Uhakiki wa Riwaya ya Takadini
RIWAYA: TAKADINI
MWANDISHI: BEN J HANSON
WACHAPISHAJI: METHEWS BOOKSTORE
AND STATIONERS
MWAKA: 2004
MHAKIKI: DAUD MAKOBA
Muhtasari wa Riwaya
Takadini ni riwaya inayojaribu
kuzungumzia matatizo ya mila na desturi yaliyopo katika jamii za Kiafrika hasa
sehemu za vijijini. Mwandishi anamuonyesha mhusika mkuu Takadini aliyezaliwa na
ulemavu wa ngozi jinsi anavyotengwa na watoto, watu wazima na jamii yote kwa
ujumla. Mwisho tunamuona Takadini akipendwa na msichana Shingai. Pamoja na
vikwazo vingi, penzi la Shingai na Takadini halikufa. Baadae Shingai anapata
mimba ya Takadini, kisha anajifungua mtoto asiye mlemavu. Hapo wana jamii
wanashangazwa na kujikuta wakiamini kuwa hata mlemavu anaweza kuzaa mtoto
asiyemlemavu.
Uchambuzi wa Fani na Maudhui
Maudhui Katika Riwaya ya Takadini
Dhamira
Ukombozi wa Kiutamaduni
Utamaduni ni jumla ya maisha ya
jamii. Katika jamii ya Zimbabwe watu wenye ulemavu hawakuruhusiwa kuishi,
waliuawa kikatili. Ni katika jamii hii pia, watu waliendelea ushikilia mila na
desturi zilizokuwa zinamkandamiza mwanamke. Shingai anachaguliwa mume na
kulazimishwa kuolewa naye bila ridhaa yake.
Ni wakati sasa jamii inatakiwa
kufunguka na kuzirekebisha mila zote zilizopitwa na wakati kwani mabadiliko ni
sisi wenyewe.
Katika riwaya hii, mwanamke
ameleta mabadiliko ya mila na desturi mbovu. Mwandishi anasema, “… Sekai wewe
na Takadini mmebadilisha mambo mengi kijijini hapa. Kwa sasa sifikirii kama
kuna mtu yeyote atakuwa na moyo wa kuharibu watoto wachanga, masope na wenye
ulemavu…” (uk 26)
Mapenzi
Mapenzi yamejadiliwa katika
nyanja mbili, yaani mapenzi ya kweli na yasiyokuwa ya kweli.
Sekai ana mapenzi ya kweli kwa
mwanaye Takadini, ndiyo maana alikuwa tayari kufa kwa ajili yake. Shingai naye
anamapenzi ya kweli kwa Takadini, kwani alimkataa Nhamo na kuolewa na Takadini
bila kujali ulemavu wake. Mzee Chivero ana mapenzi ya kweli na dhati kwa Sekai.
Alimtunza Sekai na mwanaye.
Kwa upande wa mapenzi yasiyokuwa
ya kweli, yupo mzee Makwati, huyu hana mapenzi ya kweli kwa mwanaye Takadini,
anasubiri uamuzi wa wazee ili mwanaye aweze kuuawa. sekani anampinga mumewe
vikali kwa kusema, “Ni mtoto wangu wa kwanza niliyemsubiri kwa miaka mingi.
Siwezi kukubali kumpoteza.” Vilevile kijiji cha mzee Makwati hakikuwa na
mapenzi ya kweli kwa Takadini, kwani isingekuwa juhudi ya Sekai kutoroka na
mwanaye, ni lazima mtoto angeteketezwa.
Ujasiri
Ujasiri umetumika kuleta ukombozi
wa kiutamaduni katika riwaya hii. Tunamuona Sekai akitoroka nchi yake na kwenda
nchi nyingine. Kutokana na ujasiri wake huo, anafanikiwa kumlinda mwanaye
Takadini dhidi ya watu wote waliokuwa wanataka kumwangamiza. Vilevile yupo
Shingai, msichana huyu anakataa kuolewa na Nhamo kwa sababu halikuwa chaguo
lake. Chaguo la Shingai ni Takadini, mwanamume aliyempenda kwa moyo wake wote.
Kwa ujasiri anasema, “Huyu ndiye mtu ninayemtaka mimi.”
