‘ACT’ WAZARENDO NI ‘CCM’ KIBUBUSA?
Kibubusa ni
kufanya jambo bila ya kujulikana, yaani kisirisiri. Wazarendo hawa kama
wajiitavyo, wamekuwa wakizua maswali mengi kila kuchapo kama ni kweli hawa nao
ni wapinzani au ni maigizo na ngonjera zisizokwisha?
Kumbukumbu zinaeleza
wazi kwamba, aliyekuwa injini ya maarifa ya chama hicho, Profesa Kitila mwana
wa Mkumbo alipatiwa cheo serikalini akihusika na sekta ya maji ambayo hata
hivyo toka aingie hakuna mabadiliko yaliyofanyika labda ahadi. Hata hivyo kama
wasemavyo wanasiasa, tumpe muda, atatimiza.
Hivi punde,
aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Mama Anna Mgwira,
anatangazwa kumrithi Meck Sadick katika nafasi ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro. MGHWIRA
KAULA!
Maswali mengi
yanaibuka hapa, mosi, kama wapinzani wanapewa vyeo kwa lengo la kuonesha
ukomavu wa kisiasa, kwa nini ni ACT peke yao ndio wanaodondokewa na neema hii
ilhali kuna vyama vya upinzani zaidi ya 20 hapa nchini?
Pili, kama
utoaji wa vyeo hivi unalengo la kuua upinzani, ACT wanakipi cha kutisha hata
wauliwe? Kwa nini mbinu hii isitumike kuua CHADEMA, CUF na jamaa zao wa UKAWA?
ACT wanakazi
nzito ya kuwaaminisha watu kuwa wao sio CCM B. Kwa vyovyote vile, si jambo la
kawaida kwa serikali kumkabidhi mkoa mpinzani makini, kwani kufanya hivyo ni
kupunguza nguvu ya ushawishi ya chama chake katika mkoa huo. Sababu hii
imepelekea kwa miaka dahari, ukuu wa mikoa kupewa makada wa kufa na kupona bila
kujali uwezo wao wa kuchakata mambo ilimradi tu wanajua kusoma na kuandika.
‘ACT’ WAZARENDO NI ‘CCM’ KIBUBUSA? Swali hili
linaweza kujibiwa na kitu kimoja tu…
WAKATI.