Jinsi ya Kuandika Insha

Jinsi ya Kuandika Insha
Insha ni mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayozungumziwa au kuandikwa. Urefu au ufupi wa insha hutegemea mada husika inayojadiliwa.

Muundo wa Insha

Insha bora inatakiwa iwe na mambo haya:
-      Kichwa cha insha
-      Mwanzo wa insha
-      Kiini cha insha
-      Mwisho wa insha
Zipo aina tatu za insha: insha za wasifu, insha za hoja na insha za kisanaa. Katika kipengele hiki, hatutajadili aina za insha bali tutatazamia namna ya kuandika insha kwa ujumla.
Baada ya kutazama mambo hayo, sasa soma mfano huu wa insha iliyoandikwa.

Swali la nane, mtihani wa necta mwaka 2009.

Andika insha yenye maneno 250 kuhusu moja ya mada zifuatazo:
(a) Aisifuye mvua imemnyeshea.
(b) Elimu ya msingi ina umuhimu wake katika jamii.
(c) Maradhi yanavyorudisha nyuma maendeleo ya familia hatimaye Taifa.
(d) Kuelimika kwa msichana ni kuelimika kwa jamii.
(e) Wanyama pori.

Katika swali hilo, ni vyema kama mwanafunzi atatuliza kichwa na kuchagua swali ambalo ana uhakika ataweza kulijibu vyema ikilinganishwa na maswali mengine.
Kama ningekuwa mimi nafanya mtihani huo, ningechagua swali (b) na kuandika kama inavyooneshwa hapa:
ELIMU YA MSINGI INA UMUHIMU WAKE KATIKA JAMII
Elimu ya msingi ni elimu ambayo hutolewa kwa mtu ili kumwandaa kukabiliana vyema na jamii yake. Mara nyingi elimu ya msingi hutolewa kwa watoto wadogo, hata hivyo si mara zote kwani ipo mikasa ya watu wazima kupatiwa elimu hiyo ambayo waliikosa pindi walipokuwa watoto. Elimu ya msingi ni muhimu katika jamii kama inavyoelezwa:
Elimu ya msingi huwafundisha wanafunzi kusoma, kuandika na kuhesabu. Mwanafunzi anayeyaelewa mambo haya matatu huwa na uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii yake. Mtu asiyejua kusoma huhesabiwa kuwa mjinga.
Pia, elimu ya msingi huwaandaa wanafunzi kuitumikia jamii yao. Yapo mengi yanayofundishwa miongoni mwayo ni kilimo na stadi za kazi ambazo hugeuka msaada mkubwa hata mwanafunzi anapomaliza masomo yake.
Umuhimu mwingine wa elimu ya msingi ni kwamba, hutumika kuandaa wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari. Wanafunzi ambao hufaulu darasa la saba huchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari ili kupata maarifa ya juu zaidi.
Tena, elimu ya msingi huandaa watu watakaojiunga na vyuo mbalimbali vya ufundi kama VETA na vinginevyo. Wanafunzi ambao hushindwa kuendelea na elimu ya sekondari, hujiunga katika vyuo vya ufundi ili kujipatia ujuzi.
Elimu ya msingi hufundisha historia na tamaduni za Kiafrika. Urithishaji huu wa amali za jamii una umuhimu mkubwa hasa katika zama hizi ambazo jamii yetu imevamiwa na wimbi kubwa la ongezeko la tamaduni kutoka Ulaya na Asia.
Kwa kumalizia, elimu ya msingi huandaa wananchi watakaolitumikia taifa lao. Taifa linahitaji watu walio tayari kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha usalama na kusaidia maendeleo ya nchi.
Kwa kuhitimisha, elimu ya msingi ina umuhimu mkubwa katika jamii. Serikali na jamii kwa ujumla, inatakiwa iboreshe mazingira ya utoaji wa elimu hii.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024