Uhakiki wa Riwaya ya Vuta N’kuvute
MWANDISHI: SHAFI ADAM SHAFI
WACHAPISHAJI: MKUKI NA NYOTA
MWAKA: 1999
MHAKIKI: MWALIMU MAKOBA
Utangulizi
Vuta n’kuvute ni riwaya
inayozungumzia mvutano uliopo baina ya wakoloni na watawaliwa vilevile
inaonyesha msuguano na mvutano uliopo kati ya wazazi na watoto katika suala la
mapenzi.
Maudhui
DHAMIRA
UKOMBOZI
Mwandishi anaonyesha aina
mbalimbali za ukombozi unaohitajika katika jamii. Mfano: ukombozi wa
kiutamaduni. Hapa anapinga mila zinazomkandamiza mwanamke. Kwa mfano, Yasmini
kulazimishwa kuolewa na Raza, ni unyanyasaji usiokubalika.
Pia, ukombozi wa kisiasa.
Mwandishi anaonyesha jinsi ambavyo Zanzibar ilitawaliwa na Waingereza. Wahusika
Denge na wenzake wanapambana vilivyo kuhakikisha uhuru wa Zanzibar unapatikana.
Ukiachilia mbali aina hizo mbili
za ukombozi, mwandishi pia amejadili ukombozi wa kiuchumi na fikra.
Mapenzi
Mwandishi anajadili mapenzi ya
kweli na yale ya uongo. Katika mapenzi ya kweli, Mwajuma, Denge na kundi lake
wanamapenzi ya kweli kwa jinsi walivyopendana wao kwama marafiki na jinsi
walivyoipenda nchi yao.
Matabaka
Matabaka matatu yanaonekana:
-
Wazungu.
Hawa waliheshimiwa kuliko matabaka yote. Wazungu wanawakilishwa na wahusika
kama, Inspekta Wright.
-
Wahindi.
Hawa walifuata baada ya tabaka la wazungu. Wahindi wanawakilishwa na wahusika
kama, Raza, Gulamu na wengine wengi.
-
Waafrika.
Hawa hawakuheshimiwa, walibaguliwa na kunyanyaswa. Waafrika wanawakilishwa na
wahusika kama Denge, Mwajuma, Koplo Matata, Mambo, Sukutua n.k
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Mwanamke amechorwa katika nafasi
mbalimbali:
-
Kiumbe
duni asiye na maamuzi yoyote. Yasmini analazimishwa kuolewa na mwanamume
asiyempenda kwa sababu tu alionekana duni na siyeweza kutoa maamuzi.
-
Mwenye
upendo wa kweli. Mwajuma alimpenda Yasmini hata akakubali waishi wote bila
kujali fikra za utabaka na ubaguzi wa rangi uliotawala.
-
Mwanamapinduzi
asiyependa mila zilizopitwa na wakati. Yasmini anaamua kuondoka kwa mumewe,
mwanamume ambaye alimuoa pasi na ridhaa yake. Msichana huyu anaamua kutafuta
uhuru wake mwenyewe.
-
Chombo
cha starehe. Yasmini anatumika kumstarehesha Denge. Naye Mwajuma anatumika
kumstarehesha Mambo.
Ujumbe
i.
Suala
la mapenzi lisiingiliwe na wazazi. Ni vyema maamuzi ya yupi wa kuoa/kumuoa
wakaachiwa wale tu wanaopendana. Yasmini anashindwa kuishi na Bwana Raza kwa
sababu hakumpenda.
ii.
Ukombozi
wa Afrika unahitajika kwa gharama yoyote ile. Waafrika wote waungane ili kuweza
kupambana na ukoloni mamboleo na aina nyingine za ukoloni ambazo zinarudisha
nyuma maendeleo ya bara hili.
iii.
Ukoloni
si jambo jema. Mateso wanayopata akina Denge na wananchi wengine yanauchora
waziwazi uovu na ubaya wa ukoloni.
iv.
Elimu
inahitajika katika jamii. Ni wakati sasa jamii inapaswa ipatiwe elimu ili iweze
kupambana na kuwa huru katika matatizo mbalimbali.
Migogoro
Migogoro ya wahusika
-
Yasmini
na Raza
-
Yasmini
na wazazi wake
-
Yasmini
na Bukhet
-
Denge
na Koplo Matata
-
Denge
na Koplo Matata
-
Denge
na Inspekta Wright
Migogoro ya nafsi
-
Yasmini.
Anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapoolewa na mtu asiyempenda. Suluhisho la
mgogoro huu ni Yasmini kumkimbia mumewe.
-
Bukheti.
Anampenda sana Yasmini, anapata mgogoro wa nafsi endapo kama Yasmini ataweza
kumwelewa nakumkubalia ombo lake. Suluhisho la mgogoro huu ni Bukheti kuamua
kusafiri mpaka Zanzibar. Hatimaye anafanikiwa kumuona Yasmini.
Migogoro ya kiuchumi
Wananchi wakiwakilishwa na Denge,
wanataka uchumi wao urejeshwe katika mikono yao wenyewe. Wanachukia uchumi wa
nchi yao kushikiliwa na wakoloni.
