Uhakiki wa Tamthiliya ya Nguzo Mama

UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA NGUZO MAMA
KITABU – NGUZO MAMA
MWANDISHI – PENINA MHANDO
WACHAPISHAJI – DUP
MWAKA – 1982
MHAKIKI: MWALIMU MAKOBA

Tamthiliya ya Nguzo Mama inayazungumzia matatizo anayokutana nayo mwanamke na harakati anazofanya ili kujinasua. Wakati mitazamo mingine ikisema kuwa matatizo ya mwanamke yanasababishwa na jamii yake na mila potofu Penina mhando anakuja na dhana mpya, “matatizo ya mwanamke yanasababishwa na mwanamke mwenyewe.”

Maudhui

1.   Dhamira

i.             Ukombozi wa mwanamke

Mwandishi anaonesha manyanyaso makali anayopewa mwanamke. Bi Pili anapigwa kila siku na mumewe, anafanya kazi lakini mumewe anachukua pesa yote inayopatikana. Suluhisho la matatizo haya na mengine yanayojitokeza ni kusimama kwa Nguzo Mama.

ii.            Uongozi mbaya

Mwenyekiti anaongoza kwa mabavu. Anapelekewa kesi na Bi nne. Bi Nne anamtuhumu Bi Nane. Mwenyekiti kwa kutumia mabavu anatoa maamuzi pasipo kumsikiliza Bi Nane. Udikteta kama huu, unachelewesha maendeleo ya mwanamke.

iii.           Elimu

Ni vyema elimu itolewe kwa watu wote. Kukosekana kwa elimu ni sababu mojawapo inayochelewesha maendeleo Patata. Mfano Bi Saba ambaye ni kiongozi wa kamati ya wanawake, hajui maana ya nguzo mama.

iv.          Umasikini

Suala la umasikini ni tatizo sugu ambalo bado halijapatiwa dawa. Bi Tano anaishi maisha magumu, hana pesa ya kuwanunulia nguo watoto wake, hana pesa ya kununulia chakula. Wanawake wanafanya harakati nyingi ili kuondokana na umasikini lakini bado tatizo hili linaendelea.

v.           Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwanamke amechorwa kama,
-         Chombo cha starehe
Bi Sita anafanya biashara ya kuuza mwili, wanaume wanamnunua na kumtumia kwa kujistarehesha.
-         Mwenye busara
Bi Nane ana busara, yeye anawashauri wanawake wenzake wajishughulishe na miradi tofauti tofauti ili waweze kujikomboa kiuchumi.
-         Kiumbe dhaifu na asiye weza kutoa maamuzi yoyote
Sudi anampiga mkewe Bi Pili. Anapomaliza kumpiga, anachukua hela zake zote na kwenda kunywa pombe.

-         Mama mlezi wa familia
Mwanamke amechorwa kama anayejishughulisha na mambo yote yahusuyo familia yake, yeye ndiye anayejua watoto wamekula nini na kama wako salama.

2.   Ujumbe

i.             Fimbo ya mnyonge ni umoja

Wanawake wanatakiwa kuungana ili kupambana na matatizo yanayowakabili, makundi na majungu hayana msaada.

ii.            Ili jamii iendelee lazima kuwe na misingi ya uongozi bora

Mwenyekiti na Bi Nne wanakwamisha maendeleo ya wanawake kwa sababu hawakuwa na misingi ya uongozi bora, ili jamii ijikwamue ni lazima suala hili liwekewe mkazo

iii.           Sheria kali ziwekwe dhidi ya watu wanaowanyanyasa wanawake

Sudi anampiga mkewe, suala hili likemewe.

iv.          Ulevi ni chanzo cha umasikini

Wanaume wengi katika jamii ya Patata ni walevi wa kutupwa! Hii inafanya wanaume hawa washindwe kuhudumia familia zao, mfano Sudi anamtegemea mke wake ili aweze kuishi.

