Utata Katika Uainishaji wa Tanzu za Fasihi
Fasihi
Simulizi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni: M.M. Mulokozi
(1996) anasema, Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na
kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
TUKI
(2004) wanasema, fasihi simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile;
hadithi, ngoma na vitendawili.
Balisidya
(1983) anasema, fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika
kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
Wanjara
(2011) anasema, fasihi simulizi ni sanaa ambayo vyezo kuu ya utunzi,
uwasilishaji na usambazaji wake ni sauti pamoja na vitendo. Fasihi simulizi ni
sanaa inayotumia mazunguzo na vitendo kisanii ili kuwasilisha maarifa au ujumbe
Fulani kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kwa
ujumla, fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutolewa kwa njia ya mdomo
kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Aina hii ya fasihi, huhifadhiwa kwa njia
ya kichwa, japo kutokana na mabadiliko ya teknolojia, uhifadhi wa asili umeanza
kuchukuluwa na vifaa kama: Kompyuta, vinasa sauti, kanda za video na intaneti.
Tanzu
za fasihi simulizi ni aina mbalimbali ya kazi za kifasihi simulizi. Tanzu za
fasihi simulizi zimeanishishwa na waandishi wengi kama tanzu hizo zilivyo
nyingi.
Miongoni
mwa waandishi walioanisha tanzu za fasihi simulizi ni pamoja na:
Mulokozi
ameanisha tanzu sita za fasihi simulizi kama ifuatavyo:
i. Mazungumzo
ii. Masimulizi
iii. Maigizo (drama)
iv. Ushairi
v. Semi
vi. Ngomezi (ngoma)
Mazungumzo
ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile.
Si kila mazungumzo ni fasihi mazungumzo ili yawe fasihi lazima yawe na usanii
wa aina fulani na uhalisia baada ya kuunakili. Mfano, tanzu zinazoingia katika
fungu la mazungumzo ni kama hotuba, malumbano ya watani, ulumbu, soga na
mawaidha.
Masimulizi
ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Mulokozi (1989) anasema, kuwa
masimulizi ni fasihi ya kihadithi na fani zake huwa na sifa kama kuelezea tukio
katika mpangilio Fulani mahususi, huwa na wahusika yani watendaji. Katika
Mulika 21 Mulokozi amegawanya fasihi simulizi katika tanzu zifuatazo za
kihadithi ambazo ni; ngano, visakale, tarihi, istiara, mbazi na kisa.
Semi
ni tungo au kauli fupifupi zenye kubeba maana Fulani au mafunzo muhumu katika
jamii, Mulokozi ameanisha tanzu semi kama ifuatavyo; methali, mafumbo, vitendawili.
Ushairi
ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa
na vina ushairi una ufasaha wa maneno au muktasari wa mawazo na maono ya
ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu. Ushairi hupambanuliwa na lugha ya
kawaida kwa kutumia lugha na mbinu za kimuktadha. Mulukozi (1989), amegawa
ushairi katika mafungu mawili ambayo ni nyimbo na uwasilishaji.
Maigizo
(drama) ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia au matendo ya watu na viumbe
wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani. Maigizo ni sanaa inayopatikana
katika makabila mengi. Mulokozi anasema drama (maigizo) ya kiafrika huambatana na
ngoma mtambaji wa hadithi au matendo ya kimila.
Ngomezi
ni midundo Fulani wa ngoma kuwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila hilo
mara nyingi kauli hizo huwa ni za kishairi au kimafumbo.
Mtaalamu
mwingine aliyeainisha tofauti na uainishaji wa Mulokozi ni Wanjara (2011)
ambaye anaainisha tanzu mbalimbali za fasihi simulizi ambazo ni zifuatazo:
i. Hadithi za kihistoria
ii. Hadithi za kubuni
iii. Ushairi (nyimbo)
iv. Semi
v. Maigizo
vi. Mazungumzo
vii. Ngomezi.
Wataalamu
wengine ni Ndungo na Wangali, wao wanaziainisha tanzu tano za fasihi simulizi
wanaanza na:
i. Hadithi
ii. Ushairi na nyimbo
iii. Sanaa za maonyesho
iv. Methali
v. Vitendawili.