Jamii yetu ni lazima iwe jasiri
katika kupambana na mila zote mbaya. Isifumbie macho wala kuyaacha matatizo ya
mila na desturi mbovu yaendelee kuwaumiza wanyonge.
Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii
Mwanamke amejadiliwa kwa mazuri
na mabaya yake:
-
Jasiri
na mwenye kutetea haki. Sekai ni jasiri, anatetea haki ya mwanaye – haki ya
kuishi.
-
Mama
mlezi wa familia. Wanawake waliachiwa jukumu la kulea familia kama mama
Shingai.
-
Duni.
Baadhi ya wanaume walikuwa wakiwapiga na kuwadharau wake zao. Mwandishi
anasema, “Nhariswa alimpiga mkewe kichwani na usoni mara kadhaa lakini mkewe
hakuweza kujibu.” (uk 19).
-
Mwanamapinduzi.
Sekai na Shingai wanaleta mabadiliko katika jamii yao. Silaha kubwa waliyotumia
ni ujasiri.
Malezi
Wanawake waliachiwa jukumu la
kulea familia. Baba Shingai anauliza, “Hukumfundisha mwanao maana ya tendo
hilo, we?” (uk 96).
Hii inaonyesha ni jinsi gani hata
kwenye jamii yetu wanavyohangaika na malezi ya watoto peke yao. Suala la malezi
sio la kumwachia mama peke yake, bali ni jambo ambalo linatakiwa litekelezwe na
wazazi wote wawili.
Ujumbe
Ujumbe ni funzo litolewalo na
kazi ya fasihi. Mafunzo mengi yametolewa katika riwaya hii.
i.
Binadamu
wote ni sawa.
ii.
Uchungu
wa mwana aujuaye mzazi.
iii.
Ndoa
ni makubaliano ya watu wawili na haipaswi kuingiliwa na mtu yeyote.
iv.
Malezi
ya watoto yasimamiwe na wazazi wote wawili.
v.
Jamii
iachane na mila potofu.
Migogoro
Migogoro ya wahusika
-
Sekai
na jamii ya Makwati. Huu unasababishwa na Sekai kujifungua mtoto sope. Suluhisho
la mgogoro huu ni Sekai kutoroka nchini kwake na kwenda kuishi ugenini.
-
Nhamo
na Takadini. Huu unasababishwa na Takadini kupendwa na Shingai, msichana
aliyeamrishwa kuolewa na Nhamo. Hakuna suluhisho la mgogoro huu.
-
Shingai
na wazazi wake. Wazazi wa Shingai wanamkataza asiolewe na takadini kwani
alikuwa sope. Suluhisho la mgogoro huu ni Shingai kukaidi agizo la wazazi wake
na kuamua kuolewa na Takadini.
Mgogoro wa nafsi
Mgogoro huu unampata Sekai baada
ya kuzaa mtoto Sope. Anafikiria kuhusu suluhisho la maisha ya mwanaye
anayewindwa auawe na wananchi wanaoshikilia mila na imani potofu. Suluhisho la
mgogoro huu ni Sekai kukimbilia nchi ya mbali.
Migogoro mingine iliyojitokeza ni
migogoro ya kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii.
Falsafa
Mwandishi anaamini kuwa, wanadamu
wote ni sawa.
Mtazamo/Msimamo
Mwandishi ana msimamo wa
kimapinduzi kwani anaitaka jamii itumie ujasiri kuyaondoa matatizo yote
yasababishwayo na mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Uchambuzi wa fani na Vipengele Vyake
Fani ni ule ufundi wa kisanaa
anaoutumia msanii katika kazi zake. Fani ndiyo hutupatia kile kiitwacho
maudhui. Katika riwaya hii, fani imechambuliwa kama ifuatavyo:
Wahusika
Takadini
-
Ni
mtoto wa kwanza wa Sekai
-
Ni
mlemavu wa ngozi na mguu
-
Ni
mhanga wa mila na desturi zinazowabagua walemavu
-
Anapata
mtoto asiyemlemavu
Sekai
-
Ni
mke wa kwanza wa mzee Makwati
-
Ni
mama yake Takadini
-
Ni
mwanamapinduzi
-
Ni
mfano wa kuigwa na jamii
Makwati
-
Ni
baba yake Takadini
-
Ni
mwoga
-
Ni
mkale
Chivero
-
Ni
mganga wa kienyeji
-
Ni
mshauri mkuu wa mtemi Masasa
-
Aliwapokea
Sekai na Takadini
Mtemi masasa
-
Ana
hekima
-
Ana
wake wengi
-
Ni
shujaa
Shingai
-
Ni
mke wa Takadini
-
Ana
msimamo
-
Ni
mwanamapinduzi
Wahusika wengine ni: Darai,
Rambidzai, Manyamombe, Mukaru, Chumbiri na Makaure.
