Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Mtu anaandika barua ya maombi ya kazi

Kitaalamu Zaidi, Tunaweza Kukuandikia Barua ya Maombi ya Kazi na CV Uitwe Katika Usaili na Upate Kazi. Barua Tsh. 5,000/= na CV Tsh. 9,000/=. Gusa Hapa Kuwasiliana Nasi.
Umewekeza katika elimu yako, una kila sifa ya kupata kazi fulani lakini hupati kazi hiyo, inawezekana kabisa sababu mojawapo inayokufanya usipate kazi unayoitaka ni kutokujua kuandika barua ya maombi ya kazi au unapoandika, unaandika katika namna mbaya inayofanya waajiri wakupuuze.
Kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizwa na wanafunzi na wasomaji wa mtandao wangu kuhusu jinsi ya kuandika barua ya maombi ya kazi kwa kiswahili, na wengine huuliza kuhusu jinsi ya kuandika barua ya maombi ya kazi kwa kiingereza. Waombaji wengi huuliza kuhusu maombi ya kazi ya udereva, hotelini, kazi za polisi, ualimu, afya utendaji wa kijiji na kazi chungu nzima ambazo haziwezi kutosha hapa zikiandikwa. Kazi zote siku hizi zinahitaji kuandika barua, hata kama unataka kujitolea, lazima utaandika barua!
Isivyo bahati ni kuwa, hata mtandaoni mifano inayooneshwa kuwa ni ya barua za maombi ya kazi mingi yake siyo sahihi, kila mmoja ana njia zake. Ni kama mashetani kila mmoja na mbuyu wake.
Hata hivyo, wapo wataalamu wengine ambao wanafafanua vizuri namna ya kuandika barua ya maombi ya kazi, kwa mfano, mtaalamu Alison Doyle, anafundisha vizuri namna ya kuandika barua ya maombi ya kazi tena akitoa mifano. Isivyo bahati, mtaalamu huyu anaandika kwa kiingereza na muundo anaotumia unawahusu zaidi watu wa Marekani na kufanya japo anaandika vitu sahihi, haviendani na mazingira yetu.
Barua ya maombi ya kazi huandikwa kwa malengo ya kuomba kazi. Kujifunza namna sahihi ya uandishi wa barua ya maombi ya kazi si kwamba utakusaidia katika kujibu maswali pekee, bali ujuzi huu utakufanya upate kazi halisi wakati utakapo hitaji kufanya hivyo.
Nakumbuka niliwahi kuitwa kufanya kazi katika kampuni ya global publishers kwa sababu tu, niliandika vyema barua yangu ya maombi ya kazi. Sasa nitakuelekeza yale unayotakiwa kuyafanya unapoandika barua ya maombi ya kazi. Jifunze taratibu ili baadaye uweze kuandika barua unayotaka na uweze kupata kazi.
Muundo wa Barua ya Maombi ya Kazi
i. Anuani ya mwandishi. Yaani anuani yako wewe unayeandika barua hiyo.
ii. Tarehe.
iii. Anuani ya anayeandikiwa.
iv. Salamu.
v. Kichwa cha habari.
vi. Kiini cha barua. Hii ni roho ya barua yako, ukikosea mahali hapa, kama unajibu swali katika mtihani, utapoteza alama. Na kama unaomba kazi halisi, utaikosa. Kiini kina aya nne:
Katika aya ya kwanza, eleza kazi unayoomba na mahali ulipoona tangazo la kazi hiyo. Ni katika sehemu hii unaweza kutaja umri wako.
Katika aya ya pili, eleza ujuzi wako kwa ufupi. Usieleze sana. Barua hii haipaswi kuwa ndefu kupindukia.
Aya ya tatu eleza kwa nini upewe kazi hii wewe na si mtu mwingine. Epuka kueleza shida zako binafsi ili upewe kazi. Maneno kama, ninaomba kazi hii ili niweze kumtibia mama yangu mgonjwa kitandani, hayana msaada.
Aya ya nne eleza uko tayari kwa usahili siku gani?
vii. Mwisho wa barua. Mwisho wa barua yako uwe na:
Neno la kufungia. Wako mtiifu. Wako katika ujenzi wa taifa n.k
Sahihi yako.
Jina lako
Wengine hujifunza kuandika barua ya maombi ya kazi ili waweze kujibu maswali katika mtihani, na wengine hujifunza ili waweze kuandika barua hizo, waweze kuomba kazi halisi. Vyovyote vile, mfano huu halisi wa barua, ni sahihi kwa watu wote, wanafunzi na wale wanaotafuta kazi.

