Jinsi ya Kupata Alama za Juu katika Mitihani Yako

Jinsi ya Kupata Alama za Juu katika Mitihani Yako
Siku chache zilizopita, nilipata wasaa wa kutembelewa na mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye swali lake lilikuwa moja tu, “mwalimu, nawezaje kupata A katika mtihani?” nilimtazama kwa jicho la udadisi kijana yule mdogo, akanikumbusha mkasa wa mwanafunzi wangu aliyewahi kuwa ‘Tanzania One’ mwaka fulani kidato cha nne, kijana yule alipenda kunisumbua kwa swali kama hili, na leo naulizwa tena swali lilelile.
“Achana na A, hakikisha una maarifa stahiki unayopaswa kuyapata katika masomo ili uweze kuisaidia jamii yako!” nilijibu.
“Maarifa tayari ninayo, hiyo A naipataje?” aliuliza, jicho lake kalikaza kwangu.
Sikutaka kubishana na mwanafunzi wangu mwenyewe, nikamwamuru aketi katika kiti kidogo kilichokuwa mbele ya ofisi kisha nikamtaka anisikilize kwa makini. Baada ya kurekebisha koo, nikazungumza taratibu:

“Usile chakula chochote masaa matatu kabla ya mtihani

 Kula chakula  muda mfupi kabla ya mtihani huuchosha mwili kwani huwa upo katika shughuli ya umeng’enyaji wa chakula.

Pata usingizi wa kutosha

Usingizi unakuweka sawa na kukupa nguvu. Hakikisha angalau unalala masaa sita kwa siku.

Nukuu unaposoma

Usisome kama gazeti. Nukuu mambo muhimu, pia, unapomaliza kusoma hoja fulani, kwa mfano, ‘importance of studying history, andika pembeni kujipima kama unazikumbuka hoja ulizozisoma.

Kula mboga za majani na matunda

Pia upatapo nafasi, kula ‘chocolate’ kwa kiasi kidogo.

Kuwa na ratiba ya masomo na ifuate ratiba hiyo

 Usivunje ratiba yako bila sababu maalumu. Iheshimu ratiba yako, tunza muda.

Fanya mitihani ya 'pre necta' na 'solve past paper'

Itakusaidia kujua maswali yanavyotoka.

Wakati wa kufanya mtihani wako, hakikisha huchafui kazi yako 

Uchafu, hupunguza alama.

Mwisho, jiamini,” 

nilimaliza, nikafunga sentensi zangu na kumtazama bwana mdogo alikuwa akinisikiliza kwa makini.
“Asante mwalimu,” alishukuru, kisha akaendelea, “sasa naomba unipe mbinu zitakazonisaidia kuifuata ratiba yangu bila kuivunja.”
“oooh… hilo nitakujibu siku nyingine, kwa sasa ninaelekea Kigogo, kuna kigogo nakwenda kukutana naye haraka,” nilijibu, tukatazamana kwa macho yaliyosema KWA HERI YA KUONANA.
Mwalimu Makoba

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024