Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tatu

 

Taji la mfalme

“Ndugu zangu,” alisema kwa sauti kubwa, “Wanaume msijifungie ndani, njooni nje twende tukapambane na huyu Simba. Mkiendelea kubaki ndani hakuna atakayesalia kwa sababu milango yetu siyo imara kiasi cha kumzuia asiivunje. Ni heri tufe tukipigana naye kuliko tujifungie ndani naye aje atukamate kama mwewe akamatavyo vifaranga. Je mnavyakula vya kutosha siku ngapi? Sasa hamuoni mnawindwa na njaa pamoja na simba? Aliyetayari kupambana ajitokeze sasa.”

Zilipita dakika tisa tangu azungumze maneno hayo. Hakuna mwanamume aliyetoka ndani kuja nje kuungana naye, Bwana Mako akaamua kuingia msituni peke yake kumsaka Simba mzee. Akiwa anatembea alirushiwa mkuki.

“Chukua mkuki huo utakusaidia kupambana na simba huyo,” ilisema sauti kutoka nyumba moja, kisha ikasikika sauti ya kufunga mlango, pakawa kimya.

“Ni uonevu kumuua simba mzee kwa mkuki, simba mzee anauliwa kwa viganja vitupu!” alijibu Bwana Mako kisha akapotelea msituni.

Wanakijiji walichungulia katika madirisha yao kama wanaoangalia sinema. Ukimya ukatanda tena kwa dakika ishirini.

Ukimya ulivunjwa na miungurumo ya simba, wanakijiji walitazama lakini hawakumuona simba waliishia kusikia ile miungurumo yake tu. Baadaye ikasikika sauti ya Bwana Mako akilia kisha pakawa kimya. Kimya kuliko muda wote.

Baadaye vilianza kusikia vishindo vikija katika kijiji. Hofu ikawajaa, wakasali kila mtu kwa imani yake wasijetafunwa na yule simba.

Vishindo viliendelea kusikika mpaka walipoona kitu ambacho hawakuamini. Bwana Mako alibeba mwili wa Simba yule mzee katika mabega yake. Naye alitembea kwa vishindo vya shujaa.

Furaha ilirejea tena kijijini, wanakijiji walifungua milango yao wakampokea Bwana Mako na kumshukuru kwa msaada wake. Baada ya kumaliza maombolezo ya ndugu zao waliotafunwa na Simba yule, walifanya sherehe kubwa kufurahia ushindi wa Bwana Mako.”

Dada wa kazi alimaliza kusimulia mkasa wa Mako. Hata akina dada wengine nao wakavutiwa na Mako lakini waliogopa kuonesha waziwazi kwa sababu walitambua kuwa malkia alikwisha mpenda.

***

Ilikuwa usiku wa manane katika jumba la kifalme. Malkia alilala na alizama katika usingizi. Mfalme wa Kanakantale yeye hakulala. Suala la utawala ni gumu na kuna mambo ambayo yamekuwa yakimnyima usingizi, basi akiwa kimya, alisikia malkia akiota kwa sauti.

“Mako nakupenda, naahidi kuwa wako daima, njoo unikumbatie Mako wangu.”

Mfalme aliyasikia maneno hayo, pia alibaini ilikuwa ndoto tu, hata hivyo Mako alimfahamu, alimfahamu kwa sababu ya mikasa yake ya kila siku. Kilichomtesa mfalme ni hilo jina Mako limeingiaje katika ndoto ya Malkia.

Mfalme aliamua kumuamsha Malkia na kumuuliza juu ya ndoto yake. Malkia hakuonekana kukumbuka kitu. Mfalme alisimulia ilivyokuwa, pia alimueleza Malkia kuwa, ndoto ni matokeo ya mawazo yako ya siku nzima.

Malkia alijitetea kwa kueleza tukio lake la kukutana na Mako, alisema alikutana na mtu huyo mchana wa siku hiyo na hakuna kingine kilichoendelea.

Japo Mfalme hakuendelea kujibishana na Malkia, hakulizishwa na utetezi. Asubuhi aliamuru askari wamtafute popote alipokuwa Mako, wampeleke kwake tayari kujibu mashtaka.

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nne

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1