Maneno Kuhusu Format (muundo) Mpya 2019 Mtihani Kidato cha 4

necta format 2019
Saa moja na nusu usiku, vinasikika vishindo katika kona ya mwisho nifike nyumbani kwangu. Nageuka kutazama, naona watu wakikimbia mbio kunifuata nilipo. Nashtuka, natazama bahasha ya kaki iliyojaa fedha… Sikuiweka mbali, niliishika kwa mkono wa kushoto. Naendelea kutazama, sasa wananikaribia na natambua idadi yao wapo 4+5 yaani tisa. Nawaza kimya kimya, “nimepita kote huko salama, naporwa nimefika nyumbani?” nataka kukimbia, lakini nakumbuka mimi ni mwalimu wa walimu na wanafunzi. Sipaswi kukimbia hovyo hovyo mithili ya kichwa cha mwendawazimu kikiusaka mpira! Hata hivyo, nakaa katika mkao wa kujihami, mguu wa kulia nauacha nyuma kidogo kisha najisemea, “wakinikaribia, nitampiga teke yule mfupi, kisha nitafurumusha kareti kwa wale nane waliobaki. Nasimama wima!
Vijana wale wananifikia, nabaini si watu wabaya, pengine ndiyo sababu riwaya yangu hii inageuka tamthiliya. Kumbe ni wanafunzi wangu mwenyewe!
MWANAFUNZI 1: Mwalimu, tusaidie format mpya ya mtihani imetoka.
MIMI: Niwasaidie nini? Kuirudisha ilipotoka?
MWANAFUNZI 2: (Akicheka) Hapana mwalimu, tusaidie kutuelewesha ndiyo ikoje hii? Hatujui tuelimishe.
MIMI: Format kama mnavyoiita, ni muundo tu wa mtihani, mada mnazosoma darasani ni zilezile hakuna mabadiliko. Ila muundo wa mtihani uliokuwa unauona katika mitihani iliyopita, utabadilika.
MWANAFUNZI 3: Nimekuelewa, lakini hebu ongeza mifano katika hoja.
MIMI: Nitatoa mfano katika somo la Kiswahili, format ya zamani ilikuwa na maswali 15. Na swali la 15 lilikuwa la lazima, lakini format mpya ina maswali 12. Pia jambo jipya ni kwamba, swali la kwanza litakuwa la kuchagua (multiple choice). Swali la pili litakuwa la kuoanisha, zamani swali la pili lilihusu kufupisha habari uliyosoma!
MWANAFUNZI 4: Kwa nini wamefanya mabadiliko haya mwalimu?
MIMI: Katika ripoti yao, wamesema wamefanya mabadiliko haya ili kuisaidia Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati na kupata viwanda. (Wote wanacheka).
MWANAFUNZI 5: Hiyo ni sababu dhaifu sana Mwalimu, kwa sababu sidhani kama kubadili muundo wa mtihani kunaweza kuleta viwanda, labda kama tungebadili mada zinazosomwa. Hebu tupe sababu nyingine waliyotoa.
MIMI: Sababu nyingine ni kuendana na mabadiliko ya silabasi na kuanzishwa kwa sera mpya ya elimu mwaka 2014. (Wanaafiki hoja hii.)
MIMI: (Nikiwatazama Mwanafunzi 6,7,8 na 9 ambao kwa muda wote wako kimya)… kumbukeni kuwa, kilichobadilika ni muundo wa mtihani kama vile idadi ya maswali, aina ya maswali n.k, lakini mada za kusoma ni zilezile! Katika mitihani yangu mipya ya Online, nitatunga kwa kutumia format mpya ili muweze kuona ilivyo!
Tunaagana kwa furaha. Wao wanashika njia yao, nami nashika njia yangu na ile bahasha ya kaki yenye fedha.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1