RIWAYA| SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya 10)
“Jitambulisheni nyie ni akina nani? Sivyo tunawachoma moto.” Alisema
mmoja wao aliyeonekana kuwa kiongozi.
“Tumekuja kwa amani,”
nilijibu, “sisi ni wanadamu toka sayari ya Dunia, tupelekeni kwa mfalme wenu
tuna mazungumzo.”
“Ha! ha! ha! mmeufuata
mwezi wenu, hampati kitu, na mkileta habari za kudai mwezi mtarudi bila roho
zenu.” Kilijibu kijitu kichafu, nilipokitazama usoni nikagundua ni kilekile
kilichoiba mwezi wetu na kuuweka mfukoni, nilistaajabu umbile dogo la kiumbe
yule liliwezaje kuubeba mwezi tena kwa kuutia mfukoni!
Baada ya mazungumzo walikubali kutupeleka kwa mfalme wao. Walitutaka
twende kwa mwendo pole ili tufike asubuhi maana usiku ule mfalme alilala na
haikupaswa kumsumbua.
Chombo kilitembea taratibu tukiwa tumewekwa katikati ya vile vijitu,
hatukuruhusiwa kuongea wala kukohoa. Kwa muda wote huu, msichana Minza
hakuonesha dalili yoyote ya kuchoka wala hofu.
Wakati kunakucha, sisi tulikuwa tunaingia katika makazi ya mfalme wa Vumu.
Sayari hii ilitawaliwa na mfalme mmoja, na watu wake wote walifanana. Walikuwa
wafupi, wachafu, lakini wanaoweza kupaa.
Tulipofika chombo chetu kilitua, nikashuka na Minza akashuka,
tukapelekwa mpaka ndani, humo tulimkuta mfalme akiwa amekaa katika kiti cha
dhahabu. Mfalme hakufanana na watu wake. Alikuwa mrefu tena asiyeweza kupaa,
msafi na mwenye nywele za sufi tofauti na watu wake ambao wote vichwa vyao
havikuwa na nywele. Mfalme alitukaribisha nasi hatukusita, tulikaa katika viti.
“Habari ya Duniani?”
“Nzuri.” Tulijibu kwa
pamoja.
“Endapo mmekuja kuchukua
mwezi wenu hamtafanikiwa, na endapo mmekuja kutembea karibuni sana.” Mfalme
alizungumza maneno ambayo yalitukatisha tamaa hata kabla hatujapumzika. Kauli
hiyo ilikifanya kifua cha Minza kidunde kama mpira. Nikaamua kuzungumza kwa
busara sana.
“Ni kweli tunautaka
mwezi, lakini hii ni kwa faida yetu sote. Sisi na wewe. Mwezi wa Dunia yetu
ulitengenezwa kwa ajili ya Dunia yetu, kuuweka huku kunaufanya utoe mwanga
hafifu na kikifika kipindi cha kupatwa kwa jua mwezi huu utasababisha majanga
ya asili. Zipo faida mbili za wewe kuturuhusu kuondoka salama na mwezi wetu.”
“Zitaje.” Alijibu mfalme
akiwa na hamu ya kufahamu. Nikamtazama machoni Minza aliyekuwa kimya muda wote
kisha nikaendelea kuzungumza.
“Tunafahamu ya kwamba
nyinyi si viumbe waovu ila mmeiba mwezi wetu kwa sababu mwezi wenu ulizima
ghafla. Hivyo tutauwasha tena mwezi wenu na kuwafundisha namna ya kuutengeneza
pindi uharibikapo.”
Mfalme aliachia tabasamu pana hata nikaweza kuyaona meno yake meupe.
Akatulia kwa muda akitafakari.
Itaendelea Jumapili...