Sifa Bainifu za Irabu ya Kiswahili Sanifu
Irabu
ni aina ya vitamkwa ambavyo hutolewa pasi, bila kuwepo kizuizi chochote katika
mkondohewa au hewa itokayo mapafuni ikipitia katika chemba ya kinywa au ya pua
iwapo irabu hiyo itasilimishwa. Irabu ziko za aina nyingi lakini tutatumia zaidi
irabu za lugha ya Kiswahili. Katika kuainisha sifa za irabu ni lazima
kuzingatia lugha ambamo irabu hizo zinatumika, kwa sababu kila lugha huchagua
idadi ya irabu kadhaa kutoka katika bohari la sauti kwa kuzingatia irabu msingi
ambacho ndicho msingi wa irabu za lugha mbalimbali.
Kuhusu
lugha za Kibantu kuna irabu kuu tano ambazo hutumika karibu katika lugha nyingi
za Kibantu na lugha ya Kiswahili ikiwemo kama asemavyo Massamba na wenzake
(2004). Irabu hizo huwakilishwa kiimaandishi kama ifuatavyo.
Maandishi
ya kawaida Maandishi ya kifonetiki
a) i [i] mfano katika neno lia,
pi ka
b) e [ε] mfano katika neno cheka
c) a [a] mfano katika neno kale
d) o [ɔ] mfano katika neno pokea,bomani
e) u [u] mfano katika neno tume
Zifuatazo ni sifa bainifu za irabu ya Kiswahili sanifu:
Kigezo
cha kwanza ni sehemu ya ulimi inayohusika na utamkaji wakati wa kutamka irabu
hizo. Ulimi umegawanyika katika sehemu kuu tatu; mbele ambayo inajumuisha ncha
ya ulimi, sehemu ya pili ni kati au bapa la ulimi, na sehemu ya tatu ni nyuma
au shina la ulimi. Katika sehemu hizi tunapata sauti irabu mbalimbali kama
ifuatavyo:
a)
Sehemu ya mbele ya ulimi hutumika katika utamkaji wa irabu za kibantu za [i] na
[ɛ], na irabu za lugha ya Kiingereza ambazo ni [i:], [e], [ɪ] na [æ]. Irabu
hizi hutamkiwa sehemu ya mbele ya ulimi. Irabu hizi zinajulikana kama irabu
mbele.
b)
Sehemu ya kati ya ulimi hutumika au huhusika katika utamkaji wa irabu ya
kibantu [a] ijulikanayo irabu kati, na
irabu za lugha ya lugha za Kiingereza ambazo ni
[ʌ], [ə] na [ɜ:] ambazo hujulikana kama irabu kati.
c)
Sehemu ya nyuma ya ulimi huhusika katika utamkaji wa irabu [ɔ] na [u] za
lugha za Kibantu, vile vile huhusika
katika utamkaji wa irabu za Kiingereza ambazo ni [ɑ:], [ɒ], [ɔ:], [ʊ] na [u:] zijulikanazo
kama irabu nyuma.
Kigezo
cha pili ni mwinuko wa ulimi ndani ya chemba ya kinywa. Kifonetiki ulimi
umegawanyika katika sehemu nne za miinuko ya ulimi. Miinuko hii ni mwinuko juu,
mwinuko nusu juu (juu kati), mwinuko nusu chini (chini kati) na mwinuko chini.
Katika miinuko hii sauti irabu huweza kuangukia ama kati ya mwinuko chini na
nusu chini (chini kati) au chini au juu au kati ya juu na na juu kati au
katikati ya juu kati na chini kati.
a)
Mwinuko juu – huu unahusisha utamkaji wa sauti irabu [i] na [u] za lugha
za Kibantu na za lugha ya Kiingereza
ambazo ni [i:] na [u:] zinazojulikana kama irabu juu.
b)
Mwinuko juu kati – katika utamkaji wa mwinuko huu sauti irabu huangukia eneo
lililoko kati ya juu na juu kati ambapo ulimi huinuka zaidi ya mwinuko juu kati
kidogo ambapo tunapata sauti [ɪ] na [ʊ] irabu hizi ziajulikana kama irabu juu
kidogo ya juu kati.Wakati sauti irabu za kibantu [ε] na [ɔ] hutamkiwa katika
mwinuko wa juu kati. Irabu hizi zinajulikana kama zenye sifa ya kati ya juu
kati na chini kati.
