Niliugua Ugonjwa wa Ajabu Nikatibiwa na Babu wa Kichina 1
Simulizi hii haina uhusiano wowote na tukio la kweli lililowahi kutokea, bali ni matokeo ya fikra adimu za Mwalimu Makoba.
Tajiri Maige aliniita nyumbani kwake. Hii ilikuwa
ni mara ya nane, kwa mara zote saba, ameniita asifanikiwe kunishawishi kwa
jambo alilohitaji. Alihitaji kunituma nchi za mbali, niende uchina kwa kazi ya
kumtafuta binti yake ambaye tangu aondoke nchini kwenda China kusoma, hajapata
kurejea tena na sasa yapata mwaka wa saba. Hakuna barua, hakuna simu, hakuna
mawasiliano!
“Mako… Mako… Mako…” aliniita tajiri Maige, “safari
hii sitegemei jibu la hapana. Kila kitu kipo tayari. Naomba sana, nenda kamtafute
mwanangu wa pekee Vida.”
Ukimya ulitawala kwa dakika saba sebuleni
pale. Sikuwa tayari kwenda mbali na familia yangu, nilihitaji kupumzika na
nilizichoka purukushani. Hata hivyo, nilijiwa na moyo wa huruma, nikajikuta nikitamka kwa kauli thabiti.
“Nitakwenda peke yangu. Nitarudi na binti.”
Hivyo ndivyo nilivyokubali kuondoka nchini
ili kwenda China kwa kazi ya kumtafuta mtoto pekee wa tajiri Maige. Ni binti
ambaye aliondoka kwenda kusomea udaktari, lakini hakurejea yapata miaka saba. Tajiri
Maige ambaye alifiwa na mke wake miaka tisa iliyopita, furaha pekee aliyokuwa
nayo ilikuwa ni kumuona binti yake kipenzi Vida.
Siku ya Jumatatu nilikuwa ndani ya ndege ya
kutoka Dar Es Salaam kwenda Beijing china. Nilikaa daraja la kwanza na
iligharimu shilingi za kitanzania milioni saba na laki tatu kwa safari moja ya
kwenda tu. Waliokaa daraja la pili yaani ‘bussiness’, wao iliwagharimu milioni
tano, na waliokaa daraja la mwisho yaani ‘economy’, iliwagharimu shilingi
milioni moja. Kukaa daraja la kwanza, ilikuwa raha ajabu na niliona kama dege
lile la kampuni ya ‘Fly Emirates’ kama langu!
Zilipita saa mbili baada ya safari yetu
kuanza. Hapo ndipo lilipotokea jambo la kuogopesha na kukatisha tamaa. Ndege yetu
iligonga kundi kubwa la ndege ambao inaaminika walikuwa kunguru. Injini moja
ikazima, hofu ya kifo, ikatufanya tusahau yale matabaka yetu ya daraja la
kwanza, la pili na la tatu, wote tulishikwa na hofu kuu. Abiria wengi walilia,
wachache walikaa kimya, lakini wakitetemeka.
Itaendelea...