Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne
Risala ni hotuba fupi iliyokatika
maandishi na ambayo husomwa mbele ya mgeni rasmi ikielezea kuhusu mafanikio,
changamoto na maombi ya kundi fulani.
Muundo wa Risala
-
Utangulizi.
Katika kipengele hiki, cheo cha kiongozi (mgeni rasmi) hutajwa. Pia kundi
linalowakilishwa.
-
Kiini.
Mafanikio ya kundi, changamoto za kundi, mapendekezo na ushauri.
-
Hitimisho.
Kipengele hiki hukaa shukrani.
Sasa hebu tazama mfano huu wa
risala:
Swali; Jifanye wewe ni mwanafunzi
wa kidato cha nne na umechaguliwa kuandaa risala itakayosomwa mbele ya mgeni
rasmi siku ya mahafali yako ya kumaliza kidato cha nne. Andika risala
utakayoisoma siku hiyo.
RISALA YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE KWA MGENI RASMI
Ndugu mgeni rasmi, waalimu,
wazazi, wanafunzi wenzetu, wageni waalikwa mabibi na mabwana.
Ndugu mgeni rasmi, tunayofuraha
kukualika leo hii katika sherehe yetu ya mahafari haya ya kidato cha nne ili
usherehekee pamoja nasi na zaidi uweze kusikia mafanikio yetu pamoja na
changamoto zinazotukabili.
Ndugu mgeni rasmi, awali ya yote
tunapenda kutoa shukrani kwa uongozi mzima wa shule yetu kwani wamekuwa wazazi
bora waliotuongoza katika misingi imara ambayo itatusaidia sana hata baada ya
kuwa tumemaliza elimu yetu.
Ndugu mgeni rasmi, tulianza
kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 60, lakini kutokana na changamoto mbalimbali
ikiwemo maradhi, utoro na ukosefu wa fedha, tumebaki wanafunzi 40. Wavulana
wakiwa 15 na wasichana 25.
Ndugu mgeni rasmi, miongoni mwa
mafanikio tuliyonayo katika shule yetu ni umiliki wa mradi wa miti ya matunda.
Mradi huu umetusaidia sana sisi wanafunzi kuweza kupata matunda katika kila mlo
tuupatao na hivyo kuwa na afya bora.
Ndugu mgeni rasmi, mafanikio
mengine ni uwezo wetu mkubwa kitaaluma. Ni kweli kuwa, uwepo wa waalimu bora
ndiyo umekuwa sababu ya shule yetu kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yote
ya kujipima tunayofanya na shule za mkoa wetu. Ukiachilia mbali kuwa wa kwanza,
tumepata maarifa stahiki ambayo tulipaswa kuwa nayo na tunatumaini yatatusaidia
sana katika kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii yetu.
Ndugu mgeni rasmi, mbali na
mafanikio hayo, kuna changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikitusumbua. Miongoni
mwa changamoto hizo ni ukosefu wa vitabu vya kutosha. Tatizo hili limetufanya
tusome kwa shida kwani kitabu kimoja kinachangiwa na wanafunzi saba.
Ndugu mgeni rasmi, tatizo jingine
ni uhaba wa vifaa vya maabara. Uhaba huu unapelekea wanafunzi wengi kushindwa
kuisoma sayansi kwa vitendo na badala yake tunaisoma kwa nadharia tu.
Ndugu mgeni rasmi, tunatumaini
mafanikio yetu na changamoto zetu umezisikia na utatusaidia kadri ya uwezo wako
ili shule yetu iendelee kuwa sehemu salama ya kujipatia elimu. Pia,
tunakushukuru kwa kufika mahali hapa, kwani pamoja na kuwa ulitingwa na
shughuli zako za muhimu, lakini, umeweza kupata muda wa kujumuika nasi. Asante
na karibu sana.