Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Pili
Simba
mzee alianza unyama wake kwa kumuua mzee maarufu wa kijiji aliyependwa na watu
wote. Inasemekana kuwa mzee alikuwa katika shamba lake akipalilia mahindi,
ndipo alipovamiwa na simba mzee ambaye alimrukia shingoni na kumuua kisha
akamla mpaka aliposhiba na kuacha sehemu ndogo ya mwili.
Simba
mzee hakuishia hapo, aliwatafuna watoto wawili mapacha waliokuwa wakichoma
viazi pembezoni mwa nyumba yao. Basi baada ya tukio hilo, habari ya simba huyo
ikaenea kwa wanakijiji na kila mmoja akajifungia katika nyumba yake akiogopa
kutoka kwa hofu ya yule simba mzee.
Kwa
kuwa wanakijiji walijifungia ndani, simba yule mzee alipohisi njaa, akawinda
watu asiwaone, akaanzisha kioja kipya, alianza kubomoa nyumba za watu na
kuwatafuna wote aliowakuta humo.
Tukio
la kwanza alivunja nyumba ya mganga wa kijiji, mganga alijifungia ndani kwake
yeye na wanae, nao wakawa wamewasha moto ili waweze kuonana usiku ule, simba
alivunja mlango wao, akaingia na kuwatafuna wote, hata mganga alitafunwa, kweli
mganga hajigangi!
Nyumba
ya pili ilikuwa ni nyumba ya mpiga ngoma wa kijiji, tukio hili husikitisha
sana, kwani mpiga ngoma alikuwa na mke wake, mtoto wake mmoja wa kiume mwenye
mwaka mmoja na mama yake mzazi, wote wakatafunwa na simba yule.
Wanakijiji
waligundua kuwa, milango yao haikuwa imara kuweza kumzuia simba kuingia
atakapo, lakini hawakuwa na namna yoyote ya kufanya, isipokuwa kukaa hivyo wakiomba
miungu wasije uawa na Simba mzee. Pia walitamani kupeleka taarifa kwa mkuu wa
wilaya ili atume jeshi lije kumwondoa Simba yule, lakini hakupatikana mwanamume
aliyeweza kutoka ndani ya nyumba yake kwa hofu ya yule Simba. Basi kijiji
kikawa kimya kama hakina watu. Inasemekana kwa sababu ya ule ukimya, hata hatua
za sisimizi ziliweza kusikika!
Bwana
Mako aliishi katika kijiji hicho, nyumba yake ilijitenga na nyumba za
wanakijiji wengine, aliijenga katika kilima. Ungeziona, ungezani nyumba yake ni
askari mkuu na zile zingine ni askari wadogo nao wanaamrishwa mguu pande mguu
sawa!
Bwana
Mako alishtushwa na ukimya wa kijiji, mwanzo alidhani labda shughuli
zimewachosha hivyo kwa sababu ya uchovu hawana nguvu ya kupiga kelele.
Lakini
baada ya siku kadhaa akahisi hatari, akaamua kuteremka kilimani ilipokuwa
nyumba yake na kwenda kwa wanakijiji wengine.
Alitembea
katika hali ile ya ukimya mpaka alipozifikia nyumba za wanakijiji wengine.
“Wanakijiji
kulikoni, mbona kimya na mmejifungia ndani ya nyumba zenu?” aliuliza. “Tatizo
nini ndugu zangu?”
Hakuna
aliyejibu, wanakijiji walikaa kimya kwa hofu, pengine walidhani simba yule
angetokea na kummeza Bwana Mako mara moja. Naye Bwana Mako kuona watu wako
kimya, aliamua kusogea katika dirisha la fundi cherehani wa kijiji.
“Fundi,
fundi,” alinong’ona. “Nieleze, tatizo nini?”
“Simba
ndugu yangu,” alijibu, “anatafuna watu kama atafunavyo swala.”
Bwana Mako alipopata taarifa hizo, alisogea katikati ya nyumba zote.