Matumizi ya Lugha
Nahau
Ni maneno ambayo hubeba maana
tofauti na neno lenyewe lilivyo.
“Lakini mbwa huyu amepoteza meno
yake yote.” (uk 31).
MISEMO
“Maisha ni matamu.” (uk 83).
Tamathali za Semi
-
Tashibiha
“Giza jepesi liibaki ukutani kama
mgeni asiyekaribishwa.” (uk 5).
“Mtoto alionekana mweupe sawa na
funza mkubwa.” (uk 16).
-
Tashihisi
“Ndege mbalimbali wakiimba
kuikaribisha siku mpya.” (uk 5).
“Ubongo wake ulioathirika kwa
mawazo uliufukuza usingizi.” (uk 17).
-
Ritifaa
“Mababu zangu wamenitimizia ombi
langu kuu…” (uk 1).
-
Tafsida
“Akamshambulia hata sehemu zake
za siri.” (uk 83).
“Walifanya tena tendo la ndoa.”
(uk 117).
-
Takriri
“Wewe ni sope, sope, sope.” (uk
62).
-
Mdokezo
“Sukuma mara moja tena…” (uk
125).
-
Nidaa.
Kauli hii huonyesha kushangazwa kwa jambo.
“Kumbe maisha ni matamu!” (uk
83).
Muundo
Riwaya hii imetumia muundo wa
moja kwa moja. Tunamuona Sekai akijifungua mtoto sope, anatoroka na mwanaye ili
kumuokoa dhidi ya watu wa jamii yake. Sekai anakwenda kuishi uhamishoni, akiwa
huko, mwanaye Takadini anapata mke na mtoto.
Mtindo
Mwandishi ametumia:
-
Masimulizi
na dayolojia
-
Matumizi
ya nyimbo. Rumbidzai aliimba;
…Mheshimiwa wetu amemiliki mavuno,
Kwa mikono yake halisi,
Kutokana na mashamba yetu wote,
Lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi hii isiyomea
kitu?
Mandhari
Riwaya hii imetuma mandari ya
kijijini katika maeneo kama, barabarani, shambani, porini, chumbani, nyumbani
n.k
Jina la Kitabu
Jina la kitabu linasadifu
yaliyomo kwani walemavu wanauawa ilhari hawakupenda kuzaliwa hivyo na wala sio
kosa lao bali ni mapenzi ya Mungu. Takadini yaani sisi tumekosa nini?
Linaonyesha jinsi walemavu wanavyouawa pasipokuwa na hatia yoyote ile.
Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
Kufaulu kwa Mwandishi katika Maudhui
-
Ameonyesha
matatizo yanayowapata watu wenye ulemavu
-
Ameonyesha
sababu ya watu wenye ulemavu kutokukubalika ni mila na desturi.
-
Ametoa
suluhisho la matatizo hayo kuwa ni kuachana na mila hizo.
Kufaulu Kifani
-
Ametumia
lugha inayoeleweka na ina tamathali nyingi za semi.
-
Ametumia
nafsi zote tatu.
-
Ameteua
jina zuri la kitabu ambalo linasadifu yaliyomo.
Kutofaulu Kimaudhui
-
Hajaonyesha
jinsi matatizo ya mila na desturi yanavyoweza kuwaathiri walemavu wengine.
Kutofaulu Kifani
-
Ametumia
idadi kubwa ya wahusika ambao hawabebi dhamira zozote.
-
Hajaonyesha
watu wa jamii ya Takadini walilipokeaje suala la kijana huyo kupata mtoto asiye na ulemavu.