Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tisa
Wakati
dada anasimulia, Mfalme aligonga katika chumba kile na kumtaka Malkia aongozane
naye haraka. Basi Malkia akasimama asiyetaka huku akiuliza, “Ikawaje sasa,
niambie haraka niende…”
“Mako
alienda Kwa mfalme…” alijibu dada akiongea haraka, “alipofika kwa mfalme wa
majitu akafanya maonyesho kadhaa yaliyokusanya majitu mengi ajabu. Lile jitu
lililompokea nalo likapewa cheo nyumbani kwa mfalme hata likasahau habari za
umasikini wa awali. Baada ya kuwa amekaa kwa muda wa miaka miwili, Mako akamuomba
mfalme huyo amsaidie kurejea Duniani kwa lengo la kuwatoa hofu ndugu na jamaa
zake ambao wanaweza kudhani kuwa amekufa. Basi Mfalme wa Majitu alimsaidia Mako
kurejea na tangu arejee hajarudi tena huko japo njia anaifahamu.
Alimaliza
dada kusimulia. Wakati huo mfalme alikwisha fungua mlango na kumkamata mkono
Malkia aliyekuwa amesimama kisha akatembea naye haraka kuelekea alikojua yeye.
***
Ilikuwa
mchana siku ya pili Mako akiwa gerezani. Wenzake watatu hawakuwa na hofu,
pengine wao walibakiwa na mvua nyingi zaidi. Katika hali ya kusikitisha mchana
huo, wingu kubwa lilitanda na kuashiria kuwa mvua ingenyesha muda wowote. Maana
yake ni kwamba, Mako angenyongwa siku inayofuata.
Wingu
lilikuwa jeusi hata mchana ule ukabadilika na kuwa kama usiku. Mapigo ya moyo
ya Mako yalibadilika na kudunda kwa kasi. Japo alikuwa shujaa katika jamii
yake, alitawaliwa na hofu. Hofu ya kuuawa.
Upepo
mkali ulivuma, wingu lile likasogezwa polepole kuelekea mashariki. Likasogea
tena na tena mpaka lilipoondoka kabisa katika mji wa Kanakantale. Jua
likaonekana tena. Mako akapumua kwa nguvu asiyeamini kilichotokea.
Hali
ile ilimuogopesha Mako, aliona kama angezubaa basi angeuawa ilhali hakuwa na
hatia. Sasa akapanga mpango wa kutoroka, aliona njia pekee ya kuepuka uonevu
uliotarajiwa kutendwa dhidi yake ilikuwa ni kutoroka gerezani. Alipiga hesabu
zikakamilika. Akasubiri muda wa kufunguliwa vyumbani kwenda kufanya usafi
ufike.
Saa
kumi jioni, wafungwa walitolewa katika vyumba vyao ili wafanye usafi wa mwili
na mazingira. Zoezi hili lilitumia saa mbili pekee hivyo saa kumi na mbili
wangerudishwa katika vyumba.
Mako
alitembea katikati ya Athu, Sipe na Sasi. Hawakuzungumza chochote, walitembea
wakipigana vikumbo na wafungwa wengine.
Walifika
sehemu iliyotumika kwa ajili ya kuoga. Paliwekwa vyungu vingi vikubwa
vilivyojazwa maji, wafungwa wakavua nguo zao na kuanza kuyafurahia maji yale.
Mako hakushughulika na uogaji. Jicho lake lilitembea katika uzio wa gereza. Uzio ulikuwa hatua kumi na sita kutoka aliposimama. Mbele palikuwa na askari mmoja mwanamke. Kwa kuwa uzio ulijengwa kwa miti ya mkonge iliyoacha nafasi, Mako aliweza kuona nje ya gereza. Nje palikuwa na mto uliotiririsha maji. Kuona hivyo, mwanaume akatabasamu.