shairi la Waja wa mungu
“Dunia, vyakula
hawavioni, mafakiri,
Lakini, vyakula kwao
pomoni, mabepari,
Abadani, hawa si waja
wa Mungu!”
-
Muundo wa Tarbia umeonekana katika
shairi la Afrika.
"Bara la Amerika, Na Ulaya
kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi
miaka,
Nasi tukafukarika."
-
Muundo wa Takhmisa umeonekana katika
shairi la Unganeni.
“Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo
Marefu,
Ushindi ni wetu.”
Mtindo
Mwandishi
amatumia mtindo changamano yaani amechanganya mitindo yote ya aina mbili, yaani
mtindo wa kimapokeo na mtindo wa kisasa.
Mashairi ya
kimapokeo ni kama vile, "Mcheza Hawi
Kiwete" [uk. 37-38], na "Ua
Si Ruwaza Njema" [uk. 47-48].
Matumizi ya Lugha
i.
Tamathali za semi
-
Tashibiha
Nabaki
kugunaguna, kama nyani
kwenye nyika
katika shairi la "Ningekuwa na Sauti"
[uk.10-11]
-
Sitiari
Bao
la mkahawani , kila mtu akalia, katika shairi la U wapi uzuri wako.
-
Takriri
Mbinu
hii inajitokeza katika shairi la "Dafina"
uk. 8-9 ambapo tunaona mwanzoni mwa kila mstari katika ubeti kuna maneno
yanarudiwa rudiwa.
-
Tafsida
Hawezi
kujifungua badala ya kutumia neno hawezi kuzaa ambalo ni neno kali sana, katika
shairi la "Mjamzito" uk. 7
ii.
Lugha ya picha/taswira
Lugha ya picha iliyotumika ni pamoja na
kunguru katika shairi la "Kunguru"
[uk. 26-27], tunaposoma shairi hili tunapata picha kuwa, kunguru ni sawa na
viongozi ambao tuliwachagua kuondoa matatizo katika jamii kinyume chake wao ndo
wakazidi kuleta matatizo badala ya kuyaondoa kama walivyofanya kunguru weusi
waliopandikizwa kuondoa uchafu badala yake wao ndo wamekuwa wakileta na kujaza
uchafu na kuwa kero kwa jamii, mfano katika shairi hilo mwandishi anasema,
“Kunguru
walisafilishwa,
Nchini wakahaulishwa,
Pia katika mshairi la Fungate ya uhuru mwandishi ametumia
lugha ya picha kuwaelezea viongozi ambao hawafanyi kazi, wao bado wapo Fungate
wanaponda raha.
Fungate ni kipindi
ambacho bwana na bibi Harusi hutafuta sehemu ya kujistarehesha na kupumzika,
kabla ya kuyaanza majukumu ya ndoa. Fungate hutarajiwa kufanyka kwa muda mfupi
tu na kisha baada ya hapo shughuli nyingine huweza kuendelea. Maharusi wanapoendelea
kubaki fungate kwa muda mrefu huacha mishangao na kwa vyovyote kazi zao
hazitaendelea, isipokuwa watawaumiza wale waliowachangia ili waende fungate.
Mshairi anaeleza kuwa, Viongozi wetu
toka uhuru mpaka leo bado wanasherehekea matunda ya uhuru wakiwa wamesahau
majukumu yao.
Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
Kufaulu
Kwa kiasi kikubwa
mwandishi amefaulu katika vipengele vyote vya fani na maudhui, kwa mfano,
kimaudhui, amefanikiwa kuonesha matatizo mbalimbali yanaikabili jamii yake na
kuipa njia jamii yake namna inavyoweza kuondokana na matatizo hayo. [rejea
dhamira mbalimbali]
Kifani amefanikiwa,
ametumia muundo changamani jambo ambalo linaweza kumsaidia msomaji wa kazi yake
kujifunza namna ya kuandika mashairi yenye miundo tofauti tofauti, pia ametumia
mtindo changamani yaani hakufungamana katika mtindo mmoja tu, ametumia mitindo
yote, yaani mashairi ya kimapokeo na kisasa ambayo nayo huweza kumfanya msomaji
wake, kuweza kujifunza namna ya kuandika na kutunga mashairi kwa mitindo yote
hiyo.
Kutofaulu
Kama ilivyo kawaida
huwa hakuna kazi isiyo na mapungufu, hivyo hivyo katika diwani hii kuna
mapungufu mbalimbali yanajitokeza ingawa si kwa kiwango kikubwa sana, kwa
mfano, baadhi ya njia ambazo mwandishi anazitoa jamii kuzitumia ili kuondokana
na matatizo zinaweza kuhamasisha jamii kujichukulia sheria mikononi wakati vipo
vyombo vya kisheria vinavyopaswa kufanya hivyo, mfano rejea shairi la, "Ningekuwa na Sauti" uk. 10-11, na
shairi la "Nikipata Bunduki"
uk. 11.