Nao
wataalamu Njogu na Chimera (1999) wanaainisha tanzu zifuatazo:
i. Hadithi
ii. Nyimbo
iii. Methali
iv. Vitendawili
Hivyo
basi, kuna utata mkubwa unaojitokeza katika uainishaji wa tanzu za fasihi
simulizi. Maelezo haya, yanaeleza sababu za utata wa uainishaji wa tanzu za
fasihi simulizi:
Sababu
ya kwanza inasababishwa na wataalamu wenyewe. Kila mtaalamu ameainisha ajuavyo
tanzu za fasihi simulizi. Kwa mfano, Mulokozi anataja: mazungumzo, masimulizi,
maigizo, ushairi, semi na ngomezi. Wanjara anaongeza kitu kipya ambacho ni
hadithi za kihistoria. Ndungo na wangali hawaonekani kuzikubali semi zote, wao
wanataja methali na vitendawili pekee. Nao Njongu na Chimera hawaonekani
kuyatambua maigizo kama utanzu wa fasihi, wao wanataja hadithi, nyimbo, methali
na vitendawili. Hivyo, mtazamo wa wataalamu na namna wanavyoainisha tanzu za fasihi
simulizi unasababisha utata kwani tanzu zao hazifanani.
Pia,
Utata unatokea kutokana na kutofautiana kwa vigezo vinavyotumiwa na wataalamu
mbalimbali katika ugawaji huu, kwani kila mtaalamu hutumia vigezo vyake
kulingana na matakwa ama mtazamo wake. Kukosekana kwa kigezo maalumu kilichokamilika
cha uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi ni chanzo kingine cha utata. Hakuna
kigezo kimoja kilichokamilika ambacho kingeweza kutumiwa na waandishi ili
kuainisha tanzu za fasihi simulizi. Sababu hiyo imepelekea kila mwandishi
kutumia kigezo na msingi anaoufahamu yeye na hii kusababisha utata. Hii ndiyo
sababu, japo wataalamu wanazungumzia tanzu za fasihi simulizi, kila mmoja ana
tanzu zake kulingana na msimamo wake.
Utata
mwingine unasababishwa na fasihi kubadilikabadilika katika fani. Fasihi
Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea
muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika
masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili
linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu
zinazoingiliana.
Sababu
nyingine ya utata ni wataalamu kutumia vigezo vyenye mapungufu. Vipo vigezo
ambavyo vina mapungufu makubwa na ni vigumu kuainisha tanzu fulani bila
kusababisha utata. Kwa mfano, kigezo cha unguli (protagonist of the tale),
katika kigezo hiki kunajitokeza ngano zihusuzo wanadamu, ngano za wanyama,
ngano za vichimbakazi, na ngano za miungu. Hata hivyo kigezo hiki kinaonyesha
kuwa na matatizo makubwa yanayoendelea kusababisha utata.
Sababu
nyingine ya utata ni uchanga wa fasihi simulizi. Fasihi simulizi ni change siyo
kwa sababu imeanza miaka ya hivi karibuni, ni change kwa sababu kusomwa kama
taaluma imeanza miaka ya hivi karibuni. Hivyo basi, tafiti nyingi hazijafanywa
jambo ambalo linasababisha utata. Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini
kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni sababu
inayopelekea utata.
Kukosekana
vitabu vilivyoandika kwa undani kuhusu fasihi simulizi kumesababisha utata
katika uanishaji wa vipera vyake. kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi
Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in
Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa
tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule
za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987) Mulika
namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na
wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili
lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu
tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi. Hivyo
basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za
Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo
mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa
vinavyotumika na namna ya uimbaji.
Hivyo
basi, utata katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi unasababishwa hasa na
uchanga wa taaluma ya fasihi simulizi na changamoto zingine kama kukosekana kwa
kigezo kilichokamilika. Katika lugha, kutofautiana kwa wataalamu si jambo baya,
ni mwanzo mwema wa kukubaliana na kukua kwa taaluma. Wataalamu wasichoke
kuchunguza na kuja na kigezo kimoja ambacho kitatoa tanzu zinazokubalika na
kukosa utofauti. Hata hivyo, Mulokozi anaonekana kukubalika zaidi katika tanzu
alizoainisha. Pamoja na kukubalika, tanzu zake zina mapungufu mengi kama
mapungufu yanayoonekana kwa wataalamu wengine.
MAREJEO
Mulokozi,
M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi
Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
Mulokozi,
M.M. (1989). Tanzu za fasihi simulizi. Mulika. 21:1-24. Dar-es-salaam.
TUKI,
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo
la Pili). East Africa: Oxford University Press
na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).
Wamitila,
K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.
Wamitila,
K W (2003), Kichocheo cha fasihi simulizi: Focus Publications Ltd. Nairobi