Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nane
Siku
mpya ilifika, Bwana Mako na watoto wa Jitu walikuwa wa kwanza kuamka, na tazama
akishirikiana na watoto wa Jitu, alikuwa ametengeneza meza kubwa ambayo ilikuwa
na kimo sawa na tumbo la majitu. Baada ya kukamilika kwa meza, akashirikiana na
watoto kuipeleka nyuma ya nyumba ambako kulikuwa na ukumbi mkubwa, kisha
akawaamuru watoto wakamuite baba yao.
“Niliahidi
kukufanya tajiri.” alisema Bwana Mako baada ya Jitu kufika.
“Na
hii meza ndiyo utajiri wenyewe?” Jitu liliuliza.
“Ndiyo,
meza hii ndiyo utajiri wenyewe, lakini haiwezi kuwa utajiri bila mimi niliyekaa
juu yake.”
“Sikuelewi
unanichanganya!” lililalamika Jitu.
“Sikiliza
rafiki mwema,” alisisitiza Bwana Mako, “watume wanao waende mjini, wawatangazie
watu maneno haya: Nyumbani kwa baba yetu, kuna maonyesho hayajawahi kutokea.
Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia, amemtembelea baba yetu, ajabu ni
kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani, huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama
kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa
kiingilio cha pesa mbili tu.”
Jitu
lilimwelewa Bwana Mako na liliona ubora wa wazo hilo hata likastaajabu sana
uwezo wa akili ya mwanadamu kutoka Duniani.
Basi
watoto wa jitu walitembea mjini wakitangaza, “Nyumbani kwa baba yetu, kuna
maonyesho hayajawahi kutokea. Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia,
amemtembelea baba yetu, ajabu ni kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani,
huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo
ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa kiingilio cha pesa mbili tu.”
Kufumba
na kufumbua, majitu mengi yalijaa nyumbani kwa Jitu, yote yalitaka kumuona
kiumbe kutoka duniani na yalilipa kiingilio cha pesa mbili. Yalipelekwa mpaka
katika meza aliyosimama Bwana Mako. Kwa sababu yalikuwa mengi, basi
yaligawanywa katika makundi ili yaweze kumuona kwa zamu.
Bwana
Mako alifanya michezo ya kufurahisha, kwanza alianza kwa kupiga danadana mpira,
majitu yakashangaa. Kisha akacheza mziki, halafu akaruka sarakasi, sarakasi
zenyewe hazikuwa sarakasi bali zilikuwa zile za upande upande, ni ushamba tu wa
majitu kushangaa sarakasi hizo. Ama naweza kusema, burudani haswaa ilikuwa ni
ule udogo wa Bwana Mako katika macho ya majitu. Alitaka kufanya mchezo wa
ngumi, lakini alihofia labda majitu yanaweza kuiga na kusababisha vita vya
mikono mahali pale, basi badala ya ngumi, akaweka vichekesho.
“Ujinga
wa ndoto ni huu, utaota umeokota pesa ukiamka hakuna. Utaota umeokota dhahabu
ukiamka kitandani patupu. Ila ukiota umekojoa, unakuta imooo!”
“Ha!
Ha! Ha!” majitu yalicheka yakishika mbavu.
Kuna
Jitu moja lilisikika likimwambia mkewe, “pesa yangu imekwenda kihalali, pesa
mbili, vicheko lukuki.”
Hayo
ndiyo yakawa maisha ya Bwana Mako na Jitu. Kazi hiyo iliwapatia pesa elfu mbili
kila siku. Pesa hizo ni sawa na shilingi
milioni nne za Kitanzania. Jitu likawa tajiri kama lilivyoahidiwa. Halikulala
tena njaa, maisha yakabadilika.
Bwana
Mako hakusahau kuhusu kurejea nyumbani. Ila, alitaka ashirikiane kwanza na
majitu yale ili aweze kuyafahamu zaidi. Pia, aliendelea kuikarabati ndege yake,
safari hii, hakusahau kuweka kigingi cha nne, pia alifurahishwa na miti ya
kule, ilikuwa migumu kama chuma.
Aliendelea
kufanya maonyesho na kushangiliwa na majitu kila siku mpaka taarifa
zilipomfikia mfalme wa majitu. Ujumbe ukafika haraka, kiumbe kutoka Duniani,
anatakiwa barazani kwa mfalme kabla tonge la kwanza la chakula cha mchana
halijaguswa…”