Jinsi ya Kuandika Barua za Magazetini | Barua kwa Mhariri
Barua hizi huandikwa na wasomaji wa magazeti kwa mhariri. Mhariri huzisoma na kuzichapa katika baadhi ya kurasa za gazeti lake. Barua hizi huwa na dhumuni moja kuu - kufichua maovu, hata hivyo, dhumuni jingine laweza kuwa kupongeza.
Muundo wa barua za magazetini
- Kichwa cha barua
- Mwanzo wa barua
- Barua yenyewe
- Mwisho wa barua
- Jina la mwandishi, anuani yake na tarehe
Sasa tutazame mfano wa barua hii iliyoandikwa na msomaji wa gazeti akiwapongeza vijana wa mtaa wake.
Hongera vijana wa Kigogo
Mhariri, Mwananchi.
Natoa pongezi kwa vijana wa kigogo kwa maamuzi safi waliyofanya ambayo yanachochea maendeleo. Maamuzi yao haya, ni sahihi na yanastahili kupongezwa na yeyote apendaye maendeleo.
Vijana hawa ninawapongeza kwa sababu, wameamua kuacha kuvuta bangi na kutumia aina zingine za madawa ya kulevya kama unga na mirungi. Badala yake, wanajihusisha na ufugaji wa kuku wa kisasa, tena kwa mbinu za kisasa.
Pia, ili kulinda amani ya mtaa, wameamua kuanzisha mfumo wa sungusungu. Ambapo sasa, Kigogo inalindwa na vijana! Hakuna tena tishio la wizi uliokuwa umekithiri miaka kadhaa nyuma. Hakika vijana wa Kigogo wamefanya maamuzi sahihi.
Jambo jingine ninalowasifia vijana wa Kigogo ni kwamba, wanahamasishana kuweka fedha zao benki. Hii itawasaidia kutunza fedha kiduchu wazipatazo kwa jasho lao, na baada ya muda, zitageuka mtaji wa biashara zitakazo watoa kimaisha.
Ninawahamasisha vijana wa mitaa mingine kama: Sogodo, Kwa Tumbo na maeneo mengine yote nchini Tanzania, waige mfano wa vijana wa Kigogo. Endapo haya yatafanyika, nchi yetu Tanzania, itapata maendeleo.
Mwalimu Makoba,
S.L.P 45,
Kinondoni.