Uchambuzi wa Mashairi ya Ahadi ya Mchawi na Msiba Uliotuangukia

 

Mchawi akiwa na mshumaa unaoelea juu ya mikono yake

Kwa kutumia mifano ya kutoka katika mashairi ya Ahadi ya Mchawi na Msiba Uliotuangukia (Kahigi na Mulokozi 1973), fafanua viwango vifuatavyo vya uchanganuzi wa mtindo: 3) kiwango cha sintaksia na 4) kiwango cha maana.

Kitabu cha Mashairi ya Kisasa chao Mulokozi na Kahigi, kilipata kuandikwa mwaka 1973 kikiakisi hali ya wakati ule, japo pia kinaweza kikaakisi hata mambo yanayotokea hivi leo, au yaliyotokea kabla ya kitabu hicho hakijapata kuandikwa. Miongoni mwa mashairi yanayopatikana katika kitabu hiki yanahusu mapenzi, siasa, misiba, ukulima na mashairi ya aina nyingine. Mashairi yote yametumia mtindo wa kisasa, mtindo ambao haufuati kanuni za kimapokeo za utungaji wa mashairi. Kitabu hiki kinakwenda kinyume na kanuni za uandishi wa mashairi zilizoelezwa na marehemu Kaluta Amri Abedi katika kitabu chake cha ‘Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri.’ Lengo kubwa la kutumia mtindo huu wa kisasa ni kuwafanya waandishi chipukizi hasa wale wa bara waamini kuwa sanaa ya ushairi si ngumu. Dhana ya sintaksia imejadiliwa na wataalamu mbalimbali:
Kwa mujibu wa Besha (1994), sintaksia inahusu uchambuzi na ufafanuzi wa muundo wa lugha. Hata hivyo maana hii haitoshi kuelezea dhana ya sintaksia.
Mtaalamu mwingine, O’Grady (1994), anaeleza kuwa, sintaksia ni taaluma inayochunguza jinsi maneno yanavyounganishwa ili kupata vipashio vikubwa – sentensi.
Kwa ujumla, sintaksia ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi wa miundo ya tungo na kanuni mbalimbali za lugha zinazotawala miundo hiyo.
Kwa upande mwingine, maana ya semantiki imepata kuelezwa na wataalamu mbalimbali kama inavyooneshwa:
Kwa mujibu wa Crystal (1987), semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha.
Maana nyingine ya semantiki inaelezwa kuwa “ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno na tungo katika lugha” (Massamba, 2004:75).
Kwa ujumla, semantiki ni taaluma ambayo hushughulikia maana ya maumbo au sentensi katika lugha.
Mashairi ya Ahadi ya Mchawi na Msiba uliotuangukia ni mashairi yanayotoka katika kipengele cha misiba katika kitabu cha Mashairi ya Kisasa. Ahadi ya Mchawi linapatikana ukurasa wa 18 na Msiba Uliotuangukia likikaa katika ukurasa wa 19. Ufuatao ni ufafanuzi wa viwango vya uchanganuzi yaani kiwango cha sintaksia na kiwango cha maana.
Kwa kuanza na kiwango cha kisintaksia, katika Ahadi ya Mchawi, aina mbalimbali ya virai vimetumika, miongoni mwa virai hivyo ni virai vitenzi. Mfano wa virai hivyo ni:
                             ‘utakapokufa’ na ‘nitakusagasaga’
Katika virai hivyo, njeo ya wakati ujao imetumika. Dhima ya njeo hiyo ni kutoa taarifa juu ya maamuzi yatakayofanywa baadaye. Pia njeo hii, inaonesha ahadi ya mchawi, ambalo ndilo jina la shairi hili, hivyo njeo hii imetumika kusadifu shairi na jina lake.
Kadhalika, virai nomino vimetumika. Virai hivi ni changamani na uchangamani huo upo katika sifa ya ukumushi kama vinavyooneshwa katika mfano:
                             ‘binadamu hai’ na ‘maitiyo nitayatumia’
Katika mfano huo kirai nomino hai, kinakumusha kirai nomino binadamu. Pia virai nomino hivyo vimetumiwa kwa lengo la kufufua matarajio mema ya watu wa tabaka la chini wanaonyanyaswa.
Katika shairi la Msiba Uliotuangukia virai mbalimbali vimetumiwa, ikiwa ni pamoja na virai nomino kama inavyooneshwa katika mfano huu:
                             ‘Wengine wakawa wanalialia’
Kirai nomino ‘wengine’ ni kiwakilishi kinachotoa taarifa juu ya hao watu wengine ambao walikuwa wakilialia kwa sababu ya manyanyaso waliyokuwa wakifanyiwa na zimwi.
 Vilevile virai vitenzi vimetumiwa, kama inavyoonekana katika mfano:
                             ‘Wakakaa wamenyoosha shingo zao’
Kirai kitenzi hiki kinamsaidia mwandishi kuepuka matumizi ya wakati uliopita ili kuvuta makini ya msikilizaji. Hivyo kirai hicho kinalenga kuifanya kazi iwe yenye wakati timilifu au uliopo.
Pamoja na hayo, vishazi mbalimbali vimetumika. Katika Ahadi ya Mchawi, kuna vishazi huru mbalimbali, mfano:
1.   ‘Nitakoka moto na kukukaanga’
2.   ‘Unga wako nitaufungafunga’
Kishazi cha kwanza hapo juu, kina kitenzi elekezi, ‘nitakoka’. Pia mfano wa pili, kitenzi nitaufungafunga kina dhima ya kujaziliza tungo ‘unga wako’. Pia vishazi huru hivyo vinadokeza vitendo ambavyo atafanyiwa adui atakapokufa.
Zaidi ya hayo, vishazi tegemezi vimetumika kama inavyooneshwa katika mfano:
1.   ‘ajapo mtu asokotwa tumboni’
2.   ‘ajapo mtu amekatwa vitani’
Vishazi hivi vimetumia miundo ya kipekee ambayo inaibua taharuki kwa wasomaji, na kuwafanya wajiulize baada ya hapo nini kitatokea.
Vilevile katika shairi la Msiba Uliotuangukia, vishazi mbalimbali vimetumika, miongoni mwa vishazi hivyo ni vishazi huru:
                             ‘Tulikuwa hatujaliona zimwi’
                             ‘Wengine wakatetemeka kwa hofu’
Vishazi hivi vimetumia maneno muhimu ambayo yanalenga katika kuvuta makini ya msomaji.
Juu ya hayo, vishazi tegemezi navyo vimetumika. Ifuatayo ni mifano ya vishazi hivyo:
                             ‘Na tukitaka kupaendea huko’
                             ‘Katunyamazisha sote na kusema’
Vishazi hivi vina dhima ya kujenga mtiririko wa kazi kwa kuweka utegemezi wa matukio au jambo moja kufuata jambo lingine.
Kipengele kingine ni sentensi. Aina za sentensi zinaangaliwa kwa kuzingatia vigezo viwili, kimuundo na kidhima. Kwa kuanza na kigezo cha kimuundo cha sentensi katika Ahadi ya Mchawi, aina mbalimbali za sentensi zimetumiwa miongoni mwazo ni:
Aina ya kwanza ya sentensi iliyotumika katika kigezo cha kimuundo ni Sentensi sahili. Sentensi hii inaoneshwa katika mfano huu.
                             ‘utakapokufa nitakuzikua.’
Sentensi hii ina jumla ya maneno mawili. pia inaonesha uwezo alionao mchawi, ikiwa ni pamoja na ujasiri mkubwa wa kufanya mambo magumu kama kuzikua.
Katika Msiba Uliotuangukia, mojawapo ya sentensi sahili iliyotumika ni.
                             ‘Akili zetu kweli zikazinduka’
Sentensi hii ina jumla ya maneno manne. Imetumiwa kwa makusudi ya kuongeza taharuki, wasomaji watajiuliza swali, baada ya akili kuzinduka kipi kilifuata?
Aina nyingine ya sentensi ni sentensi changamani, kama inavyooneshwa katika mfano huu chini.
                             ‘ajapo mtu asokotwa tumboni, nitamzolea konzi ajilie.’
Uchangamani wa sentensi hiyo katika mfano unatokana na utegemezi, kwamba maana haingepatikana bila kuongezwa kishazi huru, ‘nitamzolea konzi ajilie.’ Dhima ya utegemezi huu, ni kufanya taarifa ya mwisho ijichomoze kuliko nyingine. Wasomaji hawatakipa umuhimu mkubwa kishazi tegemezi kwa sababu hakina taarifa mpya. Hapa mwandishi katumia kanuni ya kipeo cha mwisho ambayo hudai kuwa, taarifa itolewayo mwishoni ni muhimu zaidi.
Katika Msiba uliotuangukia, sentensi changamani zimetumika kama inavyooneshwa katika mfano.
                             ‘Tulokuwa tumebaki kushangaa, tukaanza akili kuzitumia.’
                             ‘Walokuwa wazidi kutetemeka, kutetemeka kwao kukapunguka.’
Uchangamani katika sentensi hiyo ni wa kiutegemezi. Dhima ya utegemezi katika sentensi hiyo ni kuifanya hadhira itilie mkazo zaidi vishazi huru, ambapo vishazi huru hivyo vinamawazo chanya yanayoashiria ushindi. Vishazi hivyo vinaasa watu watumie akili na wasiwe waoga.

Pia kwa kutumia kigezo cha kidhima, aina mbalimbali ya sentensi zinapatikana katika shairi la Ahadi ya Mchawi. Miongoni mwa sentensi hizo ni:
Sentensi masharti. Mfano, ‘utakapokufa nitakuzikua.’ Sentensi hii inatoa masharti ya utokeaji wa matukio mbalimbali. Inayafanya matukio yawe yanayotegemeana katika matini.
Vilevile, sentensi hisishi zimetumika. Mfano, ‘Ajapo binamu aumwa kichwani nitachukua kidogo nimtie’. Sentensi hii inaibua hisia za hudhuni na chuki.
Katika Msiba Uliotuangukia, sentensi hisishi iliyotumika ni, ‘wamekwisha kufa, zimwi kulilisha.’ Sentensi hii inaibua hisia za hudhuni dhidi ya zimwi. Ni dhahiri kuwa wasomaji watalichukia zimwi, hivyo hii ni fursa pekee anayoipata mshairi katika kuibua fikra mpya.
Pia shairi la Msiba uliotuangukia limeibua aina tofauti za sentensi ambazo ni, sentensi taarifa. Mfano wake unaoneshwa.
                             ‘kwa kweli tulikuwa hatulijui.’
Sentensi hii imetumika kama mwanzo wa shairi hili. Ni katika sentensi hii ndipo mwanzo wa kuvutia unapatikana hivyo makini ya wasomaji inavutwa na kuwafanya waendelee kusoma shairi hili.
Aina nyingine ya sentensi iliyotumiwa ni sentensi ulizi. Sentensi hii inasema, ‘tusije kuamka – kwa wake uganga?’ Dhima ya sentensi hii ni kuishirikisha hadhira, ushirikishaji huu wa hadhira unaifanya kazi hii iwe hai na inayovutia.
Kiwango kingine cha uchanganuzi kinachojadiliwa hapa ni kiwango cha maana. Lengo la kiwango hiki ni kupata maana ya vipashio kama neno, virai, vishazi na sentensi.
Katika Ahadi ya Mchawi, kiwango cha maana kinafafanuliwa kama ifuatavyo.
Maana ya shairi. Shairi la Ahadi ya mchawi linahusu mtu mbaya anayesababisha dhiki kwa watu. Mtu huyu kwa maovu yake, anasababisha watu waugue, mfano, mshairi anasema, ‘ajapo mtu aumwa…’ pia mtu huyu anasababisha vita na njaa. Mtu huyu ni mlanguzi na mfanya biashara za magendo tena ni adui wa ujamaa.
