Uhakiki wa Tamthiliya ya Morani| Kidato cha Tano na Sita

Uhakiki wa Tamthiliya ya Morani| Kidato cha Tano na Sita


TAMTHILIYA; MORANI 
MWANDISHI; EMMANUEL MBOGO 
WACHAPISHAJI; DUP 
Mhakiki: Mwalimu Makoba

Morani, ni tamthiliya inayoeleza kuhusu wimbi kubwa la uhujumu uchumi lililoikumba nchi ya Tanzania mara baada ya kupata uhuru. Mtikisiko wa kiuchumi, ulisababisha baadaye Tanzania ikakubaliana na mkataba wa SAP na kuingia katika ubepari kwa mara ya pili baada ya mwaka 1967 kuamua kuishi kijamii bila mafanikio.

Tamthiliya hii inayaangazia maisha ya wahuni wavunja sheria waliokabidhiwa madaraka ya umma, na vijana wazalendo wanaopambana kuhakikisha mali ya umma inalindwa na nchi inasonga mbele.

Dongo ni mfano wa vijana wazalendo, anashirikiana na Jalia kupambana na wahujumu. Wahujumu hawa wanawakilishwa na watu kama, Nungunungu. Nungunungu ni Nungunungu kweli kwani pamoja na wizi wake wa mali ya umma, bado anafanya udhurufu kwa kumpachika mimba binti mdogo wa shule Aisha.

Kwa bahati mbaya, wahujumu uchumi hawashindwi. Mpaka mwisho mpambano unaendelea kuwa mkali na kupelekea kuuawa kwa kijana mzalendo Dongo. 

Japo hiki ni kitabu cha ubunifu tu, mambo yake yanaakisi jamii yetu ya Tanzania na Afrika kwa jumla. Ukitaka kupambana na uovu, JIANDAE!

MAUDHUI

i. DHAMIRA 

• Uhujumu uchumi 

Uhujumu uchumi ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya. Nungunungu anahujumu uchumi wa nchi kwa kuvusha karafuu na kahawa nchi ya jirani kwa magendo, yeye na wahujumu wengine wanachelewesha maendeleo. 

• Uzalendo 

Watu wanatakiwa waipende nchi yao ili paweze kupatikana maendeleo. Dongo na Jalia ni mfano wa vijana ambao wanaipenda na kuipigania nchi. wote kwa pamoja wanapambana na mhujumu uchumi Nungu. 

•Matabaka 

matabaka mawili yanaonekana, 

Tabaka la wenye nacho. Hili linawakilishwa na Nungunungu, tabaka hili linasaliti nchi na kuhujumu uchumi. Mfano, Nungunungu anavusha karafuu kwa magendo pia anamiliki nyumba kubwa Marekani. 

Tabaka la wasionacho. Hawa wananyanyasika na kuporwa haki yao, tunamuona kabwela mmoja akifungwa jela kwa kosa la kukutwa na mafungu mawili ya mchicha na dawa ya meno! 

•Nafasi ya mwanamke katika jamii. 

Mwanamke amechorwa kama, 

- Mwanamapinduzi. 

Mwanamke Jalia yuko msitari wa mbele kuhakikisha anawakamata wahujumu uchumi wote kwa maslahi ya nchi. 

- Mzalendo 

Jalia ana mapenzi ya kweli na nchi yake. Uzalendo alionao ndio unaomfanya ahakikishe anapambana na wahujumu wote ili waweze kukamatwa. 

- Mwenye tamaa ya pesa. 

Tamaa ya pesa inamfanya msichana mdogo Aisha atembee na mzee mtu mzima Nungunungu. 

- chombo cha starehe. 

Nungunungu hana mapenzi ya kweli na Aisha, anamhitaji msichana huyu kwa ajili ya kujistarehesha, Aisha anapopata mimba Nungu anaruka mbali na kukataa.

ii. UJUMBE

• Usaliti ni kikwazo cha maendeleo ya taifa.

Mlemeta na yusufu wanasaliti harakati za kukamata wahujumu uchumi, suala hili linaathiri ujenzi wa jamii mpya.

• Umoja na mshikamano utaleta maendeleo.

Watu wote waungane pamoja kuhakikisha jamii inasonga mbele.

• Watu wazima ni kikwazo kwa elimu na maendeleo ya watoto.

Nungunungu ni mtu mzima ambaye anampa mimba Aisha na kumfanya afukuzwe shule.