Mfano huu wa barua ni wa barua ya maombi ya kazi ya fundi umeme. Hata hivyo, muundo huu unaweza kutumika katika kuomba kazi yoyote.

Pia, barua ya maombi ya kazi, huambatana na CV, hivyo utakapomaliza kujifunza jinsi ya kuandika barua ya maombi ya kazi, tafadhali jifunze hapa jinsi ya kuandika CV.

Mfano wa Kwanza: Barua ya Maombi ya Kazi ya Fundi Umeme-Kiswahili

Simu: 0653 250 566,

Barua Pepe: milambo@gmail.com,

DAR ES SALAAM.

04/07/2022.

Mkurugenzi Mkuu,

Shirika la Reli Tanzania,

S.L.P 76956,

DAR ES SALAAM.

 

Ndugu,

 

Yah: OMBI LA KAZI YA FUNDI UMEME

Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 30. Ninaomba Kazi ya Fundi Umeme kama ilivyotangazwa na Shirika la Reli Tanzania siku ya tarehe 28/06/2022 katika Tovuti, mitandao ya Kijamii na mbao za matangazo.

Nina Cheti cha Fundi Umeme nilichotunukiwa kutoka VETA mwaka 2021. Pia, nina uzoefu wa kufanya kazi na nimefanya kazi na Taasisi Ya 21st Century Holding LTD.

Kutokana na elimu yangu, uwezo wa kufanya kazi nilionao, uzoefu, pamoja na kuwa na sifa zinazotakiwa, ninaamini kuwa ninastahili kupata kazi hii. Endapo nitapata kazi hii ya Fundi Umeme, nitafanya kazi kwa bidii kama ilivyoelekezwa. Baadhi ya majukumu yangu ni: kutengeneza mifumo ya umeme, kuhakikisha vifaa vya umeme vinafanya kazi na kufuata maelekezo nitakayopangiwa.

Nipo tayari kwa usaili siku yoyote nitakayohitajika. Vilevile, ninatarajia majibu mazuri kutoka kwako na nimeambatanisha nakala ya vyeti vyangu kwa uthibitisho zaidi.

Wako mtiifu,

____________

ISIKE MILAMBO

Mfano wa Pili: Barua ya Maombi ya Kazi Yenye Kumbukumbu namba ya Katibu Mahsusi

Kuna matangazo hususani yale yanayotolewa na Serikali, humtaka mwombaji ataje kumbukumbu namba aliyoiona kwenye tangazo. Endapo hutaweka kumbukumbu namba kwenye barua ambayo umeelekezwa uweke, maombi yako yatapuuzwa. Tazama mfano na mahali Kumbukumbu namba inawekwa:

Mfano huu ni wa mwombaji wa kazi ya Katibu Mahsusi Daraja la III

Simu: 0653 250 566,

Barua Pepe: lumumba@gmail.com,

NJOMBE.

07/07/2022.

Mkurugenzi wa Mji,

Halmashauri ya Mji,

S.L.P 405,

MAKAMBAKO.

Kumb, Na:MTC/E.80/VOL I/47

Ndugu,

 

Yah: OMBI LA KAZI YA KATIBU MAHUSUSI DARAJA LA III

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30. Ninaomba Kazi ya Katibu Mahususi Daraja la III kama ilivyotangazwa na Halmashauri ya Mji Makambako siku ya tarehe 27/06/2022 katika Tovuti, mitandao ya Kijamii na mbao za matangazo.

Nina Cheti cha Katibu Mahsusi nilichotunukiwa kutoka Mafinga Secretarial VETA, Iringa. Pia nina uzoefu wa kufanya kazi na nimefanya kazi na Jimbo katoliki la Njombe. Pia, nimefaulu somo la hati mkato ya Kiswahili na Kiingereza maneno 100 kwa dakika moja. Vilevile, nina uzoefu wa kazi na nimefanya kazi na Halmashauri ya Mji Kigoma Ujiji.

Kutokana na elimu yangu, uwezo wa kufanya kazi nilionao, uzoefu, pamoja na kuwa na sifa zinazotakiwa, ninaamini kuwa ninastahili kupata kazi hii. Endapo nitapata kazi hii ya Katibu Mahsusi Daraja la III, nitafanya kazi kwa bidii na kutimiza majukumu yangu yote. Baadhi ya majukumu yangu ni: kuchapa barua na nyaraka za kawaida, kusaidia kupokea wageni na kusaidia kufikisha maelekezo ya mkuu wa kazi.

Nipo tayari kwa usaili siku yoyote nitakayohitajika. Vilevile, ninatarajia majibu mazuri kutoka kwako na nimeambatanisha nakala ya vyeti vyangu kwa uthibitisho zaidi.

