Utungaji wa Kazi za Fasihi Simulizi | Kiswahili Kidato cha 2

Mvulana kasimama katika mti.

Kazi za fasihi simulizi hazikutokea tu, kuna mtu alitunga kazi hizo. Mada hii, inaangazia utungaji wa kazi za fasihi simulizi:

Utungaji wa mashairi

Kanuni za Utungaji wa Mashairi

Utungaji wa mashairi una kanuni mbili:
1. Fani
2. Maudhui
Katika fani, mshairi azingatie lugha anayotumia kama: tamathali za semi, methali nahau na misemo pamoja na picha na taswira.
Pia, mshairi azingatie kama mtindo wa shairi, kama ni shairi la kimapokeo au shairi la kisasa.
Pia, mshairi azingatie muundo wa shairi lake, kama atatumia mistari miwili, mmoja, sita ama apendavyo yeye.
Katika maudhui, unapotunga shairi zingatia wazo lako.  Mfano: ni lipi lengo la wewe kutunga shairi? Inawezekana unatunga shairi ili kuzungumzia hali ya umasikini unaoikumba nchi yako, au pengine una lengo tofauti.
Pia, zingatia ujumbe au mafunzo yanayopatikana katika shairi ulilotunga. Unalenga kufikisha ujumbe gani?

Mfano wa shairi lililotungwa kwa kuzingatia kanuni

Kubaka
Nimekuwa nikipima, najiuliza kichwani,
Watu kugeuka kima, asili yake nini,
Si busara si hekima, wala halina utani,
Kubaka huo unyama, chanzo chake kutamani.

Ninaanza kuwasema, tuchungue kwa makini,
Midume iso heshima, inavuruga amani,
Hawana hata huruma, utadhani hayawani,
Kubaka kama mnyama, chanzo chake kutamani.
(HRT Muzale)

Ngonjera

Ngonjera ni aina ya igizo linalotungwa kwa kufuata kanuni za ushairi wa kimapokeo. Katika ngonjera, kuna wahusika wawili au zaidi wanaojibishana. Mara nyingi mwishoni mwa ngonjera wale wanaobishana hukubaliana na hapo ngojera huwa imekwisha.
Kanuni za kutunga ngonjera
1. Kuteua mada
Mada inaweza kuwa, mjini au kijijini, ukosefu wa lishe kwa watoto n.k
2. Kuweka dhamira
Ni lipi wazo kuu la mtunzi wa ngonjera? Wazo kuu linaweza kuwa, maendeleo, uhalifu na amani.

Mfano wa ngonjera

MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU 2020
Mzee
Uchaguzi umefika, viongozi kuchagua,
Hakuna kubabaika, kama moto wa mabua,
Rushwa hiyo kwangu taka, busara kuibagua,
Mzee ama kijana, lazima kupiga kura.
Kijana
Wala Sitapiga kura, kupoteza muda wangu,
Chagua wauza sura, wasioona uchungu,
Kiona vyao vipara, ni vyeusi kama vyungu,
Nasema kura sipigi, uchaguzi ukifika.
Mzee
Kijana elewa sasa, faida za kuchagua,
Tena si vyema kususa, taja angukia pua,
Na usitoe ruksa, serikali kuiua,
Mzee ama kijana, lazima kupiga kura.
Wote
Kushiriki uchaguzi, ni bora si kulalama,
Hatuachi uchokozi, kwa uchaguzi salama,
Hakuna kumwaga chozi, kwako we baba na mama,
Mzee ama kijana, lazima kupiga kura.

Maigizo

Maigizo ni tendo la kuiga sura, tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine.

Taratibu za kutunga maigizo

1. Kuchagua tukio la kuigizwa
Tukio hilo, liwe na mchango changa katika jamii, ikiwemo kuelimisha.
2. Kuchagua mahali pa kutendeka kwa jambo
Mahali panaweza kuwa: ofisini, shuleni, kijijini barabarani n.k
3. Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa
Hapa mwandishi anaweza kutumia fumbo, vichekesho n.k
4. Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo
Maudhui hujikita katika migogoro au mivutano. Masuluhisho ya migogoro yanatakiwa kupatikana. Mfano, jambazi kuu hukamatwa mwisho wa igizo.
5. Kuweka mpangilio wa maonyesho
Mtunzi atumie mpangilio mzuri ambao utasaidia wasomaji waweze kuelewa kazi yake.
6. Kubuni wahusika
Mwandishi anashauriwa kubuni wahusika wenye sifa tofauti: wanene, weupe, weusi, warefu, wafupi n.k pia, wahusika hawa wawe na uhalisia na wahusika halisi waliopo katika jamii.

Mfano wa igizo

Bodaboda: Habari yako dada. (Akisimamisha pikipiki yake.)
Msichana: Nzuri, shikamoo!
Bodaboda: Aaaah, usinizeeshe binti, vipi, panda nikupeleke, mtoto mzuri kama malaika, haifai kutembea kwa mguu.
Msichana: Sitaki, niache nisome, ukiendelea kunifuata nakupigia kelele za mwizi.
Bodaboda: tobaa! Yamekuwa hayo tena. (Anawasha pikipiki yake na kuondoka.)

Maswali

1. Eleza kanuni muhimu za kutunga mashairi.
2. Tunga shairi la kimapokeo lenye beti nne kuhusu mada isemayo, ‘Siku ya mnada.’
3. Ngonjera ni nini?
4. Fafanua kanuni za kutunga ngonjera.
5. Tunga ngonjera juu ya mada yoyote.
6. Ni mambo gani anapaswa kuyazingatia mtunzi wa maigizo?
7. Tunga mchezo wa kuigiza kuhusu simba aliyevamia kijiji chako.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024