Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nne
Haikupita
muda, Mako aliletwa kwa mfalme akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wapandao
punda. Alishushwa, naye kwa heshima akapiga mguu wa kuume mara tatu kumsalimu
mfalme. Mfalme hakujibu salamu hiyo. alimtazama kwa ghadhabu Mako.
Baraza
lilikaa ili kusikiliza mashtaka. Mako alivalia shati kubwa la buluu, suruali
pana kiasi na viatu imara vya ngozi. Jamii ya Kanakantale, haikuwa nyuma katika
teknolojia ya mavazi, watu wake walivaa mavazi ya kisasa!
Mfalme
alianza kusoma mashtaka, “Mako, mkulima, mfugaji na muwindaji, unatuhumiwa kwa
kosa la kujihusisha na mahusiano na mke wa mfalme, yaani Malkia wa nchi ya
Kanakantale. Usiku tukiwa tumelala, nilisikia kwa masikio yangu Malkia akitamka
kuwa anakupenda na anaahidi kuwa wako daima. Japo Malkia alikuwa ndotoni,
haimaanishi kuwa huna mahusiano naye. Kinachotokea ndotoni ni matokeo ya
kilichotendeka mchana. Una chochote cha kujitetea?”
“Mfalme
wangu,” alijibu Mako, “nimekosa nini hata niwe na mahusiano na Malkia wa nchi
yangu? Naruhusiwa kuoa wanawake wengi kadri ya uwezo wangu vipi niwe na Malkia.
Tazama nchi hii ilivyojaa wanawake, wote hawa sijawaona hata nikaja kwa Malkia
wangu mwenyewe? Mfalme tuhuma hizi siyo za kweli. Siwezi kufanya hivyo.”
Baada
ya utetezi wa Mako, mfalme alikaa na baraza lake, wakajadili kwa muda. Wazee
wale wenye ndevu nyeupe, walikubaliana jambo, mfalme akasoma hukumu.
“Tumekubaliana
kuwa, Mako una hatia ya kuwa na mahusiano na Malkia. Ushahidi upo katika ndoto
ya Malkia. Jambo hili ni kosa baya kabisa tena lisilokubalika. Hivyo,
unahukumiwa adhabu ya kifo. Utakaa gerezani kwa muda wa mvua mbili, kisha
utanyongwa hadharani iwe fundisho kwa wengine. Kwa kipindi chote hicho, hakuna
anayeruhusiwa kuja kukuona ila kwa idhini ya mfalme.”
Mako
hakuamini maneno yale. Aliinamisha kichwa chake hata mikono ikagusa zile nywele
za kipilipili. Alishangazwa na hukumu ile ambayo haikutenda haki. Kukaa
gerezani kwa muda wa mvua mbili maana yake ni kwamba, angekaa gerezani mpaka
pale mvua ingenyesha kwa mara ya kwanza, kisha kwa mara ya pili, baada ya hapo
angenyongwa.
Habari
ya hukumu ya kifo cha Mako ilisambaa kama mchanga jangwani. Habari hii
iliwaumiza sana wananchi wa kawaida. Mako alikuwa msaada mkubwa kwao. Hukumu
hii iliumiza familia ya Mako na wote waliompenda kwa ule moyo wake wa kusaidia.
Pengine habari hii ilimfurahisha mfalme peke yake kwa maana hakuna mwingine
aliyefurahishwa na hukumu hii ya ajabu.
Wananchi
walionekana kutoridhishwa na hukumu hii, waliwaza, kama kweli Mako ana
mahusiano na Malkia, iweje basi ahukumiwe Mako peke yake naye Malkia aachwe?
Mchana
wa siku hiyo Mako alitupwa gerezani akiwa kavikwa mavazi meupe. Gereza lilikuwa
kubwa lililojengwa kwa miti ya mkonge. Liligawanywa katika vyumba vya watu
wanne. Wafungwa hawakuruhusiwa kutoka katika vyumba isipokuwa mara moja kwa
siku pale walipotakiwa kwenda kufanya usafi wa miili yao.
Mako aliwekwa chumba kimoja na wenzake watatu,
yeye akawa wa nne. Wote hao walisubiri hukumu ya kifo kwa makosa mbalimbali
waliyofanya.
Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tano