Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tano
Aliweza
kuwatambua watu hao. Mmoja aliitwa Sasi, kosa lake Wizi. Wala hakusingiziwa.
Sasi alikuwa mwizi aliyechukiwa na watu wote. Wa pili alikuwa Athu, yeye
alifungwa kwa kosa la uharifu kama Sasi. Naye hakusingiziwa, alikuwa mwizi wa
mifugo aliyechukiwa na wafugaji wote. Wa tatu aliitwa Sipe, alifungwa kwa hofu
ya mfalme. Mfalme alimuogopa Sipe kuwa ipo siku angempindua. Sipe alikuwa mtu
mwenye maneno ya busara. Mara chache alitabiri mambo yakatokea, hii ilimpa hofu
mfalme kwa kuona Sipe atapendwa na watu kuliko yeye na kuleta mapinduzi. Sipe
alionewa!
“Hamjambo
ndugu zangu?” Alisalimia Mako.
“Hatujambo,”
walijibu. Sipe akaendelea, “Hakuna aliyesalama, hata wewe Mako umeletwa humu?
Umefanya kosa gani hasa?”
“Ni
uonevu tu,” alijibu Mako, akikaa katika kitanda cha majani, “nina mvua mbili za
kunifanya niendelee kuwa hai. Nimehukumiwa kunyongwa kwa kosa la kuonekana
katika ndoto ya malkia. Malkia kaota kwa sauti akisema ananipenda na hawezi
kuniacha milele!”
Wote
walicheka, lakini kicheko cha huruma. Hawakuwahi kusikia hukumu ya
kustaajabisha kama hii.
Katika
hali isiyotarajiwa, mvua kubwa ilinyesha, simanzi ikawakumba wafungwa wale
wanne. Ilibaki mvua moja tu, Mako anyongwe!
Japo
Mako ni jasiri, kunyesha kwa mvua kulimtetemesha na kumkata maini. Alikiweka
kichwa chake katikati ya magoti, asiyeamini hukumu hiyo ya aina yake.
Hata
usingizi ulipotaka kumchukua, ulishindwa na hata ulipomchukua, aliota ndoto
mbaya akaamka haraka. Baridi ilikuwa kali, lakini kijasho kilimtoka.
Kwa
mbali kupitia dirishani, malkia wa nchi ya Kanakantale alionekana akibishana na
mfalme. Malkia alivaa vazi refu, pana, jeupe aliloliburuza atembeapo. Mfalme
alivaa suruali nyeusi na shati jeupe.
“Umemhukumu
kumfunga mtu asiye na hatia, mbaya zaidi anatakiwa kunyongwa… haki iko wapi?”
alilalamika Malkia.
“Mimi
ndiyo mfalme, wewe ni mwanamke tu. Huna haki ya kuhoji maamuzi haya yametoka
wapi? Nchi nzima haithubutu kunihoji utaweza wewe?”
“Hata
kama. Hukutakiwa kutoa hukumu ya kifo kwa mtu asiye na hatia. Kumbuka mtu huyu
ana familia inayomtegemea. Ana ndugu na jamaa wanaompenda, pia, hukumu hii
inawafikirisha watu kama wana mfalme anayejielewa sawasawa…”
Mfalme
aliyechoka kubishana, akamchapa kofi kali malkia na kuacha alama ya vidole
vitano vionekane katika mashavu laini ya mke huyu wa mfalme. Malkia akalia kwa
uchungu lakini walinzi hawakuweza kumsaidia kwa sababu aliyempiga kofi ni
mfalme!
Kuona
hivyo, akatoka na kuelekea katika chumba cha wale dada wa kazi wanne, dada hawa
wamekuwa wasaidizi wake wa muda mrefu nao hukaa chumba kimoja kikubwa katika
kona ya kulia ya Kasri la mfalme wa Kanakantale.
Malkia aliingia humo akibubujikwa na machozi, wasaidizi wakampokea na kumkarisha katika kitanda kikubwa cha manyoya.