Migogoro ya kisiasa
Wananchi wa Zanzibar wanataka
utawala wao wenyewe. Wamechoka kutawaliwa na wakoloni. Mgogoro huu haupati
suluhisho mpaka mwisho.
Mgogoro wa kiutamaduni
Vijana wako kinyume na tamaduni
walizozikuta. Tunamuona Yasmini akikataa kuishi na mumewe Raza ambaye
hakumpenda.
Msimamo
Msanii ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anaamini kuwa, suala la
ukoloni na tamaduni zinazomkandamiza mwanamke linaweza kuondolewa kwa kuungana
pamoja na kupambana.
Falsafa
Mwandisi anaamini kuwa, ukoloni
utaondolewa kwa kuungana pamoja na kupambana.
Fani
Muundo
Mwandishi katumia muundo wa moja
kwa moja. Anasimulia maisha ya Yasmini na Denge moja kwa moja.
Anaanza masimulizi kwa
kumuonyesha Yasmini katika ndoa, Yasmini anatoroka, kisha anakutana na Denge.
Pia, anaonyesha harakati za Denge kupigania ukombozi, anavyofungwa jela na
anapotoka.
Mtindo
Mwandishi ameiwasilisha kazi yake
kwa kutumia mtindo wa:
-
Monolojia.
Hii ni lugha ya masimulizi katika kazi ya fasihi.
-
Dayolojia.
Hii ni lugha ya majibishano.
-
Barua.
Yasmini alimuandikia barua mpenzi wake Denge.
-
Nyimbo.
Kikundi cha taarabu kilichoitwa cheusi dawa kilitumbuiza nyimbo mbalimbali.
Yasmini na Mwajuma nao waliimba taarabu palipotokea shughuli.
Matumizi ya lugha
Matumizi ya lugha hujikita katika
vipengele vitatu:
-
Tamathali
za semi
-
Misemo,
methali na nahau
-
Picha
na taswira
Tamathali za semi
Tashibiha.
“Bwana Raza amekaa juu ya kiti
amevimba kama kiboko.”
“Mweupe kama mgonjwa wa safura.”
Tashihisi
“Nuru ya jua iliingia wa hamaki
chumbani mule na ilikashifu uchafu wote wa chumba kile.”
Takriri
“Yeye hakuona isipokuwa Yasmini,
Yasmini, Yasmini gani naye?”
“Haya tunywe, tunywe kwa afya ya
mgeni wetu.”
Mjalizo
“Kula mkate wa ufuta, mkate wa
maji, mkate wa mayai.”
Tanakali sauti
“Ngo! Ngo! Ngo!”
Misemo, Methali na Nahau
“Hujui kama mkono wa serikali ni
mrefu.”
“Kumpaka mafuta kwa mgongo wa
chupa.”
“Heri nusu shari kuliko shari
kamili.”
Picha na taswira
“Yasmini alikuwa na kijiuso
kidogo, macho makubwa, pua ndogo na nyembamba, alikuwa na nywele nyingi.”
Matumizi ya lugha ya picha
Komunisti – hili ni jina ambalo
waliitwa waafrika waliojitolea kupigania uhuru kama Denge.
Wahusika
YASMINI
-
Mwanamke
asiyependa tamaduni kandamizi. Anamtoroka mumewe na kwenda kuolewa na mwanamume
anayempenda.
-
Mvumilivu.
Anayavumilia maisha magumu anayokutana nayo kwa Mwajuma.
-
Ana
upendo wa kweli. Anampenda kwa dhati mpenzi wake Denge.
DENGE
-
Mwanaharakati
na anayepinga utawala wa mwingereza kisiwani Zanzibar.
-
Kijana
aliyesoma Urusi na anaitumia vyema elimu yake.
-
Anampenda
Yasmini na wanafanikiwa kupata mtoto mmoja.
MWAJUMA
-
Rafiki
yake Yasmini
-
Ana
upendo wa kweli
-
Mwanachama
wa kikundi cha ‘cheusi dawa.’
-
Anapenda
pesa
Wahusika wengine ni: Koplo
Matata, Chande, Sukutua, Raza, Salehe, Wright, Shihab na Bukhet.
Mandhari
Mandhari yaliyotumika
yamegawanyika katika miji hii:
-
Unguja
-
Tanga
-
Mombasa
-
Dar
es Salaam
Vilevile kuna mandhari ya:
-
Dukani
-
Gerezani
-
Baharini
-
Nyumbani
-
Mitaani
-
Baa
-
Klabu
Kufaulu kwa mwandishi
-
Amefanikiwa
kuonyesha mvutano wa wazazi na watoto wao.
-
Ametumia
lugha nzuri iliyopambwa kwa tamathali nyingi za semi.
Kutofaulu kwa mwandishi
-
Suluhisho
la mgogoro wa wakoloni na watawaliwa halijatolewa na mwandishi.
-
Mwandishi
hajaonyesha mipaka ya uhuru inayotakiwa na watoto. Mfano: Yasmini anaolewa na
mwanamume anayempenda, Shihab. Lakini ndoa yao inashindwa kudumu.