Uhakiki wa Riwaya ya Mfadhili

Uhakiki wa Riwaya ya Mfadhili

Riwaya: Mfadhili
Mtunzi: Hussein Issa Tuwa
Wachapishaji: Macmillan
Mwaka: 2007

Utangulizi

Riwaya ya Mfadhili imazungumzia suala la mapenzi. Riwaya hii inajaribu kuchambua kwa kina mapenzi na athari zake.

Maudhui

Dhamira

i. Mapenzi

Mwandishi ameainisha aina mbili za mapenzi: Mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo.

Mapenzi ya kweli yameonekana kwa Gaddi Bullah na dada yake Bi Hanuna. Walipendana kwa dhati tena waliishi kwa furaha kabla Gaddi hajapatwa na matatizo.

Gaddi kwa Junior. Japokuwa Junior hakuwa mtoto wa Gaddi, Gaddi alimpenda kama mtoto wake wa kumzaa.

Kwa upande wa mapenzi ya uongo kuna:

Dania kwa Gaddi Bullah. Mwanamke huyu hana mapenzi ya kweli. Anamsaliti Gaddi na kuamua kuishi na Jerry.

Jerry kwa Dania. Kijana huyu hana mapenzi ya kweli. Anasafiri na kumuacha Dania akisubiri ndoa. Pia, Jerry anashindwa kumsaidia Dania pale anapougua ugonjwa wa ini. Anakimbia na hakuonekana tena.

ii. Usaliti: Nyambuja anamsaliti mume wake Gaddi kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa. Vilevile, Dania anamsaliti Gaddi na kumwacha akiwa mwingi wa mawazo.

iii. Uongozi mzuri: Mama Mlole ni kiongozi mzuri. Anamtetea Gaddi asifukuzwe kazi baada ya kuliingizia kampuni hasara ya fedha. Mama huyu anawajali anaowaongoza na kuwafanya watende kazi kwa ufanisi.

iv. Nafasi ya mwanamke katika jamii.

Mwanamke amechorwa kama:

- Kiumbe asiye na msimamo katika kufanya maamuzi.

- Mtu mwenye huruma. Nunu ana huruma. Anamhurumia rafiki yake Dania hivyo anaamua kumtafuta Gaddi Bullah.

- Katili na msaliti. Dania ni katili na hana huruma. Anamsaliti Gaddi Bullah na kwenda kuishi na Jerry.

- Chombo cha starehe. Jerry hakumpenda Dania, alikuwa naye kwa lengo la kujistarehesha tu.

Ujumbe

Mafunzo yanayopatikana katika riwaya hii ni:

i. Ni jambo jema kupendana, lakini tusipende katika kiwango cha kutufanya tuwe wajinga.

ii. Usaliti ni jambo baya linaloweza kusababisha madhara makubwa. Kifo cha Gaddi Bullah chanzo chake ni usaliti. Ulevi kupindukia wa Dania na hatimaye kuugua ini chanzo chake ni usaliti.

iii. Kiongozi bora ni yule anayewajali wafanya kazi wake.

iv. Kabla ya kufanya maamuzi, ni vyema kufikiri kwanza. Dania anakosea kufanya maamuzi ya kurudiana na Jerry. Matokeo yake, anajuta na kujikuta akimtafuta Gaddi amwombe msamaha pale anapozidiwa kitandani.

Migogoro

Migogoro ya wahusika

Gaddi na Nyambuja. Huu unatokea pale Gaddi anapomfumania mke wake Nyambuja.

Gaddi na Dania. Huu unatokea pale Dania anapoamua kurudiana na mpenzi wake wa zamani Jerry.

Bi Hanuna na Nunu. Chanzo cha mgogoro huu ni Nunu akishirikiana na Boaz kumteka Bi Hanuna ili awaeleze mahali alikojificha Gaddi Bullah.

Jerry na Dania. Mgogoro huu unasababishwa na Jerry kumkimbia Dania siku ya harusi. Pia, Jerry hatokei kumsaidia mpenzi wake kipande cha ini ili aweze kuokoa maisha yake.

Mgogoro wa nafsi

Dania anapatwa na mgogoro wa nafsi. Yu kitandani akiugua ugonjwa mbaya, lakini anafahamu kuna mtu alimkosea. Anatamani kumwomba msamaha Gaddi Bullah, lakini Gaddi hapatikani.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa, busara inahitajika katika mapenzi.

Msimamo

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi.  Anaamini busara itaepusha matatizo yanayosababishwa na mapenzi.

Fani

Muundo

Riwaya hii imetumia muundo wa urejeshi. Sura ya kwanza wanaonekana Nunu na Boaz wakimtafuta Gaddi Bullah. Sura zinazofuata, zinaeleza maisha na mikasa ya Gaddi, kwa nini alitoweka na maisha yake ya nyuma.

Mtindo

Monolojia

Dayolojia

Barua. Uk 65

Mandhari

Arusha, Dar es Salaam, Pemba.

Nyumbani, ofisini, hospitali, barabarani na baa.

Matumizi ya lugha

Tamathali za semi

Tashibiha

"Gari iliruka mbele kama jiwe!"

Takriri

"Sitaki! Sitaki! Sitaki!"

Mdokezo

"Ni kweli anti..."

Tanakali sauti

"Ko! Ko! Ko!"

Methali, misemo na nahau

Jibu lile lilimkata maini

Hakuna marefu yasiyo na ncha

Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni

Picha na taswira

Mwandishi amewachora wahusika wake na kumfanya msomaji awe kama anatazama televisheni. Anamwelezea Nunu akiwa amevaa suruali ya kubana na jinsi msichana huyu alivyomrembo.

Wahusika

Gaddi Bullah: Mume wa Nyambunja na mpenzi wake Dania. Ana upendo wa dhati. Anaamua kumfadhili Dania kwa kumpa kipande chake cha ini.

Dania: Hana msimamo. Mlevi. Msaliti, anamsaliti Gaddi Bullah.

Nunu: Rafiki yake Dania. Anajitolea kumtafuta Gaddi Bullah.

Jerry: Mpenzi wa zamani wa Dania. Hana mapenzi ya kweli.

Wahusika wengine ni: Nyambuja, Mama Mlole, Bi. Hanuna na Dr Viran

Kufaulu kwa mwandishi

Ameonesha matatizo ya mapenzi na ndoa.

Ametumia lugha nyepesi inayoeleweka kwa wasomaji na wasikilizaji.

Kutofaulu

Mwandishi ameonesha athari za mapenzi bila kuonesha masuluhisho yake.

Kuchanganya kiingereza na Kiswahili kunawafanya wale wasiojua lugha ya Kiingereza wasielewe.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Notes za Kiswahili Kidato cha Pili | Form Two

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2025