Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu
TAMTHILIYA; KILIO CHETU
MWANDISHI; MEDICAL AID FOUNDATION
MCHAPISHAJI; TANZANIA PUBLISHING HOUSE
MWAKA; 1995
JINA LA MHAKIKI; Mwalimu Daud Makoba
Kilio chetu ni tamthiliya inayovunja ukimya uliotawala
miongoni mwa jamii katika kutatua matatizo makubwa ambayo chimbuko lake ni
mahusiano ya kijinsia.
Katika tamthiliya hii vijana wanatoa sauti ya jitimai
iliyojaa sononeko na shutuma dhidi ya wazazi, walezi na viongozi ambao
wanafumbia macho suala hili nyeti. Ndiyo maana tamthiliya hii inasisitiza sana
haja ya kuwapa vijana elimu juu ya mahusiano ya kijinsia badala ya hofu na
vitisho ambavyo vimedhihirika kupitia hali halisi ya kuwa vimeshindwa.
FANI
MUUNDO
Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Inaanza kwa
kutuonesha wazazi wakibishana juu ya kutoa elimu ya jinsia na mahusiano. Mwisho
Joti mtoto ambaye hakupatiwa elimu hiyo anampa mimba mtoto mwenzake Suzi.
Baadae Joti anakufa kwa UKIMWI.
Pia tamthiliya hii imegawanywa katika sehemu sita.
sehemu ya kwanza. Inaonesha jinsi ambavyo gonjwa la
UKIMWI linaiteketeza, jamii wengi wao wakiwa watoto ambao hawakuwa na elimu ya
jinsia na mahusiano.
sehemu ya pili. Wazazi wanabishana juu ya kuwapatia
elimu ya jinsia na mahusiano watoto wao. Mama Suzi anasema jambo hilo liko
kinyume na maadili, lakini Baba Anna yeye anaunga mkono suala hilo.
sehemu ya tatu. Inaeleza kuhusu watoto Joti na Suzi
ambao wamekwisha anza mambo ya ngono. Pia watoto wameathiriwa na utandawazi
kwani wanaangalia video za ngono bila wasiwasi.
Sehemu ya nne. Inazungumzia tabia hatarishi za Joti
kuwa na wasichana wengi. Vilevile Anna kutokana na elimu ya jinsia na mahusiano
aliyonayo, anaendelea kukwepa vishawishi.
Sehemu ya tano. Mtoto Suzi kapata mimba, anabaki njia
panda akiwa hajui afanye nini.
Sehemu ya sita. Hii ni sehemu ya sita. Tunamuona Joti
akifa kwa UKIMWI, na Suzi anabaki akiwa na mimba pamoja na maambukizi ya virusi
vya UKIMWI.
MTINDO
Tamthiliya hii imetumia mtindo wa;
i.
Dayolojia
– majibizano ya wahusika yametawala toka mwanzo mpaka mwisho wa tamthiliya hii.
ii.
Monolojia
– mtindo huu wa masimulizi umetumika japo kwa kiasi kidogo.
iii.
Mtindo
wa masimulizi ya ki ngano - mfano katika ukurasa
wa 1 Mtambaji anasimulia,
“Hapo zamani za kale paliondokea kisiwa
kimoja kikubwa sana. Kisiwa kilikuwa na watu wa kila aina…”
iv.
Matumizi
ya nyimbo – katika ukurasa wa 29,
Anna anaimba wimbo unaokemea wanaume wanaomfuata kumlaghai.
“Anna, Anna, Anna mie niacheni mie x 2
Msichana
mdogo bado ninasoma niacheni mie.”
v.
Matumizi
ya nafsi
Nafsi zote zimetumika lakini nafsi ya
pili imetawala zaidi.
WAHUSIKA
JOTI
-
Mhusika
mkuu
-
Hana
elimu ya jinsia na mahusiano
- Anajiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi na wasichana wengi. Wengine wakiwa wakubwa kuliko
yeye.
-
Mwisho
anakufa kwa UKIMWI
SUZI
-
Mhusika
mkuu
-
Msichana
mdogo anayesoma shule ya msingi
-
Hana
elimu ya jinsia na mahusiano
-
Anajiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi mwenzake Joti, pia anaambukizwa
UKIMWI na kupata mimba.
ANNA
-
Msichana
mwenye elimu ya jinsia na mahusiano
-
Anakataa
vishawishi vya wanaume kwa sababu anajitambua kwa sababu ya kuwa na elimu ya
jinsia
MAMA SUZI
-
Anashikilia
mila na tamaduni za zamani
-
Haungi
mkono kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano, anaamini kufanya hivyo ni
kuwaharibu watoto
MJOMBA
-
Mwanaume
mtu mzima
-
Anaunga
mkono wazazi kuwapatia watoto wao elimu ya jinsia na mahusiano.
