Udhamini wa Kazi za Fasihi

UDHAMINI WA KAZI ZA FASIHI

Udhamini ni tendo la kumchukulia mtu dhamana au kugharamia kitu fulani. Udhamini umegawanyika katika aina mbili ambazo ni:
-      Udhamini wa ushawishi.
-      Udhamini wa nguvu.

Udhamini wa ushawishi

Udhamini huu huwashawishi watu kwa vitu vivutiavyo kama pesa.
UDHAMINI WA NGUVU
Huu hutumia nguvu na mabavu. Kama ni serikali basi hutumia vyombo vyake vyote vya usalama kama: Jeshi, polisi na magereza.

Sababu za udhamini

i.             Ukosefu wa fedha kwa waandishi. Waandishi wengi huwa hawana fedha za kuweza kuchapa miswada ya kazi zao. Hivyo hutegemea kupewa msaada fulani kutoka watu wenye fedha ili waweze kutimiza azima hiyo. Nchini Tanzania, kuwepo kwa vitabu vya fasihi ya watoto kulitokana na udhamini uliofanywa na mashirika ya nje.
ii.            Kutafuta umaarufu. Hii hutokea pande zote mbili. Inawezekana mdhamini akataka kupata umaarufu kupitia kazi za mwandishi anayefahamika, au mwandishi akataka kupata umaarufu baada ya kazi yake kudhaminiwa na kutoka.
iii.           Kutafuta fedha. Waandishi wengi hutafuta udhamini ili waweze kujipatia fedha kupitia kazi zao. Kadhia hii imepelekea kuongezeka kwa kazi za fasihi zilizojaa mahaba mengi na mafunzo kiduchu.
iv.          Kulazimishwa. Kuna wasanii hufanyiwa udhamini wa lazima. Nao kwa kuhofia kazi zao kushindwa kusomwa au kudhibitiwa hujikuta wakikubali yaishe na kuanza kufanya kama jinsi mdhamini anavyotaka.

Hasara za udhamini

i.             Msanii anakuwa mtumwa wa mdhamini. Msanii hutakiwa kuandika yale ambayo yanakubalika kwa mdhamini, hii humpotezea uhuru wake wa kuandika kile kinachoifaa jamii yake.
ii.            Kulingana na uduchu wa fedha zitolewazo na mdhamini, mapana ya uandishi wa msanii hupungua na kujikuta akiandika kazi ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha.
iii.           Kazi ya mwandishi huwa ni mali ya mdhamini. Hii huambatana na kuendeleza maslahi ya mdhamini.
iv.          Waandishi huanza kuandika kazi zao kwa kutafuta pesa. Mlengo wa wasanii kutoka kuikomboa jamii na kuielimisha hutenguka na kujikuta wakiandika kazi zitakazo waingizia kipato na kumfurahisha mdhamini.
v.           Kuibuka kwa matabaka. Tabaka la mwenye nacho husimama mdhamini na asiyenacho huwakilishwa na msanii mwenyewe. Katika matabaka haya mawili, mahusiano ya kinyonyaji yametawala ambapo mdhamini humnyonya msanii.
vi.          Kuibuka kwa fasihi mpya. Udhamini umepelekea kuibuka kwa uandishi mpya wa fasihi – fasihi pendwa. Kazi hizi za fasihi hazina uhalisia na jamii yetu, lakini ndizo hupendwa sana na kusomwa na watu wengi.

Faida za udhamini

i.             Huwasaidia waandishi wapya kuchapisha kazi zao na jamii kuweza kuzisoma.
ii.            Kwa kuwa mdhamini hutoa fedha, wasanii huweza kufanya utafiti ili kuandika kazi bora zaidi.

iii.           Udhamini husaidia kazi ya mwandishi kuweza kuifikia jamii na kuufanya ujumbe wake usomwe na kusaidia harakati za ujenzi wa jamii mpya.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024