Bwana Mako na Simba Mzee | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 1

kava la kitabu mikasa elfu moja ya bwana mako

Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako ni mkusanyiko wa hadithi tamu kuliko hadithi zote ulizowahi kusoma. Mwalimu Makoba kaandika hadithi hizi kwa miaka 10 mfululizo ili kuwafanya watu wapende kusoma. Anayesoma hupata faida hizi: kuchangamsha akili, kupunguza mawazo, kuongeza maarifa, kuwa na kumbukumbu na kuwa na kinga dhidi ya magonjwa ya akili!
Mkasa wa Kwanza
Bwana Mako na Simba Mzee
Katika kijiji kimoja cha kijani, waliishi watu wenye furaha. Furaha yao ilidumu kwa miaka mingi mpaka walipovamiwa na simba mmoja mzee. Simba huyu mzee, alikuwa katili kwa wanakijiji, kijiji kikakosa amani na furaha yao ikateketea kama fedha za mlevi ziteketeavyo baa.
Simba mzee alianza unyama wake kwa kumuua mzee maarufu wa kijiji aliyependwa na watu wote. Inasemekana kuwa mzee alikuwa katika shamba lake akipalilia mahindi, ndipo alipovamiwa na simba mzee ambaye alimrukia shingoni na kumuua kisha akamla mpaka aliposhiba na kuacha sehemu ndogo ya mwili.
Simba mzee hakuishia hapo, aliwatafuna watoto wawili mapacha waliokuwa wakichoma viazi pembezoni mwa nyumba yao. Basi baada ya tukio hilo, habari ya simba huyo ikaenea kwa wanakijiji na kila mmoja akajifungia katika nyumba yake akiogopa kutoka kwa hofu ya yule simba mzee.
Kwa kuwa wanakijiji walijifungia ndani, Simba yule mzee alipohisi njaa, akawinda watu asiwaone, akaanzisha kioja kipya, alianza kubomoa nyumba za watu na kuwatafuna wote aliowakuta humo.
Tukio la kwanza alivunja nyumba ya mganga wa kijiji, mganga alijifungia ndani kwake yeye na wanae, nao wakawa wamewasha moto ili waweze kuonana usiku ule, simba alivunja mlango wao, akaingia na kuwatafuna wote, hata mganga alitafunwa, kweli mganga hajigangi!
Nyumba ya pili ilikuwa ni nyumba ya mpiga ngoma wa kijiji, tukio hili husikitisha sana, kwani mpiga ngoma alikuwa na mke wake, mtoto wake mmoja wa kiume mwenye mwaka mmoja na mama yake mzazi, wote wakatafunwa na simba yule.
Wanakijiji waligundua kuwa, milango yao haikuwa imara kuweza kumzuia simba kuingia atakapo, lakini hawakuwa na namna yoyote ya kufanya, isipokuwa kukaa hivyo wakiomba Mungu wasije uawa na Simba mzee. Pia walitamani kupeleka taarifa kwa mkuu wa wilaya ili atume jeshi lije kumwondoa Simba yule, lakini hakupatikana mwanamume aliyeweza kutoka ndani ya nyumba yake kwa hofu ya yule Simba. Basi kijiji kikawa kimya kama hakina watu. Inasemekana kwa sababu ya ule ukimya, hata hatua za sisimizi ziliweza kusikika!
Bwana Mako aliishi katika kijiji hicho, nyumba yake ilijitenga na nyumba za wanakijiji wengine, aliijenga katika kilima. Ungeziona, ungezani nyumba yake ni askari mkuu na zile zingine ni askari wadogo nao wanaamrishwa mguu pande mguu sawa!
Bwana Mako alishtushwa na ukimya wa kijiji, mwanzo alidhani labda shughuli zimewachosha hivyo kwa sababu ya uchovu hawana nguvu ya kupiga kelele,

lakini baada ya siku kadhaa akahisi hatari, akaamua kuteremka kilimani ilipokuwa nyumba yake na kwenda kwa wanakijiji wengine.
Alitembea katika hali ile ya ukimya mpaka alipozifikia nyumba za wanakijiji wengine.
“Wanakijiji kulikoni, mbona kimya na mmejifungia ndani ya nyumba zenu?” aliuliza. “Tatizo nini ndugu zangu?”
Hakuna aliyejibu, wanakijiji walikaa kimya kwa hofu, pengine walidhani simba yule angetokea na kummeza Bwana Mako mara moja. Naye Bwana Mako kuona watu wako kimya, aliamua kusogea katika dirisha la fundi cherehani wa kijiji.
“Fundi, fundi,” alinong’ona. “Nieleze, tatizo nini?”
“Simba ndugu yangu,” alijibu, “anatafuna watu kama atafunavyo swala.”
Bwana Mako alipopata taarifa hizo, alisogea katikati ya nyumba zote.
“Ndugu zangu,” alisema kwa sauti kubwa, “wanaume msijifungie ndani, njooni nje twende tukapambane na huyu Simba. Mkiendelea kubaki ndani hakuna atakayesalia kwa sababu milango yetu siyo imara kiasi cha kumzuia asiivunje. Ni heri tufe tukipigana naye kuliko tujifungie ndani naye aje atukamate kama mwewe akamatavyo vifaranga. Je mnavyakula vya kutosha siku ngapi? Sasa hamuoni mnawindwa na njaa pamoja na simba? Aliyetayari kupambana ajitokeze sasa.”
Zilipita dakika tisa tangu azungumze maneno hayo. Hakuna mwanamume aliyetoka ndani kuja nje kuungana naye, Bwana Mako akaamua kuingia msituni peke yake kumsaka Simba mzee. Akiwa anatembea alirushiwa mkuki.
“Chukua mkuki huo utakusaidia kupambana na simba huyo,” ilisema sauti kutoka nyumba moja, kisha ikasikika sauti ya kufunga mlango, pakawa kimya.
“Ni uonevu kumuua simba mzee kwa mkuki, simba mzee anauliwa kwa viganja vitupu!” alijibu Bwana Mako kisha akapotelea msituni.
Wanakijiji walichungulia katika madirisha yao kama wanaoangalia sinema. Ukimya ukatanda tena kwa dakika ishirini.
Ukimya ulivunjwa na miungurumo ya simba, wanakijiji walitazama lakini hawakumuona simba waliishia kusikia ile miungurumo yake tu. Baadaye ikasikika sauti ya Bwana Mako akilia kisha pakawa kimya. Kimya kuliko muda wote.
Baadaye vilianza kusikia vishindo vikija katika kijiji. Hofu ikawajaa, wakasali kila mtu kwa imani yake wasijetafunwa na yule simba.
Vishindo viliendelea kusikika mpaka walipoona kitu ambacho hawakuamini. Bwana Mako alibeba mwili wa Simba yule mzee katika mabega yake. Naye alitembea kwa vishindo vya shujaa.
Furaha ilirejea tena kijijini, wanakijiji walifungua milango yao wakampokea Bwana Mako na kumshukuru kwa msaada wake. Baada ya kumaliza maombolezo ya ndugu zao waliotafunwa na Simba yule, walifanya sherehe kubwa kufurahia ushindi wa Bwana Mako.
Jiunge katika Group la whatsapp uwe wa kwanza kupokea mkasa wa pili Jiunge Hapa

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024