Tofuati ya Mtindo wa Mazungumzo na Mtindo wa Maandishi

Ukumbi wa Nkrumah
Swali halisi: Kuna tofauti gani kati ya mtindo wa mazungumzo (Nkrumah) na mtindo wa maandishi (waandishi uliowasoma)? Toa hoja zako ukiegemeza mifano kutoka katika mdahalo wa lugha ya Kiswahili wa tarehe 19 Machi, 2017 Nkrumah.
Wamitila (2003), anasema ‘mtindo ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi kuwasilisha ujumbe  wake, huelezea mwandishi anavyounda kazi yake’.
Leech (1969), anasema mtindo ni namna ya uzungumzaji, uandishi au utendaji wa jambo fulani.
Kwa ujumla mtindo ni matumizi ya lugha yafanywayo na mwandishi au mzungumzaji kwa njia au namna maalum, Pia kupitia mtindo tunapata mtindo wa mazungumzo ambao huwasilishwa kwa njia ya mdomo na mtindo wa maandishi ambao kuwasilishwa kwake huwa ni kwa maandishi.
Kwa kuegemea mifano kutoka mdahalo uliofanyika Nkrumah, tofauti kati ya mtindo wa mazungumzo na mtindo wa maandishi inaweza kutolewa kwa ufafanuzi kama ifuatavyo;
Tofauti ya kwanza iko katika msamiati. Mtindo wa mazungumzo mara nyingi huchagua msamiati ambao huwa sio rasmi. Msamiati huo huitwa misimu, misimu hutumiwa kwa lengo la kufanya mazungumzo yavutie na sababu nyinginezo. Mfano, katika ukumbi wa Nkrumah, dokta Manoko alitumia msamiati wa kiingereza ‘extension officer’ akiwa na maana ya mtu wa idara ya nyuki. Pia profesa kiwara kutoka Muhimbiri alisema, “Mdahalo umejitokeza kwa sababu watu tuna matende kichwani” ‘matende kichwani’ sio msamiati rasmi katika lugha ya kiswahili. Pia dokta Kahangwa alisikika akisema, “acha maneno weka mziki.” Lakini katika lugha ya maandishi, msamiati rasmi hutumiwa zaidi na matumizi ya msamiati usio rasmi huepukwa. Massamba na wenzake, (2012), wametumia msamiati rasmi, maneno kama, ‘tungo, virai, vishazi na sentensi’ yametumika.
          Tofauti nyingine iko katika utendaji. Mtindo wa mazungumzo una ushirikishaji wa hadhira. Hadhira hushiriki kwa kupiga makofi, kutikisa kichwa kukubali au kukataa au kumalizia baadhi ya maneno. Mfano katika mdahalo wa Nkrumah mzungumzaji Adolph Mkenda aliposema “nimefurahi kuona Mkumbo hajafika.” Hadhira ilipiga makofi na kuangua kicheko. Pia Mama Salma Kikwete aliishirikisha hadhira pale alipouliza “usione vya elea…” hadhira nayo ilimalizia kwa kusema “vimeundwa”. Pia kuna wakati hadhira ilimkejeli Dokta Kadeghe azungumze lugha ya kiingereza kwa sababu tu alikuwa akiitetea lugha hiyo. Lakini katika mtindo wa maandishi, hadhira huwa haishirikishwi moja kwa moja. Mfano Nyerere, (1994:59) anaposema “kumbadili waziri mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.” Katika kifungu hicho cha maneno na kitabu kwa ujumla yake hadhira hana nafasi ya kuuliza swali, kushauri wala kupiga makofi hivyo hakuna ushirikishwaji wa hadhira.
          Tofauti nyingine ipo katika sintaksia, ambapo mtindo wa mazungumzo hutumia sentensi ndefu na maneno mengi. Mfano katika mdahalo wa Nkrumah, mbunge wa Afrika Mashariki Shyrose Bhanji, alitumia sentensi ndefundefu mpaka muda wake wa kuzungumza ukaisha na kumfanya akatishwe na Profesa Mutembei, hata hivyo Shyrose alikataa na kuendelea kuzungumza. Katika lugha ya maandishi, sentensi fupifupi hutumika pamoja na maneno machache ili kuepuka gharama ya karatasi nyingi na kumchosha msomaji. Mfano Hussein, (1969), “Mama tazama – nyumba ya Kinjekitile! Moshi!” uandishi huo umetumia sentensi fupifupi kwa makusudi maalumu.
Tofauti nyingine ni tofauti ya kifonolojia ambapo sifa za kiarudhi kama mkazo, kiimbo na lafudhi huweza kuonekana. Kwa upande wa lafudhi ni rahisi kumtambua mzungumzaji eneo analotoka kwa kusikiliza lafudhi yake, mfano mzungumzaji Dokta Sima kwa lafudhi yake ilikuwa ni rahisi kutambua kwamba, alitokea Arusha. Katika lugha ya maandishi si rahisi kutambua lafudhi, mkazo wala kiimbo. Mfano, Semzaba (2008), huwezi kuitambua lafudhi yake pale unaposoma kitabu chake.
          Mtindo wa mazungumzo na ule wa maandishi umetofautiana kwa kiasi kikubwa. Lakini pamoja na utofautiano huo, kuna mwingiliano wa baadhi ya vipengele katika mitindo hii, mfano, mtindo wa mazungumzo na ule wa maandishi hutegemea mwandishi au mzungumzaji ambaye ndiye huchochea mada husika. Kupitia elimu mitindo, mitindo mingi huweza kujadiliwa kwa marefu na mapana yake.
Marejeleo
Wamitila, K.W. (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Publishers.
Leech G. (1969). A Linguistic Guide to English Poetry. London: Longman.
Hussein A. (1969). Kinjekitile. Dar es Salaam: Oxford University Press.
Nyerere J. (1994). Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers Ltd.
Semzaba E. (2008). Marimba ya Majaliwa. Dar es Salaam: E&D Vision Publishing.

Massamba na wenzake. (2012). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2025

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1