Nadharia ya Fasihi | Fasihi Simulizi
Kwa kuwa fasihi simulizi ni dhana
pana, wataalamu wengi wameeleza maana yake:
Fasihi simulizi ni aina ya fasihi
ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa
wasikilizaji na watumiaji wake. (Matteu; 1983).
Fasihi simulizi ni masimulizi
tunayopokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu awali, kwa ajili
hii basi, tutaona kuwa katika fasihi simulizi mna utumiaji wa ulumbi. (Kirumbi;
1975).
Kwa ujumla, fasihi simulizi ni
fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya masimulizi yatumiayo mdomo.
Vipera vya Fasihi Simulizi
i.
Hadithi
ii.
Ushairi
iii.
Semi
iv.
Sanaa
za maonyesho
1. Hadithi
Hadithi ni tungo za fasihi za
masimulizi zitumiazo lugha ya nathari.
Hadithi ina tanzu zifuatazo:
i.
Ngano
ii.
Tarihi/
visakale
iii.
Visasili
iv.
Vigano
v.
Soga
Ngano
Ni hadithi za kimapokeo zitumiazo
wahusika kama wanyama, miti na watu kueleza au kuonya kuhusu maisha. (Masebo
& Nyangwine; 2007).
Tarihi/ Visakale
Ni hadithi ambazo husimulia
kuhusu matukio ya kale. Matukio haya huenda yakawa ya kweli au ya kibunifu.
Visasili
Ni hadithi ambazo husimulia
kuhusu asili ya vitu fulani. Kwa mfano, asili ya fisi kuwa na miguu mifupi ya
nyuma, asili ya mbuzi kuwa na mkia mfupi… n.k
Vigano
Ni hadithi zinazoeleza makosa au
uovu wa watu ili kusaidia kurejesha maadili yaliyopotea. Nahau na methali
hutumiwa na vigano kama nyenzo ya kuufikisha ujumbe huo.
Soga
Ni hadithi ambazo hueleza mambo
kwa njia ya ucheshi.
2. Ushairi
Ushairi ni fungu linalojumuisha
tungo zote zenye kutumia mapigo kwa utaratibu maalum.
Vipera vya Ushairi
-
Mashairi
-
Nyimbo
-
Ngonjera
Mashairi ni mtungo wa kisanaa wenye mpangilio maalumu wa lugha
ya mkato, unaoelezea hisia kwa kufuata na kuheshimu utaratibu wa urari na
muwala maalumu.
Nyimbo ni tungo zenye mahadhi ya kupanda na kushuka kwa
sauti.
Ngonjera ni mashairi ya kujibishana baina ya watu wawili.
3. Semi
Semi ni fungu la tungo la fasihi
simulizi ambazo ni fupi fupi zenye kutumia picha, tamathali za semi na ishara.
Vipera vya semi ni;
Methali
Methali ni usemi wa kisanii wa
kimapokeo unaofikiriwa na jamii kuwa kweli na unaotumiwa kufumbia au kupigia
mfano na huwa umebeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa k.m.
‘hasira za mkizi furaha ya mvuvi.’ (TUKI; 2010).
Misemo
Ni fungu au mafungu ya maneno
ambayo hutumiwa na jamii ya watu kwa namna maalumu ili kutoa mafunzo. Kwa
mfano, ‘Mpaji ni Mungu.’
Nahau
Ni fungu la maneno lenye maana
maalumu isiyotokana na maana za kawaida za maneno hayo. Kwa mfano, ‘Tia
chumvi.’
Vitendawili
Ni maneno yanayoficha maana ya
kitu isijulikane kwa urahisi.
4. Sanaa za maonyesho
Sanaa za maonyesho zinajumuisha:
Michezo, majigambo, ngoma, miviga, michezo ya watoto, ngojera na vichekesho.