Jinsi ya Kuandika Hotuba

Jinsi ya Kuandika Hotuba
Hotuba ni maelezo ambayo hutolewa na mtu mbele ya watu kuhusu mada fulani.

MUUNDO WA HOTUBA

-      Mwanzo. Huu huambatana na salamu.
-      Utangulizi. Hutaja watu na kuwatambulisha kulingana na vyeo vyao.
-      Kati. Hiki ni kiini cha hotuba. Mawazo yote makuu hukaa hapa.
-      Mwisho. Muhtasari wa yale yaliyoelezwa. Pia, msemaji hupata nafasi ya kuaga na kushukuru.
Sasa tazama mfano halisi wa hotuba ambao umeandikwa kama majibu ya swali la nane mtihani wa kumaliza kidato cha nne 2010.
Eleza tofauti iliyopo kati ya hotuba na risala. Andika hotuba kuhusu “Maji ni Uhai.”
Kwa kuwa mjadala wetu ni hotuba, risala haitazungumziwa, bali nitajikita katika kuonyesha mfano wa hotuba.
MAJI NI UHAI
Wanakijiji oyeeeeeeh!
Ndugu Mwenyekiti wa Kijiji, ndugu Katibu wa Kijiji, Ndugu Wanakijiji wote mabibi na mabwana. Ninafurahi kusimama mbele yenu na kuzungumza. Nikiwa kama mwanaharakati wa muda mrefu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, leo nasimama tena kuwaeleza na kuuthibitishia umma huu kuwa maji ni uhai.
Asilimia sabini ya miili yetu ni maji. Hivyo bila maji mwanadamu hawezi kuishi lau kwa mwaka mmoja. Sisi ni maji, lazima tuishi kwa tahadhari kubwa kuyanusuru maji haya yasipotee tukaadhirika.
Laiti kama tungepata nafasi ya kutembelea watu waishio jangwani, tukawaona jinsi wanavyopata shida ya maji, tungejifunza kitu. Kuna visa kadhaa vimekuwa vikiripotiwa katika vyombo vya habari kuhusu watu na wanyama waliokufa kwa ukosefu wa maji.
Ukiachilia mbali matumizi yetu, hata viumbe wengine kama mamba, samaki, viboko na pweza wanategemea maji hayahaya ili waendelee kuishi. Ndugu zangu lazima sasa tukubaliane kuwa, maji ni uhai.
Ni kipi hakihitaji maji? Hata viwanda hivi tunavyovitegemea kwa uzalishaji wa bidhaa, bila maji ya kupozea mitambo yake haviwezi kufanya kazi. Mwaka jana nikiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kijiji hiki tulikumbwa na kasheshe ya kuharibikiwa na injini ya gari letu, tulipochunguza tukagundua ilichemka kupita kiasi kwa kukosa maji!
Wanyama na mimea tunaowategemea kwa chakula ili tuendelee kuishi, wanategemea maji. Kilimo bila maji hakuna kitu. Bila maji wote tutakwisha na kusahaulika mara moja.
Niwaombe ndugu zangu, tuiache mara moja hii tabia mpya iliyozuka. Tabia ya kunywesha mifugo katika vyanzo vya maji itatuletea balaa. Pia, kuna mkasa mwingine wa watu kukata miti hovyo. Hatukatazi kukata miti, lakini hakikisha unapokata mti uwe na kibali maalumu na pia, kata mti panda mti. Vijana wa siku hizi wamebadili msemo huu, wanasema panda mti ndipo ukate mti! Nawaunga mkono.
Ni matumaini yangu makubwa mtayafanyia kazi yote niliyoyasema. Msingi zaidi, tuhakikishe tunaepuka tabia zote ambazo zitatuharibia vyanzo vyetu vya maji. Mwisho niwashukuru wote kwa kunisikiliza, nasema asanteni sana.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2025

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1