Kwa upande mwingine, maana ya shairi la Msiba Uliotuangukia, ni ukoloni. Linazungumzia namna ambayo watanzania walitawaliwa na jinsi walivyoungana pamoja ili kumwondoa mkoloni. Maana ya shairi hili imejengwa na vipengele vidogovidogo kama, taswira. Mfano, taswira ya zimwi ikimaanisha ukoloni na mnuko ikimaanisha shida zilizotokana na ukoloni. Pia matumizi ya tashibiha nayo yamesaidia sana katika kuijenga maana ya shairi hili. Mfano, na waliokuwa wako kama mabubu. Ikimaanisha ukimya waliokuwa nao watu wakati wa kipindi cha ukoloni.
Kipengele kingine ni msamiati. Katika Ahadi ya Mchawi, msamiati wa kawaida umetumika kwa kiasi kikubwa isipokuwa msamiati mmoja tu, ‘umemenga’. Msamiati wa kawaida umetumika ili kuwafanya wasomaji waweze kuielewa matini. Pia katika kipengele hiki msamiati rasmi umetumika. Msamiati kama kufa, maiti na kidogo ni rasmi. Msamiati rasmi umetumika ili kurahisisha uelewekaji wa shairi hilo. Hata hivyo msamiati usio rasmi nao umetumika, mfano ‘umemenga’. Lengo la kutumia msamiati huo ni kuihakikishia hadhira au wasomaji kuwa shairi hili linatoka katika mazingira yao ya kibantu na hivyo kuamini kuwa kazi hii inazungumzia mambo yanayoihusu jamii.
Kaika Msiba Uliotuangukia, msamiati mgumu na mwepesi umetumika. Mfano wa msamiati mgumu ni, rajua – ikimaanisha matumaini, uki – ikimaanisha asali na  mswano – ikimaanisha utamu. Lengo la matumizi ya msamiati mgumu ni kuwafikirisha wasomaji.
Kipengele kingine ni virai. Katika Ahadi ya Mchawi, virai mbalimbali vimetumika kwa makusudi maalumu. Mojawapo ya virai hivyo ni virai nomino. Mfano ‘maitiyo nitayatumia.’ Kirai hiki kinamaana kwamba mshairi atatumia kifo cha adui kuboresha maisha ya watu aliyoyaharibu. Dhima ya kirai hiki ni kurudisha matumaini ya wanyonge.
Katika Msiba uliotuangukia, virai nomino vimetumika. Mfano, ‘viongozi walikuwa wakilialia.’ Maana ya kirai hiki ni vilio walivyokuwa navyo viongozi wa jamii ya kiafrika baada ya kuvamiwa na wakoloni.
Aina nyingine ya virai vilivyotumika ni virai vitenzi. Katika Ahadi ya Mchawi, kirai kitenzi ‘umemenga’ kimetumika. Kirai hiki kinamaanisha pale ambapo maiti ya adui itakapokuwa imekaushwa.
Katika Msiba Uliotuangukia, kirai kitenzi, ‘wakakaa wamenyoosha shingo zao,’ Kimetumika. Kirai hiki kinamaanisha kundi la watu waoga ambao huliangalia tatizo bila kulitatua. Mshairi anaamsha fikra mpya kwa wanachi, aghalabu wanapokutana na matatizo ni vyema kuyatatua na si kuishia kuyatazama.
Kipengele kingine ni vishazi. Katika Ahadi ya Mchawi, vishazi huru vimetumika. mfano,
                             ‘katika chungu changu nitakutia’
Kishazi hicho kina maana kwamba, mshairi atampoteza kabisa adui wa watu kwa kumuweka ndani ya chungu. Na kupitia kumpoteza huko, atatumia nafasi hiyo kusaidia wanyonge.
Katika Msiba Uliotuangukia, vishazi huru vimetumika kama mfano mmojawapo wa vishazi hivyo unavyooneshwa hapa chini.
                             ‘Tulikuwa hatujaliona zimwi’
Kishazi hiki kinatoa maana kwamba jamii ya watanzania ilikuwa haijauona ukoloni hapo kabla. Pengine ndio sababu iliyopelekea wakoloni waweze kutawala kwa urahisi.
Aina nyingine ya vishazi vilivyotumika ni vishazi tegemezi, katika Msiba uliotuangukia, mfano wa kishazi tegemezi unaoneshwa.
                             ‘ajapo mtu asokotwa tumboni.’
Kishazi hiki kimetumika kwa lengo la kujenga taharuki kwa wasomaji. Msomaji atatamani kujua hatma ya kila tukio.
Katika Ahadi ya Mchawi, kishazi tegemezi hiki kimetumika, ‘Na tukitaka kupaendea huko.’ Kishazi hiki kinamaana kwamba, watu wote wenye njaa, watapatiwa chakula. Pia kishazi hiki tegemezi kinaamsha taharuki kwa msomaji.
Kipengele kingine ni sentensi. Kwa kujikita katika kigezo cha maana aina mbalimbali za sentensi zimeweza kuonekana katika mashairi yote mawili.
Katika Ahadi ya Mchawi, sentensi masharti isemayo, ‘utakapokufa nitakuzikua.’ Imetumika. Maana yake ni kwamba, pale ambapo adui atakufa, mshairi atahakikisha anaifukua maiti yake kisha kumkaanga ili kumpoteza kabisa. Sentensi hii haikutumiwa kwa bahati mbaya, bali inalenga kujenga fantasi kwa wasomaji.
Katika Msiba Uliotuangukia, sentensi taarifa isemayo, ‘kwa kweli tulikuwa hatulijui.’ Sentensi hii, kama lilivyojina lake, inatoa taarifa iliyokuwa nayo jamii kuhusu ujinga kuhusiana na wakoloni.
Katika Ahadi ya Mchawi, sentensi hisishi hii imetumika, ‘Ajapo mtu amekatwa vitani, nitachukua kidogo nimtie.’ Maana yake ni kwamba, kwa mtu yeyote katika jamii ambaye atapatwa na tatizo, mshairi yuko tayari kumsaidia. Sentensi hisishi hii imetumiwa kuamsha hisia za msomaji.
Katika Msiba Uliotuangukia, sentensi hisishi hii imetumika, ‘Wamekwisha kufa, zimwi kulilisha.’ Sentensi hii, inamaanisha unyonyaji uliokuwa unafanywa na wakoloni. Unyonyaji huu ulipelekea maisha ya watawaliwa kuwa magumu.
Aina nyingine za sentensi zilizotumika katika shairi la Msiba Uliotuangukia ni:
Sentensi taarifa. Mfano, ‘kwa kweli tulikuwa hatulijui.’ Sentensi hii inatoa taarifa na kumwelewesha msomaji juu ya ujinga waliokuwa nao wanajamii kuhusiana na suala la ukoloni.
Juu ya hayo, sentensi ulizi imetumika. Mfano, ‘nchi iliyojaa uki na maziwa?’. Sentensi hii inatumia msamiati mgumu uki, ikiwa na maana ya asali. Sentensi hii inayataja matarajio waliyokuwa nayo wanajamii. Ni dhahiri kuwa walichoshwa na jinsi walivyomezwa na zimwi ambalo ni ukoloni, walitamani warejee maisha yao kabla ya ukoloni ambapo maisha yalikuwa mazuri yenye usawa kwa watu wote.
Kwa kuhitimisha. Shairi la Ahadi ya mchawi na Msiba uliotuangukia, ni mashairi ambayo yanauhalisia na jamii ya kitanzania. Mashairi haya yaliandikwa miaka ya 1970, ambapo ni katika miaka hii, ndipo Tanzania ilianza taratibu kuporomoka kiuchumi. Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu kwa jamii ya watanzania. Mashairi haya na mengine yanayopatikana katika kitabu cha Mashairi ya Kisasa, yanalenga katika kuijenga jamii mpya. Jamii mpya itajengwa kwa kuondoa maovu yote ambayo yamekuwa yakifanyika katika jamii. Ujenzi wa jamii mpya ni suala la muda mrefu. Hata leo hii bado jamii yetu haijabadilika, hivyo ni vyema yale yanayosemwa na washairi kama hayataishiwa kusomwa tu na kuachwa vitabuni, bali yafanyiwe kazi ili kuweza kuikomboa jamii yetu inayoserereka katika giza, bila dira, bila mwanga.
MAREJELEO
Besha, R.M, (1994). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Kahigi, K & Mulokozi, M, (1973). Mashairi ya Kisasa. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House Limited.
Massamba P. B. D, (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1