Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Saba
Akiendelea kushangaa, alishtushwa na sauti ya vishindo, alipotazama mbele, aliona Jitu kubwa refu lipatalo futi hamsini na unene wake ni kama mibuyu miwili. Bwana Mako mwenye futi tano nukta nane, alionekana kiumbe mdogo ilhali Duniani alikotoka yeye ni miongoni mwa watu warefu. Basi kwa kuhofia, alikimbia akajificha nyuma ya mbao mojawapo ya ndege.
“Usijifiche,”
jitu lilisema kwa upole, “nimekuona tangu unadondoka na chombo chako. Siwezi
kukudhuru kiumbe mdogo.”
Bwana
Mako alisogea karibu na Jitu akizungumza, lakini kwa sababu ya ule urefu wake,
Jitu halikuweza kumsikia, hivyo lilimbeba likamweka juu ya bega lake mahali
palipo karibu na sikio mazungumzo yakaendelea.
“Asante
kwa msaada, hapa nipo wapi?” aliuliza Bwana Mako.
“Hapa
ni Mailanda, nchi ya mfalme Solupa, katika bara la pili kati ya matatu yaliyopo
katika sayari yetu isiyo na jina.” Jitu lilijibu. Bwana Mako akagundua kuwa,
ndege yake ilimshusha katika sayari nyingine ya watu hao wakubwa.
Waliendelea
kuzungumza, Bwana Mako alisimulia alivyotengeneza ndege yake na jinsi
alivyosafiri, alisimulia yote bila kuacha kitu. Mwisho jitu liliahidi kumsaidia
kurudi nyumbani, lakini lilimtaka limpeleke nyumbani kwake ili apumzike. Wakati
wanaondoka, lilimuweka Bwana Mako katika mfuko wa shati, kisha likayabeba
mabaki yote ya ndege kwa mkono mmoja na kuanza kutembea kuelekea uliko mji.
Jitu
lilifika nyumbani kwake likiwa limemuweka Bwana Mako mfukoni. Mke wa Jitu
pamoja na watoto wake wawili, walikaa sebuleni. Jitu lilipoingia tu, watoto
walilikimbilia wakifurahi kurejea kwa baba yao. Hata hivyo, Jitu halikuwa na
furaha kwa sababu siku hiyo halikurudi na chochote cha kulisha familia. Kumbe
Jitu lilikuwa masikini!
Jitu
lilisogea mpaka alipokaa mkewe, likamshika mkono wa utosi kuashiria kwamba
halikufanikiwa kupata chochote. Mke wa Jitu asiye na maneno mengi, aliwaamuru
watoto waingie vyumbani kulala kuisubiri kesho.
Bwana
Mako aliyaona yote haya akichungulia kutoka mfukoni mwa shati alimokuwa. Nalo
jitu lilikwenda mpaka katika kitanda kikubwa likakaa na kumtoa.
Bwana
Mako asiye na hofu tena, aliliamuru Jitu limuweke sikioni apate kuliambia
jambo.
“Rafiki
mwema,” Bwana Mako alianza kusema, “nimeona wewe ni masikini, kiasi kwamba huna
chochote cha kulisha wanao. Lakini rafiki, nakuahidi kukufanya tajiri mkubwa
katika jamii yako.”
“Ha!
Ha! Ha!” Jitu lilicheka, “kwa umbo lako, huwezi kufanya kazi yoyote wala jambo
ukaondoa umasikini wangu, nadhani utakuwa umechanganyikiwa kwa sababu ya ile
ajali kiumbe mdogo.”
“Ni
nani huyo unayezungumza naye?” mke wa Jitu aliuliza, kumbe muda wote alikuwa
akimtazama mumewe akiwa katika maongezi.
“Kabla
sijakuambia, niitie watoto ili niwaeleze kwa pamoja habari za huyu kiumbe
mdogo.”
Watoto
walifika na Jitu lilisimulia namna lilivyompata Bwana Mako. Mwisho Bwana Mako
alikwenda kulala na watoto. Walimbeba na kurushiana kwa zamu, isingekuwa
uhodari wao wa kudaka, Bwana Mako angeanguka na kuvunjika mbavu.