Jinsi ya Kuwafanya Wanafunzi Wapende Kusoma
Tumezungukwa na wanafunzi wanaotamani kufaulu lakini
hawapendi kusoma. Wengine huomba kufundishwa mada za muhimu zitakazowafanya
wafaulu mitihani yao, ukiona hivyo, tambua mwanafunzi huyo hapendi kusoma. Pia,
hakuna mada za muhimu na zisizo za muhimu. Mada zote ni za muhimu na huenda
zikawa na maswali katika mtihani. Mwanafunzi anayefaulu ni yule anayesoma, iwe
kwa kupenda au kutopenda, ni lazima usome kwani mtihani hupima yale uliyoyaweka
kichwani kwa kusoma.
Walimu wamekuwa wakiniuliza swali juu ya namna ya
kuwafanya wanafunzi wao wapende kusoma. Makala hii ni jibu kwao. Hata wale
wanafunzi wasiopenda kusoma, makala haya yatawasaidia. Yafuatayo ni mambo
yanayoweza kuwafanya wanafunzi wapende kusoma:
1. Onyesha faida ya kile unachowafundisha
Kama unachofundisha hakina faida kwao, wanafunzi hawawezi
kupenda kusoma. Taja faida ya somo au mada katika maisha yao. Mimi nifundishapo
mada mpya katika somo la Kiswahili huanza kwa kusema:
“Mada ya leo inaitwa Utumizi wa Lugha. Mada hii ni muhimu
sana kwenu kwa sababu inawafundisha namna sahihi ya kutumia lugha. Ipo siku
humu ndani, mtakuja kuwa viongozi, mtatakiwa kutumia lugha vizuri ili
mnaowaongoza wawaelewe. Wengine mtakuja kuwa wasemaji wa serikali na taasisi
mbalimbali, pote mnahitaji matumizi mazuri ya lugha. Jambo zuri zaidi ni
kwamba, hata usipopata nafasi ya cheo kikubwa, bado nina uhakika utakuja kuwa
japo msemaji wa familia yako. Unahitaji kuyafahamu matumizi ya lugha. Hivyo,
mada hii ni muhimu kwa kila mmoja wetu.”
Utangulizi huo unamvutia mwanafunzi na kumfanya apende
mada, somo na mwalimu wake. Unamfanya aone kumbe hayupo darasani kupoteza muda,
bali kujipatia maarifa yenye faida lukuki katika maisha yake.
2. Washawishi wapate muda wa kusoma peke
yao
Washauri wanafunzi wakae wasome peke yao, wajulishe kuwa,
wasomapo, wawe na yale yanayohusiana na masomo pekee. Simu na vifaa vingine
visivyo muhimu waviweke mbali.
3. Washauri wanafunzi wafundishane wenyewe
kwa wenyewe
Kupitia kufundishana wenyewe kwa wenyewe, watafurahia
somo. Wataona kama wanaofahamu zaidi hata kupata hadhi ya kuwa walimu. Si hivyo
tu, mwanafunzi anayefundisha wenzake, hukumbuka zaidi na kuelewa masomo kuliko
yule anayefundishwa pekee. Katika kukumbuka, tunakumbuka 10% ya yale
tunayosoma, 20% tunayosikia, 30% tunayoona, 70% tunayojadiliana na wengine, na
tunakumbuka 95% ya yale tunayowafundisha wengine. Hivyo basi, mwanafunzi
anayefundisha wengine, ananafasi ya kukumbuka zaidi masomo.
Mwalimu asikate tamaa, awe mpole kwa wakati wote na
ajitahidi kuwasaidia wanafunzi kupenda kusoma. Kuwafanya wanafunzi wapende
kusoma, ni jambo gumu, linalohitaji muda, upendo na bidii.