3.   Migogoro

i.             Migogoro ya wahusika

-         Bi Pili na Bwana Sudi
-         Bwana Sudi na Totoro
-         Bi Nne na Bi Nane
-         Bi Nane na Mwenyekiti

ii.            Mgogoro wa nafsi

Bi Nane anapatwa na mgogoro pale anapopelekwa kwa mwenyekiti wa kijiji kujibu tuhuma zinazomkabili. Anawaza iwapoa aendelee kushirikiana na wanawake wenzake au atengeneze maisha yake mwenyewe.

iii.           Migogoro ya kiuchumi

Migogoro hii inasababishwa na uvivu pamoja na ukosefu wa elimu. Inaoneshwa katika kitabu, wanaume wavivu wakiwapiga wake zao ili wawape fedha.

iv.          Migogoro ya kifalsafa

Uongozi mbaya umeonekana, kwanza viongozi wanachangia kuibuka kwa migogoro kwa sababu hawana elimu ya kutosha. Mfano mwenyekiti anatoa hukumu bila kusikiliza upande wa pili wa mtuhumiwa.

4.   Msimamo

Msanii anamsimamo wa kimapinduzi kwani anashauri kuwa matatizo yote yanayowakabili wanawake yataondoka endapo watakuwa na umoja na mshikamano.

5.   Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa chanzo cha matatizo ya mwanamke ni mwanamke mwenyewe.

Fani

1.   Muundo

Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Tamthiliya inaanza kwa kuonesha nguzo mama ikiwa imelala, wanawake wanafanya harakati za kuiinua lakini wanashindawa.

2.   Mtindo

Msanii ametumia mtindo wa,
-         Dayolojia
-         Masimulizi
-         Nyimbo
-         Mtindo wa kishairi

3.   Matumizi ya lugha
i.             Tamathali za semi
-         Tashibiha
“anatembea kama kapigwa bumbuwazi.”
-         Tashihisi
“hasira zikampanda bi nane.”
-         Sitiari
“mbwa mume wako anayefuata wanawake ovyo.”
-         Takriri
“wakajaribu, wakajaribu.”

ii.            Methali, misemo na nahau
-         La mgambo likilia lina jambo
-         Utakiona cha mtema kuni
-         Utakufa kibudu

iii.           Picha na taswira
-         Nguzo mama
Hii ni lugha ya picha ambapo neno nguzo mama linaashiria ukombozi wa mwanamke, nguzo mama ni mambo yote mazuri ambayo anayahitaji mwanamke ili akombolewe, mwanamke anajitahidi kupambana kuiinua nguzo mama lakini anashindwa.

4.   Wahusika

i.             Bi Moja
-         Mke wa Shabani
-         Hana msimamo katika kuisiamisha nguzo mama
ii.            Bi Pili
-         Mke wa Sudi
-         Ananyanyaswa na mume wake
iii.           Bi Tatu
-         Anabembeleza mume wake kwa kuogopa kuachwa
-         Ni mpenda starehe
iv.          Bi Nne
-         Hapendi maendeleo ya watu wengine
v.           Bi Tano
-         Anahasira sana
-         Ni mke wa Maganga
vi.          Bi Sita
-         Anatembea na waume za watu
vii.         Bi Saba
-         Shemeji zake walimnyang’anya mali mara baada ya kufiwa na mumewe
viii.       Bi Nane
-         Alipenda kuelimisha wenzake katika shughuli za maendeleo
ix.          Chizi
-         Ni mfichua maovu yaliyoko katika jamii
x.            Mwenyekiti
-         Ni kiongozi mbaya tena asiye na elimu

Mandhari

Msanii anatumia madhari ya kubuni ya mji wa Patata. Tamthiliya hii imetendeka katika mandhari ya,
-         Vilabuni
-         Uwanjani
-         Mtaani

Kufaulu kwa mwandishi

Amefaulu kuonesha matatizo yanayowapata wanawake. Matatizo hayo ni kama, manyanyaso, umasikini, ukosefu wa elimu na uongozi mbaya.
Pia mwandishi ametumia lugha rahisi inayoeleweka kwa awasomaji wengi

Kutofaulu kwa mwandishi

Hitimisho la kushindwa kuiinua nguzo mama kwa wanawake linakatisha tamaa na kupeleka ujumbe kuwa, matatizo ya wanawake hayawezi kuondoka.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024