Mtihani wa Kiswahili 1 Kwa Wanafunzi wa Kidato cha Sita 2

kitabu na kikombe cha chai


Endapo unataka kufanya mtihani huu ili usahihishwe na Mwalimu, zingatia mambo haya:
1. Mtu yeyote na popote alipo anaruhusiwa kufanya mtihani huu.
2. Fanya mtihani huu kwa kutumia aina yoyote ya karatasi.
3. Ukimaliza, piga picha karatasi hizo kisha zitume WhatsApp kwenye namba ya Mwalimu Makoba, 0754 89 53 21.
4. Subiri mtihani wako usahihishwe, Urudishiwe na ufanyiwe masahihisho.
5. Gharama ya mtihani huu ni shilingi 2,000/= (elfu mbili).
Namba za malipo ni: M – Pesa 0754 89 53 21 (Daud Mhuli) na Tigo pesa 0653 25 05 66 (Daud Makoba)
“Kwa kuwa lengo la mtihani huu ni kutaka kujua uwezo na mapungufu ya mwanafunzi ili aweze kupewa mbinu mbadala za kumsaidia kufaulu mtihani wake wa mwisho, kuangalizia majibu hakuna faida yoyote kwani lengo la mtihani si kubaini nani atakuwa wa kwanza na yupi atakuwa wa mwisho!”
It is far more honorable to fail than to cheat.
Sasa fanya mtihani wako…
Muda: Saa 3
SEHEMU A (Alama 20)
UFAHAMU
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma kwa umakini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu kwa usahihi maswali yanayofuata.
Vitabu vina manufaa makubwa kwa mwanadamu. Yeyote asiyesoma vitabu, hana tofauti na mnyama asiyejua chochote. Iko haja ya kuhamasisha mashuleni, watu wapende vitabu.
Kwa watu wengi, kusoma vitabu ni mpaka walazimishwe. Hata wanafunzi bila kuambiwa kitabu fulani kina msaada katika mitihani yao, hawawezi kukisoma. Hii ni hatari kwani tunasababisha ugoigoi wa ubongo.
Hata vile vitabu vya fasihi vyenye hadithi tamu, wanafunzi hawavisomi, wao husimuliwa hadithi yake tu, kisha wakaenda kujibia mitihani. Hili limewafanya wawe na ufaulu mdogo.
Wengi wanapomaliza shule, hudhani ndiyo mwisho wa kusoma vitabu. Kumbe elimu haina mwisho bali hujidanganya tu, huenda ikawa kwa kutokujua, bahati mbaya au makusudi.
Maarifa yote tuyaonayo yamewekwa katika vitabu. Asomaye hupata maarifa na kumfanya awe mtu wa pekee kabisa.
Kila kiungo katika mwili huhtaji kufanyiwa mazoezi. Tunahitaji kukimbia ili kuimarisha misuli yetu, kifua na miguu. Mazoezi mengine pia yanasaidia kuviweka sawa viungo vyetu vya mwili. Lakini vipi kuhusu ubongo, zoezi la kukiweka sawa kiungo hiki ni kusoma vitabu. Hakuna mbadala katika hili. Usiposoma vitabu, utakuwa na ubongo legelege usioweza kuchambua mambo kwa kina.
Huko vijijini wangesoma vitabu, wasingeua vikongwe kwa madai eti ni wachawi. Nani angethubutu kumchinja mlemavu wa ngozi kwa kudhani kufanya hivyo ni kuupata utajiri?
Kumbe basi vitabu ni kito cha thamani. Tusichoke kuzama ndani ya maandishi, kwani kufanya hivyo, kutatufanya tuibuke tukiwa bora.
Maswali
(a) Andika kichwa cha habari uliyoisoma kwa maneno yasiyozidi matano.
(b) Eleza mawazo makuu mawili ya mwandishi.
(c) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika habari hii.
(i) ugoigoi
(ii) elimu
(iii) ubongo
(iv) legelege
2. Fupisha habari uliyoisoma kwa maneno mia moja.
SEHEMU B (Alama 20)
MATUMIZI YA SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali mawili (2) kutoka sehemu hii.
3. (a) Eleza maana ya viambishi vya O-rejeshi .
(b) Unganisha sentensi zifuatazo kwa kutumia O-rejeshi .
(i) Kanu ameleta mpira wa miguu. Ulikuwa unahitajika mpira.
(ii) Rukia anatafuta vitabu. Vitabu vimekwisha.
(iii) Gazeti lilichapwa. Gazeti limekwisha.
(iv) Mtoto ametekwa nyara. Mtoto ameptaikana.
(v) Yule msichana amesimama pale. Yule msichana ni dada yangu.
4. Kwa kutumia mifano bainisha kazi mbili za mnyumbuliko na kazi tatu za uambishaji katika lugha ya Kiswahili.
5. Mtumiaji wa lugha ya Kiswahili ambaye ni mahiri wa lugha zingine, umahiri wake hukabiliwa na changamoto mbalimbali. Kwa kutumia hoja nne na mifano, fafanua changamoto hizo.
6. Bainisha matumizi ya “ki” iliyopigiwa mstari katika sentensi zifuatazo:
(i) Kiti ki dogo
(ii) A ki ja apewe mzigo wake
(iii) Kitabu ki mechanika
(iv) Kiti ki kidogo
(v) Wana ki subiria
(vi) Analima a ki imba
(vii) Atavuna alicho ki panda
Ukurasa wa 3 kati ya kurasa 4
(viii) Ki toto hiki sikiwezi
(ix) Aliruka juu ki huni
(x) Anacheza ki toto
SEHEMU C (Alama 20)
UTUNGAJI
Jibu swali la saba (7) .
7. (a) Taja na kueleza mambo muhimu saba ya kuzingatia katika kuandika kadi ya mwaliko.
(b) Jifanye wewe ni mzazi wa mwanafunzi Sikujua Kizito anayehitimu Kidato cha Sita mwaka 2017. Andika kadi ya mwaliko kuwaalika ndugu, jamaa na marafiki katika sherehe ya kumpongeza mtoto wako itakayofanyika tarehe 7/6/2017. Jina lako liwe Sikutegemea Kizito .
SEHEMU D (Alama 20)
MAENDELEO YA KISWAHILI
Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.
8. Waingereza na Waarabu walidumaza maendeleo ya Kiswahili wakati wa ukoloni nchini Tanzania. Thibitisha dai hilo kwa kutumia hoja nne kwa Waingereza na hoja nne kwa Waarabu.
9. Eleza kazi za BAKITA na UKUTA katika kukuza na kueneza Kiswahili. Toa hoja tatu za BAKITA na hoja tatu za UKUTA.
SEHEMU E (Alama 20)
TAFSIRI
Jibu swali la kumi (10) .
10. “Kazi ya kutafsiri ina taratibu mahususi.” Fafanua dai hili kwa kueleza mambo muhimu sita ya kuzingatia wakati wa kufanya tafsiri.

Popular posts from this blog

Notes za Kiswahili Kidato cha Pili | Form Two

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2025