Dhima Tano za Mofimu KI Katika Lugha ya Kiswahili
Siku
zote ambazo nilisimamia mitihani ya taifa, nilisimamia wanafunzi waliokuwa
shule. Sikuwahi kusimamia wanafunzi wa kujitegemea mpaka ilipowadia mwaka
fulani ambapo nilipangwa kwenda kusimamia mtihani wa taifa katika shule fulani
ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Muda
ulipowadia, nilifika katika kituo changu, baada ya kufuata taratibu zote,
nilisimama pembezoni ya mti ili niweze kuwaona wanafunzi waliokuwa wakifika
shuleni hapo tayari kufanya mtihani.
Alipita
binti mmoja mrembo sana ambaye naye alikuwa miongoni mwa wale wanaofanya
mtihani, kwa sababu ya urembo wake, nilikosa nguvu za kusimama na isingekuwa
kuushikilia ule mti, ningedondoka! Hata hivyo, nilikaa katika hali ya kuhisi
kizunguzungu kwa muda wa dakika tano, hali ilipokuwa shwari, nikaelekea
darasani ambako ndipo mtihani ulikuwa ukifanyika.
Niliingia
darasani, mimi na mwenzangu mmoja tuliyekuwa tunasimamia pamoja, tulitimiza
taratibu zote na mtihani ulianza. Katika chumba hiki cha mtihani, yule binti
mrembo sana, alikuwamo na alikaa siti za katikati.
Wakati
mtihani ukiendelea, nilitembea hapa na pale, nikipiga jicho huku na kule ili
kuhakikisha mtihani unafanyika kwa kufuata sheria hizi na zile.
Katika
hali isiyo ya kawaida, yule binti mrembo sana, mara baada ya kukaribia
alipokaa, alificha kitu kwa haraka, nami nilisogea kwa kasi ileile aliyotumia
kuficha kile kitu, nikafunua karatasi yake na kuona karatasi moja ndefu
isiyokuwa sehemu ya mtihani ambayo iliandikwa baadhi ya mada za somo la Kiswahili.
“Nisamehe
mwalimu…nitakupa chochote unachotaka,” alinong’ona mrembo akiwa amesogeza mdomo
wake karibu na sikio langu. Nikatabasamu kama kitoto cha mamba, kisha nikalamba
midomo hata ungedhani ni mwanamziki anahojiwa. Hoja ya kupewa chochote
ilinifurahisha na kunipa matumaini mapya. Hata hivyo, haikutosha kunitoa katika
misingi.
Niliichukua
karatasi yake ya mtihani na ile ya kujibia, nikaandika vitu fulani, alipoona
nilichoandika, machozi yalimbubujika na matone saba yalidondoka haraka, tone la
nane nililidaka, kisha nikamwambia, “Simama juu, nisubiri pale nje.”
Mimi
na wasimamizi wenzangu tulifanya taratibu zote zinazohusu mwanafunzi aliyevunja
sheria za mtihani, ili kubaki na kumbukumbu, nikapiga picha upande mmoja wa
majibu aliyoingia nayo yule mrembo, na majibu hayo yalisomeka hivi:
Dhima za Mofimu KI
“Taja
dhima tano za mofimu ‘KI’ katika sarufi kisha tunga sentensi mbili kwa kila
dhima.”
1.
Hutumika
kudogesha
Mifano:
Kitoto kinacheza mpira.
Kimeza
kimesombwa na mafuriko.
2.
Huonyesha
idadi
Mifano:
Kijiji kimependezeshwa na bustani za matunda.
Kitabu
hiki kinakurasa nne pekee.
3.
Huonyesha
upatanishi wa kisarufi
Mifano:
Kiatu kimechakaa kama mvaaji wake.
Kiti
kimepatikana mtoni.
4.
Kuonyesha
mtendwa katika tungo
Anachokipenda
kimependwa na wenye nguvu.
Anachokitafuna
hana uwezo wa kukimeza.
5.
Kuonyesha
kuendelea kwa tendo
Nilipofika
kwao alikuwa akicheza.
Alikuwa
akisakata dansa bila hofu ya wakwe.