Uhakiki wa Kazi za Fasihi Andishi | Kuuelewa Uhakiki
Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na
kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalumu.
Kwa maana nyingine tunaweza kusema, uhakiki ni uchambuzi wa
kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi kwa lengo la
kufafanua vipengele vya fani na maudhui.
Misingi ya uhakiki
Misingi ya uhakiki hujikita katika fani na maudhui, nazo
fani na maudhui huwa na vipengele vyake ambavyo ndivyo huhakikiwa.
Kuhakiki Fani
Fani ni mbinu anazotumia mwandishi
ili kuwasilisha maudhui.
Vipengele vya fani ni;
i. Mtindo
Mtindo ni mbinu za kipekee zinazotofautisha msanii mmoja na
mwingine. Mambo yaonekanayo katika mtindo ni; matumizi ya monolojia, dayolojia,
barua, nyimbo, nafsi n.k
ii. Muundo
Ni mpangilio wa
visa na matukio katika kazi ya fasihi. Miongoni mwa aina za uwasilishaji wa
visa na matukio ni;
Muundo wa moja kwa moja au msago
Hii ni namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, yaani
kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia.
Muundo wa urejeshi
Huu ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji
anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo.
iii. Wahusika
Wahusika ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi
huwatumia ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Wahusika hugawanywa katika makundi mawili;
Wahusika wakuu
Ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa
kazi ya fasihi.
Wahusika wadogo
Wahusika hawa hujitokeza mara chache na huwa na lengo la
kumsaidia mhusika mkuu kufikisha ujumbe.
Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika
katika makundi yafuatayo:
- Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
- Mhusika
bapa ni
mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano; kama
ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama
ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
iv. Mandhari
Ni sehemu
ambayo matukio ya kazi ya fasihi yanafanyika.
Matumizi ya lugha
Lugha ndiyo
nyenzo kuu katika kazi ya fasihi, matumizi ya lugha hupita katika maeneo
matatu;
1.
Tamathali za semi
2.
Misemo, methali na nahau
3.
Matumizi ya picha na taswira
Tamathali za semi
Tamathali za Usemi ni matumizi ya
maneno kwa namna fulani ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia na kuifanya kazi ya
sanaa iwe ya kupendeza.
Baadhi ya tamathali za semi;
Tanakali za Sauti:Ni mbinu ya kutumia maneno
yanayoiga sauti au hali fulani. Mfano ‘nyau’.
Tashibiha: Hii ni mbinu ya lugha
inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha;
‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. Mfano, ‘mnene kama kabati’.
Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu
kisicho binadamu sifa ya mwanadamu. Mfano, ‘Panya akasema, “Nani atamfunga paka
kengele.”
Takriri: Ni
mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe
fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
Sitiari: Ni
mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama
‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, Magwangwala ni mwamba.
Mubaalagha: Ni
kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano. ‘Nina
nguvu nyingi, nilimpiga kofi punda akakohoa.’
Kuhakiki Maudhui
Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika
kazi ya fasihi.
Vipengele vya maudhui ni pamoja na;
1. Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo
mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika
makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
2.
Migogoro; hii ni mivutano na misuguano
mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika,
familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile
migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, migogoro ya nafsi, na migogoro ya
kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa
visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
3. Ujumbe; hili ni funzo
linalopatikana katika kazi ya fasihi.
4. Msimamo; Msimamo ni ile hali ya mwandishi
kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Ama ni jinsi ambavyo mwandishi
anatoa masuluhisho juu ya matatizo fulani katika jamii. Kuna aina mbili za
msimamo,
-
Msimamo
wa kiyakinifu/kimapinduzi;
msimamo huu huyaangalia mambo kisayansi na hutoa masuluhisho yanayoweza kuondoa
tatizo endapo yatafanyiwa kazi. Mfano suluhisho la umasikini wa nchi
zinazoendelea ni kufanya kazi kwa bidii.
-
Msimamo
wa kidhanifu;
msimamo huu msingi wake mkuu ni mambo ya kudhani tu na ni vigumu kuyathibitisha
kisayansi. Mfano. suluhisho la umasikini wa nchi zinazoendelea ni kumuomba
mungu.
5. Falsafa; ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa
na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Falsafa
ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.