Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne | Oktoba 08 2017
Maelekezo ya mtihani huu
i. Jibu
maswali yote.
ii. Usifanye
udanganyifu katika mtihani huu. Lengo la mtihani siyo kuuona uwezo wako wa
kupata A, bali kutambua kipi kinachokusumbua katika somo hili ili uweze kusaidiwa.
Jinsi ya kufanya mtihani huu wa online na usahihishaji wake
i. Andika
majibu yako katika karatasi yoyote utakayoona inafaa kujibia.
ii. Ukimaliza kufanya mtihani, piga picha majibu yako katika karatasi zote ulizotumia kisha tuma picha hizo kwa njia ya WhatsApp kwenda namba 0754895321 ili ziweze kusahihishwa.
ii. Ukimaliza kufanya mtihani, piga picha majibu yako katika karatasi zote ulizotumia kisha tuma picha hizo kwa njia ya WhatsApp kwenda namba 0754895321 ili ziweze kusahihishwa.
iii. Karatasi
zitakazosahihishwa ni zile zitakazokuwa zimelipiwa kiasi cha
shilingi 1,000
(elfu moja). Namba za malipo ni MPESA 0754 89 53 21 na TIGO PESA 0653 25 05 66.
Hata hivyo kama huna uwezo kabisa wa kulipia gharama hiyo, unashauriwa ufanye
mtihani huu kisha umpatie mwalimu yeyote aliyekaribu nawe asahihishe kazi yako.
Kwa kuwa kiwango cha malipo ni kidogo sana, ni vizuri zaidi kama utasahihishwa
na timu yetu.
iv. Kwa
kuwa lengo la mtihani huu ni kubaini matatizo yanayomsumbua mwanafunzi katika
somo hili ili tuweze kuyaondoa mapema na kumsaidia mwanafunzi husika kufaulu na
kupata maarifa stahiki, suala la muda halijazingatiwa, hivyo unaweza ukafanya
kwa wakati wowote utakavyoona inafaa.
SASA FANYA MTIHANI WAKO: KUMBUKA KUJIBU MASWALI YOTE
SEHEMU A (Alama 10)
UFAHAMU
1.
Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yatakayofuata:
Saa mbili asubuhi Wananchi wote tulikusanyika kwenye
kibaraza cha mfalme kama ilivyoamriwa. Mfalme akiwa amevalia joho jeupe
alisimama akasema,
“Leo
viongozi hatujalala, matatizo yaliyotokea jana yalitufanya tukeshe tukijadili
mwafaka wa Dunia bila mwezi. Kijitu kilichouiba mwezi kinatoka Dunia nyingine
iitwayo Vumu iliyo katika mfumo wa jua lingine. Inasemekana katika sayari yao
hiyo, mwezi wao ulizimika ghafla wakati watoto waliotumwa kwenda kuusafisha
walipozidisha kiasi cha mafuta. Vijitu hivi vinamaarifa mengi sana lakini
havijui kitu katika elimu ya kuukarabati mwezi, hivyo suluhisho lao lilikuwa
kuiba mwezi mwingine. Sasa basi anatakiwa atumwe mtu kwenda katika sayari ya Vumu kuurejesha mwezi wetu. Hatutaki
uhasama wala vita tena katika nchi hii… hivyo atakayekwenda huko aende kutatua
matatizo kwa njia ya Amani.” Mfalme alikohoa kidogo kisha akaendelea kuzungumza
kwa sauti kubwa zaidi,
“Kama
mjuavyo chombo chetu cha masafa ya mbali huwa hakiwezi kupandwa na mtu mzima
ila mtoto mdogo tu kwa sababu ya nguvu ya mvutano ya Dunia, hivyo anatakiwa
apatikane mtoto mdogo asiyezidi miaka 15 na asiyepungua miaka minane…”
Kabla mfalme hajaendelea kuzungumza, nilipaaza sauti
huku nikisogea mahala aliposimama,
“Mimi
Nkenye, nitakwenda Vumu kuusaka mwezi, nina umri wa miaka tisa, nimekuwa
nikifanya kazi ya kuusafisha mwezi pale unapochafuka na kutoa mwanga hafifu,
pia mimi ni mtoto wa shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya anga kwa
kipande cha sindano butu!”
a. Kipi kinafaa kuwa kichwa cha habari uliyosoma?
b. Unadhani hadithi hii ina ukweli wowote? Eleza.
c. Ni ipi sababu ya chombo cha masafa ya mbali kupandwa
na mtoto mdogo?
d. “Shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya
anga kwa kipande cha sindano butu!” Usemi huu una maana gani?
2. Andika ufupisho wa hadithi
hiyo kwa maneno yasiyozidi 60.
SEHEMU B (Alama 25)
SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
3. Taja tofauti mbili kati ya mofimu huru na mofimu
tegemezi.
4. Eleza maana ya vidahizo vifuatavyo kisha tunga
sentensi moja kwa kila kidahizo: Chapuo, Funganyumba, Ghariki, Harabu, Kifuku.
SEHEMU C (Alama 10)
UANDISHI
5. Andika insha yenye maneno 250 kuhusu mada
isemayo: ELIMU YA MSINGI INA UMUHIMU WAKE KATIKA JAMII.
SEHEMU D (Alama 10)
MAENDELEO YA KISWAHILI
6. Huku ukitoa mifano ya kutosha, fafanua mchango wa
Waarabu katika kukuza lugha ya Kiswahili.
SEHEMU E (Alama 45)
FASIHI KWA UJUMLA
7. Jadili jinsi washairi walivyoishauri jamii yao.
8. Mandhari ni kitu pekee ambacho humsaidia
mwandishi wa riwaya kuweza kueleza yalikofanyika matukio ya kazi yake. Tumia
riwaya mbili kujadili mandhari yalivyotumiwa na mwandishi.
9. Kuna wakati waandishi wa tamthiliya hufaulu
wakapongezwa. Na kuna kipindi hushindwa wakakosolewa. Jadili kufaulu na
kutofaulu kwa waandishi wawili wa tamthiliya uliowasoma.
10. Tunga ngonjera yenye beti nne kuhusu umuhimu wa
kumsomesha mwanamke.