Mke wa Mugabe Hakamatiki, Atoa Povu Kali
Kama asivyoishiwa vituko mumewe,
Bi Grace Mugabe naye ni pasua kichwa! Wakati utawala wa Mugabe ukielekea
ukingoni kutokana na umri mkubwa wa mzee huyo mtawala wa Zimbambwe, kumezuka
hali ya kutokuaminiana hii yote ikisababishwa na watu fulani kutaka kukalia
kiti cha urais baada ya Mugabe.
Bi Grace kwa kuyatambua hayo,
amesema kuna uwezekano wa kutokea mapinduzi nchini humo kuhusu harakati za
kumrithi Mugabe.
Grace amemshutumu bwana
Mnangangwa kwa maneno makali kama alivyonukuliwa:
“Tunatishiwa usiku na mchana
kwamba iwapo mtu fulani hatokuwa rais, tutauawa.”
Ugomvi wa madaraka katika nchi za
Kiafrika ni suala lililozoeleka. Kupigana vikumbo, kudondoshana, kuzodoana na
hata kuuana vimekuwa tabia ya wasaka madaraka. Ni wakati sasa Wazimbabwe, wanatakiwa
kuungana pamoja na kutafuta muafaka mapema kabla hayajawakuta yaliyoziangusha
serikali nyingi.