Wahusika wengine ni; Baba joti, Mama Joti, Baba Anna, Choggo,
Mwarami, Jumbe, Chausiku, Jirani, na wengineo.
MANDHARI
Mandhari ya mjini yametumiwa na mwandishi. Pia kunayo
mandhari ya;
Nyumbani, kijiweni, barabarani, n.k
MATUMIZI YA LUGHA
Tamathali za semi
i.
Tashibiha.
“Wakapukutika kama majani ya kiangazi.”
Uk 1
ii.
Sitiari.
“We mbwa mweusi.” Uk 10
iii.
Takriri. “vikawazoa, vikawazoa… vikawazoa.” Uk 3
iv.
Tanakali
sauti. “pwi, pwi, pwi,” uk 18
v.
Tafsida.
“Kafa kwa kukanyaga nyaya.” Uk 4
vi.
Mubaalagha.
“mtu si mtu, kizuka si kizuka” uk 4
2. Misemo, nahau na methali
i.
Msemo.
“Wembamba wa reli treni inapita.” Uk 7
ii.
Msemo.
“Kukimbilia suti na nepi hujavaa.” Uk 28
iii.
Methali.
“umeula wa chuya.” Uk 29
iv.
Methali.
“shukrani ya Punda ni mateke” uk 19
v.
Nahau. “nimekuvulia kofia” uk 6
3. Picha na taswira
“Dubwana” –ugonjwa wa UKIMWI;
“Nguru” –aina ya Samaki wabaya–amefananishwa
na mtu mbaya;
“Kinyago”- Suzi.
MAUDHUI
DHAMIRA
Dhamira nyingi zimejadiliwa katika tamthiliya hii, miongoni
mwa dhamira hizo ni;
i. Elimu ya jinsia na mahusiano
Jamii imekumbwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili pamoja na
maradhi hatari yasiyotibika kama UKIMWI. Hivyo wazazi wanapaswa kuwaelimisha
watoto wao juu ya njia sahihi za kujikinga na matatizo haya. Katika tamthiliya
tunaona pande mbili, ule unaoshikilia ukale na upande unaotaka mabadiliko. Baba
Anna, anawaelimisha watoto wake juu ya madhara ya kujihusisha na ngono katika
umri mdogo, Anna anaelewa na anafanikiwa kukwepa vishawishi. Hali ni tofauti
kwa Mama Suzi anaamini kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano ni
kuwaharibu na kuwapoteza. Anaposhauriwa kuwapatia watoto elimu hiyo anafoka,
“Huko
si ndiko kunifundishia wanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono…”
Kutokana na kutokukubali kuwapatia
wanawe elimu hii, Suzi anapewa mimba na kuambukizwa UKIMWI.
ii. Mmomonyoko wa maadili
Maadili hayazingatiwi tena katika jamii. Watoto kwa wakubwa
wote wamepotoka. Tunaona watu wazima wakitembea na watoto wadogo, mfano
Chausiku anamahusiano na mtoto mdogo Joti. Pia watoto wamejiingiza katika
mahusiano ya kimapenzi, Joti anamahusiano na Suzi. Watoto hawahawa wanaangalia
video za ngono bila kuogopa chochote. Katika ukurasa wa 20 Joti anasikika akiwahamasisha wenzake.
“Yaap,
ukimtaka Suzi, chukua. Picha ya ngono, matusi angalia!”
Mmomonyoko huu wa maadili utaondolewa
endapo watoto watapatiwa elimu.
iii. Athari ya sayansi na teknolojia
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta
mabadiliko makubwa katika jamii, mfano katika tamthiliya hii, watoto wanakwenda
kuangalia picha za ngono na kuwafanya waharibikiwe kifikra kwa kutamani kuigiza
kile wanachokiona. Joti, mtoto kinara wa kutazama picha hizo anaambulia UKIMWI
na kufa angali mtoto mdogo.
iv. Nafasi ya mwanamke katika jamii
Nafasi ya mwanamke ni jumla ya mambo yote ayatendayo
mwanamke katika kazi ya fasihi. Mengine huwa mazuri yanayostahili pongezi na
machache huwa mabaya yanayostahili kukemewa kwa nguvu. Katika tamthiliya hii,
mwanamke amechorwa kama;
-
Chombo
cha starehe. Mfano Joti anamtumia Suzi kwa ajili ya kujistarehesha.
-
Asiyependa
mabadiliko. Mama Suzi hataki kutoa elimu ya jinsia kwa wanaye.
-
Asiye
na maadili. Suzi hana maadili, anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi katika
umri mdogo.
-
Mwenye
elimu na asiyedanganyika. Anna ana elimu ya jinsia na mahusiano, wanaume
wanashindwa kumdanganya kwa pesa na maneno matamu.
UJUMBE
i.
Asiyefunzwa
na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Suzi na Joti hawakufunzwa vyema na wazazi wao,
badala yake ulimwengu unawafunza.
ii.
Elimu
ya jinsia na mahusiano itolewe kwa watoto. Elimu hii itawafanya waepuke
vishawishi.
iii.
Sheria
kali zitungwe dhidi ya watu wanaowalaghai watoto. Kuna watu wazima
wanaowaingiza watoto katika vitendo vya kimapenzi kama Chausiku anavyomlaghai
Joti. Sheria kali itungwe na isimamiwe kuwakomesha.
iv.
Wazazi
wote washirikiane katika malezi ya watoto. Baba Anna na Mama Anna
wanashirikiana katika malezi ya watoto wao. Matokeo bora yanaonekana.
MIGOGORO
Migogoro iliyojitokeza ni pamoja na;
Migogoro ya wahusika
i. Mgogoro wa Joti na Suzi
Mgogoro huu unasababishwa na tabia ya joti kuwa na mahusiano
na wasichana wengi. Suluhisho la mgogoro huu ni Joti kumuomba msamaha Suzi.
ii. Mgogoro wa Suzi na Mama yake
Mgogoro huu unasababishwa na mama Suzi kuvikuta vidonge vya
kuzuia mimba katika sketi ya mwanaye. Suluhisho la mgogoro huu ni Mjomba
kumwamuru Suzi aende ndani na mazungumzo kati ya Mjomba, Mama Suzi na majirani
wengine yanaendelea.
iii. Mgogoro kati ya Mjomba na Mama Suzi
Chanzo cha mgogoro huu ni Mjomba kumshauri Mama Suzi ampe elimu
ya jinsia na mahusiano binti yake. Mama Suzi anakataa na kusema kufanya hivyo
ni kuwafundisha watoto umalaya.
iv. Mgogoro kati ya Chausiku na Joti
Chausiku anamlaumu Joti kuwa anamahusiano na wasichana
wengine, anaendelea kulalama kuwa, hata zawadi anazompatia anawapatia wasichana
wengine. Chausiku anamtisha Joti kuwa atamchoma moto yeye na visichana vyake.
KICHEKO!!
Mgogoro wa nafsi
Huu ni mgogoro ambao humpata mhusika peke yake kati yake
yeye na nafsi yake.
-
Suzi
anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapopata mimba na kuambukizwa virusi vya
UKIMWI. Anabaki akilia, lakini hakujilaumu mwenyewe, bali anamlaumu mama yake
kwa kushindwa kumpatia elimu ya jinsia na mahusiano. Katika ukurasa wa 40,
anasema,
“Mimi
na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa tusingetumbu…”
Msimamo
Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Katika tatizo la watoto
wengi kuangamia kwa ugonjwa wa UKIMWI, anashauri elimu ya jinsia na mahusiano
itolewe ili kuleta ukombozi kwa jamii.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa elimu ya jinsia na mahusiano
ikitolewa kwa watoto itawasaidia kupambana na hatari ya kuambukizwa virusi vya
UKIMWI.
KUFAULU NA KUTOKUFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Kufaulu katika fani
-
Mwandishi
ametumia lugha nyepesi inayoeleweka kwa urahisi.
-
Mwandishi
ametumia wahusika ambao wameibeba vizuri dhamira kuu
-
Mwandishi
ametumia muundo rahisi wa moja kwa moja ambao haumchoshi msomaji wal a
kumchanganya.
Kufaulu kwa maudhui
-
Mwandishi
amefaulu kufikisha dhamira katika jamii juu ya umuhimu wa kuwapatia watoto
elimu ya jinsia na mahusiano.
-
Pia
mwandishi ameifungua jamii na kuionya juu ya hatari ya sayansi na teknolojia
endapo itatumiwa vibaya.
KUTOKUFAULU
Kutokufaulu katika fani
-
Mwandishi
ametumia mandhari ya mjini pekee kana kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI
yanawakabili watoto waishio mjini tu.
Kutokufaulu katika maudhui
-
Ugonjwa
wa UKIMWI huwapata watu wote bila kuzingatia umri. Lakini katika tamthiliya
hii, wanaougua ugonjwa huu ni watoto pekee. Kwa kiasi fulani mwandishi
hajafaulu.
Hata hivyo kazi hii ni bora na inastahili pongezi kwa
mafunzo makubwa inayoyatoa katika jamii yetu iliyogubikwa na utandawazi.