Mbinu Saba za Kufaulu Mtihani Wowote Shuleni
Namba
saba ni namba ya ajabu katika orodha ya namba tulizonazo. Kuna mabara saba,
bahari saba, elimu ya msingi ina madarasa saba, upinde wa mvua una rangi saba,
tuna sikukuu inaitwa sabasaba, tuna maajabu saba ya dunia, na sasa nakwenda
kukueleza mbinu saba za kufaulu mtihani wowote. Tafadhali zizingatie mbinu hizi. Lakini kabla sijaeleza, hebu tafakari japo kwa dakika moja, inakuwaje shule fulani wanafeli wanafunzi wote, yaani darasa zima halikuwa na mtu mwenye uwezo wa kufaulu? Lakini pia, inakuwaje shule fulani wanafunzi wote wanafaulu tena kwa daraja la kwanza, ama unadhani shule hizo zimekuwa zikiiba mitihani, siyo kweli, nimefanya kazi katika shule za aina hii kwa miaka mingi na sijawahi kuona udanganyifu wowote. Tofauti ya shule zinazofaulisha kwa wingi na zile zinazofelisha kwa kiwango kikubwa, ipo katika mbinu hizi saba. Ni mbinu ambazo bahati mbaya wanafunzi wengi hawaambiwi, lakini wewe una bahati, zisome mbinu hizi zaidi ya mara moja na utaweza kufaulu mtihani wowote.
1.
Fundishwa
Kuwa
na vitabu vya somo, kusoma somo hilo peke yako na kuliewa haimaanishi kwamba
hutakiwi kufundishwa. Inawezekana unachosoma unakielewa lakini kuna mambo
unakosa kwa sababu huna mtu anayefahamu kitu hicho. Hivyo kama unataka kufaulu
mtihani wako, tafuta Mwalimu akufundishe. Unapotafuta Mwalimu, tafadhali kuwa
makini kutafuta Mwalimu mwenye taaluma na ujuzi. Walimu wengi ni wazuri, lakini
bahati mbaya kuna walimu wachache ambao siyo walimu bali ni watu waliovamia
tasnia, hivyo kuwa makini katika kumtafuta Mwalimu sahihi.
2.
Jisomee
Soma
yale uliyofundishwa, pia soma ambayo bado hujafundishwa. Hakikisha unakuwa na
ratiba ya kujisomea kila siku. Tengeneza ratiba ambayo haitakubana sana,
ukitengeneza ratiba ya masomo ambayo inakubana sana, hutaweza kuitimiza na
utajikuta husomi kabisa. Hivyo ni vyema kuwa na ratiba ya masomo ambayo
unaamini unaweza kuifuata.
3.
Fanya
maswali ya Mwalimu
Mwalimu
akikupa maswali lengo lake ni kutaka kufahamu uwezo wako, wapi ulielewa na wapi
hukuelewa. Mwalimu hutoa maswali kupima uwezo wako wa masomo pia udhaifu
ulionao. Kupitia maswali unayofanya, unamsaidia mwalimu kubadili mbinu ili
uweze kuelewa. Usipofanya maswali, mwalimu hataweza kufahamu uwezo wako na
namna ya kukusaidia. Hivyo, fanya maswali.
4.
Fanya
mitihani ya mwalimu
Kama
yalivyo maswali, mitihani nayo hulenga kukupima uwezo wako pamoja na madhaifu
uliyonayo. Faida kubwa ya mitihani ni kukusaidia kufanya mazoezi ya kutosha
kabla ya mtihani wako wa mwisho. Mtihani wa mwalimu, ni mazoezi ya mtihani wako
wa mwisho.
5.
Pitia
mitihani iliyopita
Pitia
mitihani iliyopita hususani mitihani ya NECTA. Katika mitihani hii, utaweza
kuona namna mtihani wako wa mwisho ulivyo, utaweza kuona aina ya maswali na
mpangilio wa mtihani huo. Huwezi jua, inawezekana baadhi ya maswali yakajirudia
katika mtihani wako. Hata hivyo, usitegemee bahati hii, badala yake soma kila
kitu.
6.
Soma
vitabu/notes sahihi
Wengi
wameshindwa mitihani kwa sababu hawakuwa na vitabu sahihi vya kusoma. Vitabu ni
vingi na vinapatikana kila mahali. Vitabu vingine vinapatika mitandaoni, na
vingine katika maduka ya vitabu. Bahati mbaya sana, vitabu vingi havijafuata
mtaala katika kuandikwa kwake na haijulikani sababu ni nini. Hata uwe na uwezo
mkubwa, kitabu kibaya kitakupa matokeo mabaya. Hivyo, tafuta vitabu sahihi.
7.
Zingatia
muda
Weka
ratiba na ifuate. Kuwa na muda wa kuongea na marafiki, kutembea, kufanya usafi
na mambo mengine mbalimbali. Zingatia na tumia vizuri muda vinginevyo utashangaa
tarehe ya mtihani inafika na wewe hujakamilisha maandalizi ya mtihani huo.
Hivyo basi, mbinu saba za kufaulu mtihani wowote shuleni ni: kufundishwa, kujisomea, kufanya maswali ya mwalimu, kufanya mitihani ya mwalimu, kupitia mitihani iliyopita, kusoma vitabu au notes sahihi na kuzingatia muda.