RIWAYA| SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (22)
KAMA ULIIKOSA SEHEMU ILIYOPITA ISOME HAPA: SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (21)
Kisha endelea kuisoma...
Mzee Samike alikuwa uvunguni.
Nilistaajabu nikauliza, “umefikaje nami nimekuacha nje?” hakunijibu. Alicheka
akitoka chini ya uvungu na kukaa kitandani.
“Unafahamu kisa cha mimi
kupelekwa jela?” aliniuliza.
“Sifahamu mzee…”
“Nilimfanyia mauzauza afisa mmoja
wa jeshi la polisi. Kwa hasira akanitengenezea kesi bandia. Hata hivyo
hawakuniweka sana wakaniachia!”
“Ndiyo mzee… nilikuona gerezani
nikiwa katika harakati za kukutafuta!”
“Hata mimi nilikuona!” Alijibu,
tukabaki tukitazamana kwa mshangao!
“Chakula chako kiko sebuleni… kwa
sasa nahitaji kuzungumza nawe kuhusu kuyakomesha haya mauzauza yako,” mzee
alisema. Nikapata matumaini.
Tulifanya mazungumzo yaliyonipa
matumaini makubwa. Mzee alinambia amekwisha mzuia mtu wa ajabu na kamwe sitamuona
tena. Nilifurahi nikashangilia kwa ushindi. Pia, mzee alisema hapendi kuniona
nikihangaika na kazi zisizoeleweka, akaniomba nihamie kwake ili nishirikiane
naye katika shughuli ya uvuvi. Sikuwa na pingamizi, nilikubali mwenye furaha ya
kutosha. Nikiwa na matumaini ya kufanikiwa na kudhani mwisho wangu wa kupambana
na vitu vya ajabu ulifika, jambo jipya likaongezeka.
“Asante kwa kukubali kuishi hapa
na kushirikiana nami katika shughuli za uvuvi,” mzee alishukuru, “hata hivyo,
kuna kazi naomba unisaidie!”
“Kazi gani tena mzee? Uvuvi ndo
huu… kuna kingine?” nilihoji.
“Ndiyo… mjukuu wangu Chimota hakufa
kama unavyodhani!”
“Tobaaah!” nilishtuka.
“Amini… mimi nilizaliwa na ulozi
wangu mkononi. Wachawi wote walinifuata kunitaka nijiingize katika uchawi wao
na wanga. Nilikataa kufanya uchawi wa kuwadhuru watu, sikukubali… sikuwa tayari
kumkamata mwanadamu mwenzangu nimfanya msukule… nilipinga jambo hilo.
“Basi wanajumuiya wenzangu
wakaniona msaliti kwao, wakafanya hila za kila namna. Wakanichonganisha na
wanajamii wote wanaonifahamu hata nikakosa rafiki. Watu wote wakaniogopa kuwa
mimi ni mtu hatari ninayesababisha misiba ya watoto wao… kuogopwa huku ndiko
kumenifanya leo hii niishi katika jumba hili la upweke.
“Walipoona wamenichonganisha na
kunikosesha amani kwa kila kitu, ndipo walipoamua kuniharibia familia yangu
pekee niliyoishi nayo kwa furaha. Walimchukua binti yangu mapema sana baada ya
kujifungua. Walimtia uzuzu, akapambana nao kisu kwa kisu, wakaona wakimwacha
atawamaliza wakamwua na kumtupa katika bonde la hasara.
“Binti yangu aliniachia kijukuu
kizuri cha kiume… jina lake Chimota. Alilala hapo ulipolala wewe, nilipenda
alivyoota. Ndoto zake zilijaa matumaini. Kuna kipindi aliota chuki kati ya
watawala na watawaliwa imekwisha nayo roho ya kisasi imemezwa na kumeng’enywa.
Kuna wakati aliniacha hoi alipoota ati vijana wote wenye nguvu kawaona wamepata
kazi, hakuna hata mmoja anayekaba na kufanya uzinzi kama uliofanya wewe Mako.
“Wachawi hawakufurahishwa na
hikima iliyojaa katika kichwa cha mjukuu wangu Chimota. Wakambeba. Watu wote
hudhani Chimota alikufa… la hasha! Chimota yungali hai katika nchi ya matumbawe.
Kavundikwa na hawaishi kutaka kumbadili awe na akili kama zao. Awe katili kama
wao. Hawataweza!” mzee alimaliza, nami nikauliza swali:
“Bila shaka unahitaji msaada wa
kumrejesha mjukuu wako, lakini mimi si mlozi. Huoni kama watanipiga kwa pigo
moja tu mzinzi mimi?”
“Asante kwa kunielewa… ishi na
mimi, nitakufua vyema na hakuna atakayeweza kupambana na wewe! Chimota atarudi.
Nawe utamrejesha!
Tulimaliza mazungumzo yale na
mzee. Nikamwomba ruhusa nifuate vitu vyangu ili nihamie kabisa mahali pale.
Mzee hakusita, aliniruhusu nami nikatumia masaa matatu kukamilisha shughuli ya
uhamishaji wa vifaa vya kapuku.
Asubuhi sana, mimi na mzee
tuliongozana kuelekea baharini. Mzee alivalia kaptura ya kijivu na shati jeupe
lililochoka kiasi. Mimi nilikuwa na suruali nyeusi na fulana ambayo kusema
kweli siitambui rangi yake kwa sababu ya ule mpauko ilioupata baada ya kuwekwa
mwilini kwa miongo kadhaa. Basi mimi na mzee tukatembea haraka kuiwahi safari
ya kuvua samaki.
Tulifika baharini mzee akafungua
nanga ya mtumbwi wake na pasipo kupoteza muda, mtumbwi ukaivamia bahari na
kuisabahi kwa salamu ya kuwataka samaki wa maji chumvi.
“Mzee sasa tumezama chumvini!”
nilitania. Mzee akacheka!
Mtumbwi ulisogea taratibu hata
tukafika mbali. Lakini ghafla mimi na mzee tuliliona wimbi kubwa likija.
Nikapatwa na mshituko mkubwa nisiyejua cha kufanya.
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21
Shusha maoni yako mdau!...