Wako mtiifu,

____________

WEMA LUMUMBA

Mfano wa Tatu: Barua ya Maombi ya Kazi ya Tutorial Examination Officer II-Kiingereza

Endapo tangazo la kazi limeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hata wewe andika barua yako kwa lugha hiyo. Huu ni mfano wa barua ya maombi ya Kazi iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Mfano wa Barua ya Maombi ya Kazi kwa Kiingereza

Mfano wa Nne: Barua ya Maombi ya Kazi ya Udereva-Kiswahili

Simu: 0653 250 566,

Barua Pepe: daudmakoba@rocketmail.com,

DAR ES SALAAM. 
14/06/2024.

Ofisi ya Rais,
Utumishi,

S. L.P 2320,

DODOMA.

 

Ndugu,

 

Yah: OMBI LA KAZI YA UDEREVA

Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 31. Ninaomba Kazi ya Udereva kama ilivyotangazwa katika mbao za matangazo na mitandao mbalimbali ya kijamii siku ya tarehe 13/06/2024.

Nina elimu ya kidato cha Nne na nimesoma katika shule ya Sekondari Igunga na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2012. Nina uzoefu wa kazi hii na nimefanya kazi na ‘Sumbawanga Limited’ kwa muda wa miaka saba. Uzoefu wangu wa kazi ya udereva, umenifanya niwe bora katika kazi hii na niweze kutimiza majukumu yangu yote kama vile kuhakikisha gari ipo salama, kuendesha kwa kuzingatia kanuni zote za barabarani na majukumu mengineyo. Ni matumaini yangu kwamba, sifa zangu hizi, zinanifanya nistahili kupata kazi hii.

Nipo tayari kwa usaili siku yoyote nitakayohitajika. Vilevile, ninatarajia majibu mazuri kutoka kwako na nimeambatanisha nakala ya vyeti vyangu kwa uthibitisho zaidi. 

Wako mtiifu,

_________

NJIKA MASUKE LONUNGU

Mfano wa Tano: Ombi la Kazi ya Daktari Daraja la II

Simu: 0653 250 566,

Barua Pepe: daudmakoba@rocketmail.com ,

DAR ES SALAAM.
15/06/2024.

Mganga Mfawidhi,

Hospital ya Mkoa Katavi,

S.L.P 449,

MPANDA.

 

Ndugu,

 

Yah: OMBI LA KAZI YA DAKTARI DARAJA LA II

Mimi ni mwanamume Mtanzania mwenye umri wa miaka 38. Ninaomba Kazi ya Daktari Daraja la II kama ilivyotangazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Nina Shahada ya Udaktari niliyotunukiwa na chuo kiitwacho European School of Medicine. Pia, nina uzoefu wa kazi na nimefanya kazi na hospitali zifuatazo: Champion Hospital, Hospitali ya Rufaa Iringa, na Heal Now Superspecialized Polyclinic.

Kutokana na uzoefu wangu, elimu, uwezo wa kufanya kazi nilionao pamoja na kuwa na sifa zinazotakiwa, ninaamini kuwa ninastahili kupata kazi hii. Endapo nitapata kazi ninayoomba, nitafanya kazi kwa bidii na kutimiza majukumu yangu yote ikiwemo kutoa uchunguzi na matibabu.

Nipo tayari kwa usaili siku yoyote nitakayohitajika. Vilevile, ninatarajia majibu mazuri kutoka kwako na nimeambatanisha nakala ya vyeti vyangu kwa uthibitisho zaidi. 

Wako mtiifu,

_________

MAHONA KIJA


Sasa nadhani umeona jinsi barua ya maombi ya kazi inavyoandikwa. Unaweza kuandika barua yako kwa mfumo huo niliotoa, hata kama ni kwa kiingereza, muundo unabaki kama huo hapo juu, tofauti ni lugha tu.

Kama umeona mifano ya barua hizo, lakini hutaki kuandika barua wewe mwenyewe, pengine hutaki kufanya kosa hata moja litakalosababisha ukaikosa kazi uitakayo, au labda inatakiwa barua ya kiingereza na wewe hutaki kuhangaika kuanza kutafuta maneno ya kiingereza, naweza kukuandikia barua. Bei ni ndogo na haifanani na bei zingine, barua peke yake ni sh. 5,000/= (elfu tano tu), na cv peke yake ni sh. 9,000/=  (elfu tisa tu).

Kitaalamu Zaidi, Tunaweza Kukuandikia Barua ya Maombi ya Kazi na CV Uitwe Katika Usaili na Upate Kazi. Barua Tsh. 5,000/= na CV Tsh. 9,000/=. Gusa Hapa Kuwasiliana Nasi.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute