Uhakiki wa Tamthiliya ya Orodha
Jina la kitabu: ORODHA
Mwandishi: Steve Reynolds
Mwaka: 2006
Mhakiki: Mwalimu Makoba
Tamthiliya hii ya Orodha inahusu suala zima la UKIMWI na athari zake katika jamii. Mhusika mkuu Furaha na wahusika wengine, wametumiwa kuonesha athari za gonjwa hili lakini pia mbinu za kupamban na UKIMWI, zimechorwa vyema.
Jina la Kitabu
Jina hili (ORODHA) linasadifu yaliyomo. Mhusika Furaha anaandika orodha ya kusomwa kwa sauti wakati wa mazishi yake ambayo jamii ya kijiji inaamini inafichua majina ya watu waliomwambukiza virusi vya UKIMWI. Orodha inayotolewa na mhusika furaha ambayo aliomba isomwe katika mazishi yake ni, uwazi, ukweli, uadilifu, uelewa, upendo, elimu, uwajibikaji na msamaha.
Maudhui
Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika kazi za fasihi, pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.
Vipengele vya maudhui ni pamoja na , dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe na msimamo.
Dhamira
i. Athari na mapambano dhidi ya gonjwa la UKIMWI. Mwandishi anamtumia mhusika Furaha kuonesha athari ya gojwa hili, lakini pia, mapambano makali dhidi yake.
Furaha anakufa akiwa katika umri mdogo, lakini anaacha orodha ambayo itaongoza mapambano dhidi ya UKIMWI.
“Katika miezi ya mwisho, nimelala kitandani, nikifa, nikizidi kuugua.. katika ukurasa unaofuata kuna orodha ya vitu ambavyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu.” (Uk 44)
Mapambano ya UKIMWI, yataongozwa kwa kuzingatia mambo haya, uepukaji, matumizi ya kondomu, uaminifu, elimu, uelewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha.
Dhamira zingine zinazojitokeza katika tamthiliya ya Orodha ni pamoja na:
ii. Mmomonyoko wa maadili. Mhusika furaha hana maadili, anatoroka nyumbani usiku wa manane na kwenda baa kunywa pombe na wanaume. Furaha anasikika akisema,
“Sawa, lakini nakunywa kidogo tu hapa…” (uk 8)
Vilevile, mtumishi wa Mungu, padri James ambaye ndiye alitakiwa ahakikishe maadili yanakuwepo katika jamii yake, anamlaghai furaha na ufanya naye mapenzi. Padri James anasikika akisema,
“Mlango utakuwa wazi… taa zitakuwa zimezimwa… kuficha utambulisho wako. Usimwambie mtu yeyote mwanangu. Njoo peke yako”
iii. Athari za marafiki. Furaha anapotea kwa sababu ya ushauri mbaya anaopewa na rafiki yake Mary. Mary ndiye anayemfundisha Furaha kutafuta wanaume na kunywa pombe. Katika ukurasa wa tano, Mary anasikia akimnong’oneza Furaha, “Furaha… Psss… Furaha…! Haraka wanatusubiri kule baa!”
iv. Suala la mapenzi. Suala hili limejadiliwa katika nyanja mbili. Mapenzi ya kweli na mapenzi yasiyo ya kweli. Kwa upande wa mapenzi ya kweli, tunawaona baba na mama Furaha wakimuonya mtoto wao dhidi ya tabia yake mbaya. Hawa wanampenda binti yao, hivyo hawataki kumuona akipotea. Kwa sauti ya upole kiasi, mama Furaha anasikika akisema, “Hivi sasa umemaliza shule. Lazima uyafikirie maisha yako ya siku za baadaye.” (uk 21).
Upande wa mapenzi yasiyo ya kweli, wahusika Bwana Ecko, Bwana Juma, Kitunda, Mary, Padri James na Salim, hawana mapenzi ya kweli kwa furaha, wao walitaka kumtumia kwa starehe zao.
v. Hofu. Jamii inagubikwa na hofu kuu juu ya ugonjwa wa UKIMWI. Wanakijiji katia kijiji cha Furaha hawajui chanzo hasa cha gonjwa hilo. Wengine wanadhani inatokana na uchawi, wengine wakidhani pengine kwa sababu ya kugusana. Pamoja na kuliogopa gonjwa hilo, wanakijiji hawa hawaonekani kuzijua njia za kujikinga na maradhi haya.
Hofu inatanda kwa Salim, Padri James, Bw. Ecko na Kitunda pale wanaposikia kuwa Furaha kaacha Orodha. Wote hawa wanahangaika kuitafuta Orodha iliyoachwa bila mafanikio. Bwana Ecko anapomuona Kitunda ameingia katika chumba ilimolazwa maiti ya Furaha, anachimba mkwara kwa Kitunda. “Ni wewe Kitunda, unafanya nini hapa, mtoto wewe? Unawezaje kuthubutu, nitakufanya ukamatwe!”
vi. Nafasi ya mwanamke katika jamii. Hii ni jumla ya mambo yote ambayo yanafanywa na mwanamke katika jamii yake. Wakati mwingine mwanamke hufanya mambo mema yenye kufurahisha, lakini pia mwanamke huweza kufanya mambo mabaya yenye kukera. Katika Tamthiliya hii, mwanamke amechorwa katika nyanja zifuatazo:
a. Chombo cha starehe. Wanaume wanaonekana kumtumia mwanamke kama chombo cha starehe. Furaha anatumiwa na akina Bwana Ecko na wenzake kwa lengo la kuwaburudisha.
b. Pia, mwanamke amechorwa kama jasiri anayesema ukweli. Furaha ni mwanamke jasiri, anaandika orodha ya mambo yote ambayo yamemfanya aambukizwe UKIMWI.
c. Mama mlezi wa familia. Mama Furaha anajitahidi sana kuilea familia yake. Hasiti kumshauri Furaha pale anapokosea.
d. Asiye na maadili. Msichana Marry na Furaha hawana maadili yanayotakiwa katika jamii. Wanawake hawa wanakunywa pombe na wanaume usiku wa manane.
Ujumbe
Haya ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Mafunzo yanayopatikana katika tamthiliya hii ni:
i. Elimu kuhusu UKIMWI. Itolewe kwa wanajamii. Wanajamii wanapaswa kuelimishwa zaidi ili wajue nini maana ya UKIMWI na mbinu za kuepukana na maradhi haya. Katika kitabu, mwanakijiji 1, hana elimu yoyote kuhusu UKIMWI, kama asemavyo:
“Rahisi! Kuna mtu kamroga… Pengine rafiki msichana mwenye wivu.”
Mwanakijiji huyu anaamini kuwa maradhi haya huenezwa kwa njia ya uchawi.
ii. Uepukaji, matumizi ya Kondomu, uaminifu, elimu, uelewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha vitayafuta na kuyaondoa kabisa maradhi ya UKIMWI
iii. Ugonjwa wa UKIMWI upo na unaua. Ugonjwa huu unaua! Mhusika Furaha anapoteza maisha na kuiacha familia yake ikiwa na hudhuni. Mwandishi anakumbusha wanajamii kuchukua tahadhari.
iv. Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Furaha anashindwa kusikiliza ushauri wa wazazi wake. Anaamini kufuata mienendo yake mibaya mwisho anakufa kwa UKIMWI.
Migogoro
Ni mvutano, misuguano na kukosekana kwa maelewano katika ngazi ya fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, ama inaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na migogoro aya nafsi.
Migogoro ya wahusika
i. Baba Furaha na Furaha. Mgogoro huu unasababishwa na Furaha kuanza mienendo mibaya. Suluhisho la mgogoro huu ni Furaha kumkanya binti yake huyo asiendelee na tabia yake mbaya isiyoridhisha.
ii. Salim na Furaha. Huu unasababishwa na Furaha kumnyima orodha kijana Salim. Suluhisho la mgogoro huu ni Salim kuamua kuondoka na kumuacha Furaha akikata roho.
iii. Dada mdogo na Furaha. Huu unasababishwa na Dada Mdogo kumuona Furaha akijaribu kutoroka kupitia sehemu ya dirisha. Suluhisho la mgogoro huu ni Furaha kutishia kumchinja Dada Mdogo.
Mgogoro wa nafsi
Mgogoro huu unampata Furaha. Anapata majuto makuu kuhusiana na mambo yote aliyoyatenda hadi kupekelekea kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Suluhisho la mgogoro huu ni Furaha kuandika Orodha ambayo itatoa funzo kwa wanajamii ili waweze kuepuka mambo yote yasababishayo UKIMWI.
Migogoro ya kiuchumi
Uchumi mdogo (umasikini) alionao Furaha, ndio unaomfanya apate tamaa ya kujiingiza katika mahusiano na wanaume wenye pesa kama akina Bwana Ecko, ambaye ni tajiri mkubwa kijijini pale. Mzee huyu alimilika baa, aliwatapeli wasichana wadogo kwa fedha zake na vijizawadi vidogovidogo.
Falsafa
Hii ni imani ya mwandishi katika kazi yake ya fasihi. Katika tamthiliya hii, mwandishi Steve Reynolds anaamini kuwa, kutoa elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa wa UKIMWI kutapunguza maambukizi.
Msimamo
Ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Mwandishi wa tamthiiya hii ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anajadili mambo yanayosababisha kutokea kwa ugonjwa wa UKIMWI. Pia anaonesha suluhisho la matatizo hayo, anatilia mkazo suala la kutolewa elimu.
Fani
Ni ufundi wa kisanaa autumiao msanii katika kufikisha maudhui aliyokusudia. Fani imegawanyika kataka vipengele vitano ambavyo ni: wahusika, muundo, mandhari, matumizi ya lugha na mtindo.
Muundo
Mwandishi ametumia muundo rejeshi. Katika sehemu ya kwanza na ya pili, anatuonesha mahali yanapofanyika mazishi ya Furaha. Sehemu ya tatu na 20 anatuonesha juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo chake.
Mwandishi ameweka kazi yake katika onyesho moja. Katika onyesho hilo ameweka sehemu ndogondogo 20 zinazojenga na kukamilisha tamthiliya nzima.
Mtindo
- mtindo wa dayolojia au majibizano. Mfano:
Baba: unafanya nini binti yangu?
Furaha: Sifanyi kitu baba
- Mtindo wa monolojia au masimulizi. Mfano: “sehemu ya baa. Furaha na Mary wanatazamana kutokea pembeni wakati Bwana Ecko akicheza kufuata muziki kando ya baa… (uk 6)
- Matumizi ya barua. Barua iliandikwa na Furaha katika uk 44. Katika barua hii Furaha ameweka orodha ya mambo yote yaliyomfanya akapata UKIMWI.
- Matumizi ya nafsi. Mwandishi kwa kiasi kikubwa ametumia nafsi ya kwanza umoja na wingi. Pamoja na hayo, matumizi ya nafsi ya pili na ya tatu yameonekana.
Mandhari
Mwandishi ametumia mandhari ya vijiji vya Afrika ya Mashariki. Pia ametumia mandhari ya: mtaani, kanisani, barabarani, hospitali, makaburini, baa, nyumbani, vichochoroni, chumani na sebuleni.
Wahusika
Furaha
- Mhusika mkuu
- Binti mdogo wa miaka kati ya 13 na 19
- Ni malaya
- Ni mwathirika wa UKIMWI
- Ni mlevi
- Ni mkweli na muwazi
-
Mama Furaha
- Ni mama yake Furaha
- Ni mkweli na muwazi
- Ana upendo
- Ni jasiri
- Ni mpole na mchapakazi
Baba
- Ni baba yake Furaha
- Ni mkali
- Ana upendo
Mary
- Ni rafiki yake Furaha
- Ni malaya
- Ni mlevi
- Anapenda anasa
- Anatamaa
Bwana Ecko
- Ni mwanaume mtu mzima
- Ni malaya
- Ni mlevi
- Ni muathirika wa ugonjwa wa UKIMWI
- Ni laghai kwa mabinti wadogo
Juma
- Ni muathirika wa UKIMWI
- Ni laghai kwa mabinti wadogo
- Ni mlevi
- Ana tamaa
- Anapenda anasa
Padri James
- Ni mtumishi wa Mungu
- Si muadilifu
- Anauogopa ukweli na uwazi
- Ni dhaifu kwa wanawake
Wahusika wengine ni: Kitunda, Salim, Wanakijiji na Dada Mdogo
Matumizi ya lugha
- Tamathali za semi
Sitiari. Mfano, “Furaha… Waridi changa zuri.”
Tafsida. Mfano, “mayai yangu madogo.”
Mubaalagha. Mfano, “kuna majengo makubwa kiasi kwamba unaweza kuona mlima Kilimanjaro kwa juu!”
Tashibiha. Mfano, Furaha ni kama punda wa kijiji
Mdokezo. Mfano, ndiyo padre… ni…
Nidaa. Mfano, Ooo!
Takriri. Mfano, “sana, sana… sana sana.”
Tashtiti. Mfano, Mama Furaha: wewe na marafiki zako wa kiume?
Furaha: marafiki gani wa kiume
Onomatopea/ tanakali sauti. “myauuuu!”
Misemo
Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyopanda.
Kufaulu na kutofaulu kwa mwandishi
Kufaulu
Kimaudhui
i. Mwandishi amefaulu kuonesha mambo yasababishayo UKIMWI na njia za kuepuka.
Kifani
i. Mwandishi ametumia wahusika ambao wameendana na kile alichotaka kuifahamisha jamii.
Kutofaulu
i. Mwandishi ameegemea mno kijijini, utadhani ugonjwa wa UKIMWI, unawahusu wakazi wa vijijini pekee.
ii. Katika muundo mwandishi ametumia onyesho moja tu liligowanyika katika sehemu ishirini. Tamthiliya hii ilipaswa iwe na maonyesho mengi zaidi.