Njia Nne Zitumikazo Kuunda Misimu ya Lugha ya Kiswahili
Niliketi katika kiti kirefu
nikinywa kinywaji ambacho siwezi kukitaja. Katika kiota nilichokuwamo, mhudumu
alikaa mbele yangu sehemu iitwayo ‘kaunta’ nasi tulitenganishwa na dirisha
kubwa lililokuwa na nondo pana.
“Mwanaidi ongeza kinywaji,”
nilisema kwa sauti kali, nilijiamini kwa sababu katika kiota hiki, tulikuwa
wawili tu, mimi na Mwanaidi. Kiota cha Mwanaidi hakina wateja wengi na leo
nilikuwa peke yangu.
Aliongeza kinywaji kama
nilivyotaka, kisha akabadili wimbo na kuweka dansa moja matata. Nilitaka
kuinuka ili nisakate dansa, lakini nikajizuia baada ya kukumbuka kuwa mimi ni
mwalimu, tena siyo mwalimu wa kawaida, ni mwalimu wa walimu na wanafunzi. Basi
nikakaa tuli nikitikisa kichwa na mabega.
Lakini ghafla tukavamiwa na
watu watatu. Watu hawa walivaa sare za jeshi la polisi. Bila shaka, walikuwa
polisi.
“Kwa nini unafungua biashara
yako mpaka saa saba usiku tena ukipiga mziki kwa sauti ya juu?” aliuliza askari
aliyekuwa na mbavu nene kuliko wenzake. Mwanaidi hakuwa na cha kujibu. Askari
akanigeukia mimi.
“Na wewe ndiyo mteja wake, leo
mnaenda kurara polisi. Haya ndiyo majambazi afande!”
“Mimi siyo jambazi afande,
mimi ni mwalimu,” nilijitetea.
“Mwalimu wa somo gani?” askari
aliyekuwa kimya muda wote aliuliza.
“Kiswahili na masomo mengine
ya sanaa,” nilijibu. Baada ya jibu hilo, alisogea karibu yangu zaidi kisha
akaniuliza swali lililonifanya nikaandika habari hii.
“Unaelewa nini kuhusu neno
misimu? Kwa kutumia mifano, fafanua njia nne zitumikazo kuunda misimu ya lugha
ya Kiswahili.”
Bila kupepesa macho, nilimjibu
swali lake kwa hoja zifuatazo:
Njia Nne za Kuunda Misimu
Misimu ni semi za muda na
mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalumu. Njia nne
zitumikazo kuunda misimu ya lugha ya Kiswahili ni:
1.
Kufupisha
maneno
Mfano, neno refu kama
kompyuta, kufupishwa na kuwa komp.
2.
Kutohoa
Misimu huweza kuundwa kwa
kutohoa kutoka lugha za kigeni. Mfano, mother-maza.
3.
Kutumia
sitiari
Mfano, Golikipa-nyani. Mtu
mwenye nguvu-simba.
4.
Kutumia
tanakali
Mwigo wa sauti ya kitu,
hutumika kama jina la kitu hicho. Mfano, bunduki-mtutu.
Hizo ndizo njia zitumikazo
kuunda misimu ya lugha ya Kiswahili.
Baada ya majibu hayo, askari
walituacha lakini wakimshauri hasa Mwanaidi kuwa, atii sheria bila shuruti. Kila
ifikapo saa sita usiku, afunge kiota chake.