Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (26)
Walinilaza juu ya jiwe. Kisu
kikali kikaandaliwa kuigawanya shingo yangu. Aliyeshika kisu kikali alisogea
taratibu mahali nilipolazwa, akaanza kukishusha taratibu kama aliyetaka
kuchinja kuku.
Hakufanikiwa, ghafla kitu kama
radi kilipiga. Watu wale wote wakadondoka chini waliopoteza fahamu zao. Baada
ya hapo, akatokea mzee aliyejaa misuli – Samike.
“Asante, wangeniua wapuuzi hawa!”
nilishukuru nisiyeamini kisanga kilichotokea.
“Ondoa hofu, mapambano lazima
yaendelee Mako!” alijibu mzee.
“Lakini mzee, nguvu zangu mimi ni
ndogo sana kupambana na hawa watu, kwa nini usiingilie wewe?”
“Hapana… mimi sasa ni mzee nisiye
na ubunifu mpya. Vita hivi vinahitaji akili na nguvu. Usichoke kupambana, nipo
nyuma yako, penye shida nitatokea kama nilivyotokea leo. Adui zako
nitawachonganisha wapigane wao kama nilivyoyachonganisha majoka uliyokutana
nayo,” alimaliza kuzungumza mzee kisha akapotea.
Niliendelea na safari katika nchi
ile ya Matumbawe. Nilitembea kuelekea nisipopajua kama kawaida yangu. Nilijihisi
mpweke. Punde yule ndege akarejea tena. Safari hii alipiga kelele nyingi na
kuimba kwa sauti kali. Yote kwa sababu sasa tulizoeana vilivyo.
Wakati nikiendelea kutembea
mchana ule, mbele yangu niliona watu wengi wakiwa wamevalia mavazi ya vita,
bila shaka walikuwa askari wa nchi ya Matumbawe wakiilinda mipaka dhidi ya
wavamizi. Niliwaona wakiwa wameshika mapanga na marungu ambayo yangetosha
kumwaga ubongo wa yeyote ambaye angenasa katika mikono yao. Rafiki yangu ndege
alitoweka, nami nikajificha chini ya shimo dogo huku nikiwachungulia maadui.
Walitembea taratibu wasio na
wasiwasi. Hawakutambua kama kuna kiumbe kipya kilikuwa ndani ya nchi yao.
Nilishuhudia askari mmoja aliyekuwa na pua kubwa isivyokawaida akiwasihi
wenzake wawe makini. Kwa ukubwa wa pua ya askari huyu, bila shaka alikuwa
kitengo cha kunusa nyayo za maadui.
Wenzake walitulia, yeye akaanza
kunusa taratibu. “Kuna mtuuu!” alipiga kelele. Nikaogopa.
Aliwaongoza wenzake kuelekea
mahali nilipojificha. Kuona hivyo, nikatambaa kama nyoka chini kwa chini mpaka
upande wa pili uliokuwa na mti mkubwa. Nilisimama hapo nikaanza kukimbia
mithili ya swala aliyefukuzwa na chui.
Nilionekana. Wote wakaanza
kunikimbiza, nami nikakimbia kwa bidii kuyanusuru maisha yangu. Kwa kuwa msitu
ulikuwa mnene, nilikimbia hata nikapotea machoni mwa adui. Hapo nikaanza
kutembea kwa tahadhari kubwa.
Walikuwa askari wenye maarifa ya
vita. Walikubaliana kusambaa msituni ili waweze kuniwinda na kunikamata mzima
mzima. Mipango yao niliisikia nikiwa katika harakati za kuwatoroka kwani
hawakujua kunong’ona.
Nikiendelea kunyata taratibu
kuwakimbia mabazazi wale, nilikutana na mmoja! Aliponiona akacheka. Hakuujua
moto wangu niliouwasha katika TAHARUKI. Haraka bila salamu nilimrukia nikampiga
teke kali la shingo, alidondoka chini. Nilimuacha pale akisubiri mazishi.
Niliendelea kujikokota ndani ya
msitu. Ile roho yangu ya mapigano ikawa imenivaa, nilikuwa tayari kwa lolote.
Hata hivyo, niliogopa kiasi kama ilivyo kwa watu wengine.
Nilirushiwa rungu kubwa
nikakwepa. Aliyerusha sikumwona. Ilitosha kutambua sasa sikuwa salama, nilikuwa
hatarini nikipambana na mpuuzi asiyeonekana. Nikiendelea kushangaa, mgongoni
nilichapwa na ubapa wa panga, nikagugumia maumivu makali.
“Kama unaweza kupigana jitokeze…”
nilisema kwa sauti, nikiwa nimekunja ngumi tayari kwa mtifuano.
Niliyemwomba ajitokeze
alijitokeza. Sikuamini, alikuwa ni mtoto mdogo ambaye kwa makadilio asingezidi
miaka tisa wala kupungua miaka nane. Alivaa suruali pana nyeusi na shati la
kung’aa ambalo hata hivyo, halikuwa na vishikizo. Kifua chake laini kama kidali
cha kuku, kilionekana kikiwa kimeufunika moyo uliodunda taratibu. Alinichapa
teke la mguu nikashindwa kusimama na kujikuta nikipiga magoti bila kupenda.
Nikiwa chini nimepiga magoti
nisiye na ujanja wowote, alichomoa kamba ngumu za katani akanifunga mikono.
Akiwa amekunja midomo kwa hasira, alisema:
“Naitwa Chimota. Hakuna
aliyethubutu kuniambia nijitokeze akabaki salama!” alinichapa kofi zito,
nikapoteza fahamu.
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21