c)
Mwinuko chini kati – katika mwinuko huu sauti irabu za lugha za Kibantu
ambazo hutamkwa katika mwinuko huo ni
[e] na [o] na katika lugha ya Kiingereza
irabu hizi huangukia katikati ya mwinuko juu kati na chini kati. Irabu
hizo ni [e], [ɔ:], [ɜ:] na [ə] sauti hizi mwinuko wa ulimi si juu kati wala si
chini kati halisi bali uko kati ya juu kati na chini kati.
d)
Mwinuko chini – katika mwinuko huu irabu [a] ya lugha ya Kibantu hutamkiwa na
sauti [ɑ:] ya lugha ya Kiingereza hutamkiwa katika mwinuko huo. Lakini kuna
sauti irabu [æ] na [ɒ] za lugha ya Kiingereza hutamkiwa juu kidogo ya mwinuko
chini wakati irabu [ʌ] hutamkiwa kati ya mwinuko chini na chini kati (nusu
kati) , nayo ni irabu ya lugha ya Kiingereza.
Kigezo
cha tatu ni hali ya midomo wakati wa utamkaji wa irabu. Hapa hali ya midomo au
umbo la midomo huwa katika hali tatu, uviringo, msambao na utandazo au hali
ambayo si bainifu.
a)
Uviringo wa midomo, hali au umbo hili la midomo huhusu utamkaji wa sauti irabu
[ɔ] na [u] za lugha za Kibantu wakati huo huo huhusu utamkaji wa irabu [ɔ:], [ɒ],
[ʊ] na [u:] za lugha ya Kiingereza.
b)
Msambao wa midomo, hali au umbo hili la midomo huhusu utamkaji wa irabu [i] ya
lugha za Kibantu na irabu [i:], [ɪ] na [æ] za lugha ya Kiingereza. Midomo
inapokuwa imesambaa kama kwamba unataka kutabasamu basi sauti au irabu hizi
hutamkwa.
c)
Utandazo wa midomo, hali ya midomo inapokuwa si mviringo wala si msambao huitwa
hali ya midomo si bainifu au ya utandazo. Umbo hili la midomo huhusu utamkaji
au hupelekea kutamkwa kwa sauti irabu [a], [ɛ] na [e] za lugha za Kibantu
wakati huo huo irabu [e], [ɑ:], [ʌ], [ɜ:] na [ə] za lugha ya Kiingereza.
Mchoro huu unaonesha sifa za irabu ya
Kiswahili kwa kuzingatia sehemu ya ulimi wakati wa utamkaji na mwinuko wa ulimi
Mchoro huu unaonesha sifa za irabu kwa
kuzingatia mkao wa midomo
Hivyo
ndivyo vigezo vyote vya msingi katika kubainisha sifa pambanuzi za irabu
zinazozitofautisha irabu moja na irabu nyingine. Kwa mwanafunzi wa somo la
fonolojia na mwanaisimu wa lugha lazima azingatie vigezo hivi, vipo katika
upambanuzi wa sifa bainifu za irabu.
Marejeo
Makoba,
D. (2017). Faida za Matumizi ya Alama za
Kifonetiki. Imepatikana https://www.mwalimumakoba.co.tz/2017/09/faida-za-matumizi-ya-alama-za-kifonetiki.html
Clements,
G.N (1983) CV Phonology: Generative Theory of the Syllable. MIT
Press, Combridge Mar
Jones,
D (1918) An Outline of English Phonetics. New Delhi, Kalyani
Publishers.
Katamba
, F (1986) An Introduction to
Phonology. New York, Longman Publishers
Kennedy,
M. S (1967) Perception of the Speech Code. University of Toronto
Press.
Kihore,
Y.M, Massamba , D.P.B na Msanjila, Y.P (2003) Sarufi Maumbo ya Kiswahili
Sanifu. Sekondari na Vyuo. Dar es salaam. TUKI
Massamba,
D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2004) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu.
Sekondari naVyuo. Dar es salaam. TUKI
Mgullu,
R. S (1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili.
Nairobi. Longhorn Publishers