• uhujumu uchumi ni chanzo cha umasikini uliokithiri katika jamii.

Vitendo vya Ulanguzi na biashara ya magendo vinasababisha mlipuko wa bei usioweza kuhimiliwa na watu wa tabaka la chini.

iii. MIGOGORO

•Migogoro ya wahusika

- Jalia na Mlemeta

- Jalia na Yusufu

- Jalia na Nungunungu

- Dongo na Nungunungu

- Aisha na Nungunungu

• Mgogoro wa nafsi

Huu unampata Aisha pale anapopewa mimba na Nungu, anawaza afanye nini ikiwa shule kafukuzwa, nyumbani kafukuzwa na Nungu naye hamtaki tena.

• Migogoro ya kiuchumi

Uchumi unamilikiwa na wahujumu akina Nungu. watu wa tabaka la chini wanataabika na wanaishia kumiliki uchumi mdogo. dongo anajitahidi kutengeneza usawa.

• Migogoro ya kisiasa

Serikali inapambana na wahujumu, lakini katika utawala, watawala hawaelewani, wengine wanasaliti harakati na kushirikiana na waharifu kama anavyofanya Yusufu na Mlemeta.

iv. MSIMAMO

Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani anaamini kuwa kupiga vita uhujumu uchumi na kuweka uongozi mzuri kutaondoa tatizo la umasikini katika jamii.

v. FALSAFA

Mandishi anaamini kuwa uhujumu uchumi ndicho kikwazo cha maendeleo.

FANI

MUUNDO

Tamthiliya hii imetumia muundo wa urejeshi. Mchezo unaanza kwa kuonesha kifo cha Dongo, kisha baadae sababu za kifo cha Dongo zinatolewa.

MTINDO

Mwandishi ametumia mtindo wa,
· Dayolojia
· Monolojia
· Nyimbo
· Matumizi ya nafsi zote tatu

MATUMIZI YA LUGHA

· Tamathali za semi

- Tashibiha 

"Kesho tutawasambaza kama punje za mtama."

- Tashihisi

"Jua lilipotabasamu na kutandaza mbawa zake."

- Tafsida

"Tutaenda umana au wasiwasi."

- Takriri

"Mpumbavu, mpumbavu mimi..."

· Methali, misemo na nahau

"Mwenzako akinyolewa wewe tia maji."

"Anatuchomea utambi."

"Umeota meno jana."

· Picha na taswira

- picha ya mizuka inayolima shamba la tajiri. hii inaashiri tabaka la wavuja jasho ambao wamekuwa wakifanya kazi ngumu bila manufaa yoyote huku wakiwanufaisha watu wa tabaka la juu.

- Nguzo ya uswezi. hii inamaanisha amali za azimio la Arusha.

WAHUSIKA

1. Dongo

- kiongozi mwanamapinduzi
- ni mzalendo kwa nchi yake
- anauawa kwa kupambana na wahujumu uchumi

2. Jalia 

- mwanamke anayejitoa mhanga kupambana na wahujumu uchumi
- Anashirikiana na Dongo kuandaa maandamano makubwa ya kuwapinga wahujumu uchumi.
- Anaongoza askari kumkamata mhujumu uchumi Nungu bila ya woga.

3. Nungunungu

- ni mhujumu uchumi
- anavusha karafuu na kahawa kwa magendo
- ni miongoni mwa watu wanaoliingizia taifa hasara kwa kukwepa kodi

4. Yusufu na mlemeta

- wako msitari wa mbele kukwamisha harakati za maendeleo
- wanatetea wahujumu uchumi kama akina Nungu
- ni vijana wenye tamaa ya fedha

MANDHARI

Mandhari yaliyotumika ni,
- Nyumbani
- ofisini
- porini
- baa
- hospitalini n.k

KUFAULU KWA MWANDISHI

· Mwandishi amefaulu kuonesha matatizo yanayoikabili jamii ikiwemo suala la uhujumu uchumi na umasikini.
· Amefaulu kutumia mtindo unaovutia kwa wasomaji wa kila rika.

KUTOFAULU KWA MWANDISHI

· Msanii ametumia lugha ngumu yenye utajiri wa picha nyingi na taswira, si rahisi kwa mtu mwenye elimu ndogo kuelewa kinachoelezwa kitabuni.
· Kifo cha Dongo ambaye ndiye mpigania ukombozi kinakatisha tamaa na kuwatisha wanaharakati kuwa kazi ya kudai ukombozi ni ngumu na yenye hatari nyingi.


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024