Mchango wa Sarufi Geuzi Zalishi Katika Uchambuzi wa Lugha

Barafu Ikigeuka


Kwa mujibu wa Matinde (2012), sarufi ni taaluma ya lugha inayochunguza na kuchanganua vipashio na kanuni mbalimbali zinazotawala muundo wa lugha. Maana hii inatazama muundo wa lugha pamoja na vipashio vyake ambayo vinaongozwa na kanuni mbalimbali ili kuweza kutupatia lugha.

Naye Kapinga (1983), anasema, sarufi ni utaratibu wa kanuni ambazo humwezesha mtumiaji wa lugha kutunga tungo sahihi zinazoeleweka mara zinapotamkwa. Maana hii inasisitiza kanuni ambazo humsaidia mzungumzaji wa lugha kutoa tungo sahihi zinazoeleweka pale zinapotamkwa. Wazungumzaji wa kawaida huwa hawazitambui kanuni hizo, lakini wanazo katika akili zao na huwasaidia kutoa tungo zinazoeleweka.

Hivyo basi, sarufi ni kanuni za lugha ambazo humsaidia mtumiaji wa lugha kutoa tungo zinazoeleweka. Kanuni hizi zinaweza kuwa zinafahamika kwa mzungumzaji, hasa mzungumzaji ambaye ana elimu ya sarufi, au hazifahamiki kwa mzungumzaji, hasa yule ambaye hana elimu ya sarufi.

Kwa upande wa sarufi geuzi, Matinde (2012), anasema, Ugeuzi ni utaratibu unaotumiwa kubadili umbo la tungo kuwa umbo jingine kwa kutumia kanuni maalumu. Kwa hiyo ugeuzaji ni mbinu ya kisarufi ambayo hutumiwa katika sarufi geuza maumbo zalishi kuzalisha sentensi lukuki kwa kufuata sheria mahususi. Kwa mujibu wa maana hii, safuri geuzi inasaidia lugha kujipatia sentensi nyingi zinazokidhi mawasiliano.

Wataalamu Habwe na Karanja (2007), wanasema, Sarufi geuzi hueleza ujuzi wa lugha ambao msemaji mzawa anao ujuzi anaomwezesha kutumia lugha. Maana hii inatupa wazo jipya kuwa, sarufi geuzi ndiyo humuwezesha mzawa kutumia lugha yake katika mazungumzo ya kila siku.

Kwa ujumla, Sarufi geuzi maumbo ni utaratibu wa kubadili maumbo kuwa maumbo mengi kwa kufuata kanuni maalumu. Sarufi geuzi maumbo huwawezesha watumiaji wa lugha kujitengenezea sentensi nyingi zinazokidhi mawasiliano na kutumia lugha katika mazungumzo ya kila siku.

Sarufi geuzi zalishi ina mchango mkubwa katika uchambuzi wa lugha ya Kiswahili kama inavyoelezwa:

Kwanza Sarufi Geuzi Zalishi inachanganua sentensi kwa kuzingatia umbo la nje na umbo la ndani katika sentensi. Katika nadharia hii sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linajitokeza katika usemaji na hata inapoandikwa na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na kujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea (maana). Sarufi Geuzi Zalishi imeweza kuonesha uhusiano wa tungo ambazo zina umbo la nje tofauti na umbo la ndani sawa.

Kwa mfano:

(a)Machibya anawasha simu.

(b)Simu inawashwa na Machibya.

Mfanano wa tungo hizi umekitwa katika maana japokuwa sentensi “a” inaanza na Makida na “b” inaanza na mpira na mtendwa katika sentensi zote ni yuleyule na imebeba maana ile ile. Mchakato wa kubadili umbo la nje la sentensi “a” na kuwa “b’ umesababisha uchopekwaji wa kiunganishi “na” na kiambishi tendwa “w” katika kitenzi “cheza” hivyo kanuni geuzi tendwa ndiyo iliyotumika kuingiza mabadiliko hayo.

Pili, Sarufi Miundo Geuzi Zalishi imeweza kueleza utata  wa sentensi kwa kuangalia maumbo yake ya ndani; hapa tunazungumaza utata wa  kimuundo na maneno.

Mifano:

(a)Wanaume na watoto ishirini walikuja

(b)Wanaume idadi haijulikani, na watoto ishirini walikuja

(c)Wanaume kumi na watoto kumi walikuja

Sentensi zote hizi zinaelezea maana halisi iliyo katika sentensi kuu . Inakua vigumu kwa anayesikia sentensi hiyo kujua  msemaji anamaanisha nini lakini katika sarufi miundo geuzi  zalishi wameweza kutuondolea utata katika maana za sentensi mbalimbali kwa kuonesha dhahiri hitaji la sentensi hiyo k wa msikiaji, ndio maana tukaweza  kupata aina hizo tatu za sentensi zenye maana sahihi isiyo tata.

Tatu, Sarufi Geuzi Zalishi wameweza kuonesha uhusiano uliopo baina ya sentensi zaidi ya moja zenye maumbo tofauti. Kwamba katika sarufi geuzi zalishi wameweza kubainisha kuwa sentensi zinaweza kuwa na maumbo tofauti lakini zikawa na maana moja .

Mifano:

(a) Malima amempiga Kingunge

(b) Kingunge amepigwa na Malima

Sentensi ya kwanza inasonesha kauli tendi na sentensi ya pili inaonesha kauli tendwa.Kuna  uhusiano mkubwa kati ya sentensi ya kwanza na sentensi ya pili na uhusiano huu umeweza kuoneshwa dhahiri na sarufi miundo geuzi zalishi. Kwamba sentensi ya kwanza mtenda ni Malima na mtendwa ni Kingunge , pia katika sentensi ya mtendwa na mtendwa na ni wale wale. Hivyo kilichobadilika hapo ni umbo la sentensi lakini maana ni ileile.

Nne, Sarufi Miundo Geuzi Zalishi wanaeleza na kuchanganua kinaganaga sentensi changamano; Hii ni kutoka na kuonesha vitenzi dhahiri katika sentensi changamano ambapo sarufi za nyuma zilishindwa kuonesha vitenzi hivyo na kuvifanya kama kishazi vumishi elezi .

Mifano:

(a) Mbuzi aliyepotea jana ameonekana asubuhi

(b) Kijana aliyekuja jana ameondoka leo

Katika sentensi hizi mbili maneno ‘aliyepotea ‘ na aliyekuja’ huonekana kama kitenzi, lakini katika sarufi za nyuma kabla ya sarufi miundo geuzi  zalishi maneno hayo yalionekana kama kishazi vumishi.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba, Sarufi Geuzi Zalishi ina mchango mkubwa katika uchambuzi wa lugha ya Kiswahili. Namna ambavyo Sarufi Geuzi Zalishi hucheza na maumbo ya lugha, husaidia sana kuzalishwa kwa sentensi zisizokuwa na ukomo na hivyo kuipa uhai lugha. Ni ukweli kwamba, Sarufi geuzi ilianzishwa kutokana na mapungufu katika sarufi muundo virai. Sarufi iliyokuwepo, sarufi miundo virai, ilishindwa kuonyesha mahusiano yaliyokuwepo baina ya sentinsi zinazo husiana kimaana. Hivyo kutokana na upungufu huo kulikuwa na haja ya kuonyesha uhusiano huo.

Marejeo

Kapinga, M.C. (1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Dar-es-Salaam: TUKI.

Massamba, D.T. Kihore, M.Y. & Hokororo. (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). Dar-es-Salaam: TUKI.

Matinde, S.R.(2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1